1Ukumbuke, ee Yawe, mambo yaliyotupata!
Utuangalie, uone haya yetu!
2Inchi yetu imepewa kwa wageni,
nyumba zetu kwa watu wengine.
3Tumekuwa wayatima, bila baba,
wamama zetu ni kama wajane.
4Maji yetu tunayapata kwa feza,
kuni zetu kwa kuzinunua.
5Tunalazimishwa kufanya kazi kama punda,
tumechoka, lakini haturuhusiwi kupumzika.
6Tumewanyooshea Wamisri na Waasuria mikono,
kusudi tupate chakula cha kutosha.
7Babu zetu walitenda zambi na sasa hawako tena;
nasi tunabeba makosa yao.
8Watumwa wanatutawala,
wala hakuna wa kutuokoa toka katika mikono yao.
9Chakula chetu tunakipata kwa kuhatarisha maisha yetu,
maana wauaji wanazungukazunguka katika jangwa.
10Ngozi zetu zinawaka moto kama furu,
kwa sababu ya njaa inayotuchoma.
11Wanawake wetu wanatendewa kwa kinguvu katika Sayuni,
na wabinti wetu katika miji ya Yuda.
12Wakubwa wetu wametundikwa kwa mikono yao;
wazee wetu hawapewi heshima yoyote.
13Vijana wanalazimishwa kusaga ngano kwa mawe,
watoto wanayumbayumba kwa mizigo ya kuni.
14Wazee wameacha kutoa mashauri yao,
vijana wameacha kuimba.
15Furaha ya mioyo yetu imetoweka,
michezo yetu imegeuzwa kuwa maombolezo.
16Taji tuliojivunia imeanguka.
Ole kwetu maana tumetenda zambi!
17Kwa ajili ya hiyo tumeugua ndani ya moyo,
kwa ajili ya hiyo macho yetu yamefifia.
18Maana mulima Sayuni umeachwa utupu,
mbweha wanazungukazunguka humo.
19Lakini wewe Yawe unatawala milele,
kiti chako cha kifalme kinadumu kwa vizazi vyote.
20Sababu gani umetusahau kwa muda murefu hivyo
na kutuacha siku nyingi hivyo?
21Utugeuze, ee Yawe,
kusudi tukurudilie.
Uturudishie hali ya zamani.
22Au, umetukataa kabisa?
Umetukasirikia sana?
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.