Mezali 2 - Swahili Congo Revised Bible 2002

Mafaa ya hekima

1Mwana wangu, ukikubali maneno yangu,

na kushika maagizo yangu,

2ukitega sikio lako kwa kusikiliza hekima,

na kuelekeza moyo wako upate ufahamu,

3ukiomba upewe akili,

ukisihi upewe ufahamu,

4ukitafuta hekima kama feza,

na kuitaka kama hazina iliyofichwa,

5utaelewa maana ya kumwogopa Yawe,

utafahamu maana ya kumujua Mungu.

6Maana Yawe anawapa watu hekima;

katika kinywa chake kunatoka maarifa na ufahamu.

7Anawawekea watu wa usawa akiba ya hekima safi,

yeye ni ngao kwa watu wanaoishi kwa ukamilifu.

8Analinda mienendo ya watu wanaofuata sheria yake,

na kuchunga njia za waaminifu wake.

9Ukinisikiliza,

utafahamu haki, usawa, na kufuata sheria ya Mungu;

utafahamu kila njia nzuri.

10Maana hekima itaingia ndani ya moyo wako,

na maarifa yatapendeza nafsi yako.

11Hekima itakulinda,

ufahamu utakuchunga;

12vitakuepusha na njia ya uovu,

na watu wa maneno mapotovu,

13watu wanaoacha njia zenye kunyooka

kwa kufuata njia za giza,

14watu wanaofurahia kutenda maovu

na kupendezwa na upotovu wa maovu,

15watu ambao mienendo yao imepotoka,

nazo njia zao haziaminiki.

16Utaepukana na mwanamuke mwasherati,

mwanamuke kahaba wa maneno matamu,

17mwanamuke anayemwacha mwenzake wa ujana wake,

na kusahau agano la Mungu wake.

18Nyumba yake inaelekea kifo,

njia zake zinakwenda kuzimu.

19Yeyote anayemwendea harudi hata kidogo,

wala harudilii tena njia ya uzima.

20Kwa hiyo utafuata mufano wa watu wazuri,

na kufuata mienendo ya wenye haki.

21Maana watu wa usawa watarizi inchi,

na watu wakamilifu watadumu ndani yake.

22Lakini waovu wataondolewa katika inchi,

na watu wabaya watangolewa toka ndani yake.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help