Matayo 14 - Swahili Congo Revised Bible 2002

Yesu anawaziwa kuwa Yoane Mubatizaji(Mk 6.14-29; Lk 9.7-9)

1Katika siku zile, Herode, liwali wa jimbo la Galilaya, akasikia habari za Yesu.

2Halafu akawaambia wasimamizi waliokuwa chini yake: “Mutu huyu ni Yoane Mubatizaji aliyefufuka! Ni kwa sababu hii amepata uwezo wa kufanya miujiza.”

3Herode alikuwa amemukamata Yoane akamufunga minyororo na kumutia ndani ya kifungo. Herode alifanya vile kwa sababu ya Herodia, muke wa ndugu yake Filipo.

4Naye Yoane alikuwa amemwambia Herode kwamba hana sheria ya kumwoa yule muke wa ndugu yake.

5Herode alitaka kumwua Yoane, lakini aliwaogopa watu kwa maana wote walimuhesabia Yoane kuwa nabii.

6Na ilikuwa kwa sikukuu ya kuzaliwa kwa Herode, binti ya Herodia akacheza mbele ya wote walioalikwa. Binti yule akamupendeza Herode sana

7hata akamwahidi kwa kiapo kwamba atamupa kitu chochote atakachomwomba.

8Na kwa ajili ya kusukumwa na mama yake, yule binti akamwambia Herode: “Unipe hapa hapa ndani ya sahani kichwa cha Yoane Mubatizaji!”

9Mutawala huyu akahuzunika, lakini kwa sababu ya viapo alivyotoa na kwa sababu ya waalikwa, akaamuru binti yule apewe kichwa kile.

10Basi akaamuru waende kukata kichwa cha Yoane ndani ya kifungo.

11Halafu wakaleta kile kichwa chake ndani ya sahani na kukitoa kwa yule binti, naye akakipeleka kwa mama yake.

12Wanafunzi wa Yoane wakakuja kubeba maiti yake na kuizika. Nao wakaenda kumwelezea Yesu habari ile.

Yesu anakulisha watu elfu tano(Mk 6.30-44; Lk 9.10-17; Yn 6.1-14)

13Yesu aliposikia habari hii, akaondoka pale ndani ya chombo, na kwenda peke yake kwa pahali penye ukiwa. Nayo makundi ya watu waliposikia vile, wakatoka katika miji yao na kumufuata Yesu kwa miguu.

14Yesu alipotoka ndani ya chombo, akaona kundi kubwa la watu, naye akawasikilia huruma, akawaponyesha wale waliokuwa wagonjwa kati yao.

15Na ilipokuwa magaribi, wanafunzi wake wakamufikia na kumwambia: “Hapa ni pori na sasa ni magaribi. Uage kundi hili kusudi waende katika vijiji kwa kujinunulia vyakula.”

16Lakini Yesu akawajibu: “Si lazima waende; ninyi wenyewe muwape chakula.”

17Lakini wao wakamujibu: “Hapa tuko tu na mikate mitano na samaki mbili.”

18Yesu akawaambia: “Muvilete hapa.”

19Kisha kuwaamuru watu waikae juu ya majani, Yesu akatwaa ile mikate mitano na samaki mbili, akainua macho mbinguni, akamushukuru Mungu. Akamega ile mikate, akawapa wanafunzi wake, nao wakaigawanya kwa kundi la watu.

20Watu wote wakakula na kushiba. Kisha wanafunzi wakaokota vipande vya mikate vilivyobaki, wakajaza vitunga kumi na viwili.

21Hesabu ya watu waliokula ilikuwa yapata wanaume elfu tano, pasipo kuhesabu wanawake na watoto.

Yesu anatembea juu ya maji(Mk 6.45-52; Yn 6.15-21)

22Mara moja kisha mambo hayo, Yesu akawalazimisha wanafunzi wake waingie ndani ya chombo na kumutangulia ngambo ingine ya ziwa. Kwa wakati ule yeye alibaki akiaga lile kundi la watu.

23Kisha kuagana nao, akapanda kwenye kilima peke yake kwa kuomba. Na giza lilipoingia, alikuwa angali kule peke yake,

24lakini chombo kilikuwa kimekwisha kufika mbali sana na inchi kavu, kikirushwarushwa na zoruba, kwa maana upepo ulikuwa ukitokea mbele.

25Ilipokuwa karibu na mapambazuko, Yesu akawafikia wanafunzi wake, akitembea juu ya maji.

26Nao walipomwona akitembea juu ya maji wakashikwa na hofu, wakisema: “Ni muzimu!” Nao wakaanza kulalamika kwa ajili ya woga.

27Lakini mara moja Yesu akasema nao, akiwaambia: “Mujipe moyo, ni mimi! Musiogope!”

28Basi Petro akamwambia: “Bwana, ikiwa kweli ni wewe, utoe amri kusudi nifike pale unapokuwa, nikitembea juu ya maji.”

29Naye Yesu akamujibu: “Kuja.”

Halafu Petro akatoka ndani ya chombo, akaanza kutembea juu ya maji kumufikia Yesu.

30Lakini alipoona upepo, akaogopa, na kwa vile alivyoanza kuzama ndani ya maji, akalalamika akisema: “Bwana, uniokoe!”

31Mara moja Yesu akanyoosha mukono, akamushika na kumwambia: “Ee wewe mwenye imani ndogo! Kwa sababu gani uliona shaka?”

32Nao wote wawili walipopanda ndani ya chombo, upepo ukatulizana.

33Basi wanafunzi waliokuwa ndani ya chombo wakapiga magoti mbele ya Yesu, wakisema: “Kweli wewe ni Mwana wa Mungu!”

Yesu anaponyesha wagonjwa(Mk 6.53-56)

34Walipokwisha kuvuka ziwa, wakafika pande za Genezareti.

35Na watu wa kule walipomutambua Yesu, wakatuma habari katika sehemu zile zote. Halafu wakamuletea wagonjwa wote

36na kumusihi awaruhusu waguse hata upindo wa nguo yake tu. Nao wote waliougusa walipona.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help