1Daudi alimwimbia Yawe wimbo huu siku ile Yawe alipomukomboa toka katika mikono wa waadui zake, na toka katika mukono wa Saulo.
2Alisema:
Yawe ni:
kikingio changu,
kimbilio langu,
mukombozi wangu,
3Mungu wangu,
yule ambaye ninamukimbilia,
ngao yangu,
nguvu ya wokovu wangu,
munara wangu,
kimbilio langu.
Mwokozi wangu, unaniokoa kutoka watesaji wakali!
4Ninamwita Yawe anayestahili sifa anisaidie,
nami ninaokolewa kutoka kwa waadui zangu.
5Mawimbi ya kifo yalinizunguka,
mafuriko ya maangamizi yalinishambulia,
6kamba za kuzimu zilinizunguka,
mitego ya kifo ilikuwa mbele yangu.
7Katika taabu yangu,
nilimwita Yawe;
nilimwita Mungu wangu.
Toka katika hekalu lake alisikia sauti yangu;
kilio changu kilifika katika masikio yake.
8Halafu, dunia ikatetemeka na kutikisika,
misingi ya mbinguni ikayumbayumba na kuruka,
kwa maana Mungu alikuwa amekasirika.
9Moshi ulifuka kutoka katika pua yake,
moto wenye kuteketeza ukatoka katika kinywa chake,
makaa ya moto yakatokea.
10Aliinamisha anga, akashuka chini,
na wingu jeusi lilikuwa chini ya miguu yake.
11Alipanda juu ya kerubi na kuruka;
akaruka juu ya mabawa ya upepo.
12Alijifunika giza pande zote;
kifuniko chake kilikuwa mawingu mazito ya mvua.
13Umeme ulimetameta mbele yake,
makaa ya moto yakawaka.
14Yawe alinguruma kutoka mbinguni;
Mungu Mukubwa akatoa sauti yake.
15Aliwapiga waadui mishale, akawatawanya;
alirusha umeme, akawakimbiza.
16Yawe alipovikaripia,
pumzi ya pua yake
ilifunua vilindi vya bahari
na misingi ya dunia ikaonekana.
17Mungu alinyoosha mukono wake kutoka juu, akanitwaa,
alininyanyua kutoka ndani ya maji mengi.
18Aliniokoa kutoka adui yangu mwenye nguvu,
kutoka hao walionichukia na kuwa na nguvu kunishinda.
19Walinishambulia nilipokuwa katika taabu,
lakini Yawe alinikinga.
20Alinileta, akaniweka kwenye nafasi ya usalama;
aliniponyesha kwa sababu alipendezwa nami.
21Yawe alinitendea kwa kadiri ya haki yangu;
alinilipa kwa vile mikono yangu haina kosa.
22Maana nimefuata njia za Yawe,
wala sikujitenga na Mungu wangu kwa ajili ya uovu.
23Nimeshika maagizo yake yote,
sikuacha kufuata masharti yake.
24Mbele yake nilikuwa mukamilifu,
nimejikinga nisikuwe na kosa.
25Yawe amenilipa kwa kadiri ya haki yangu,
kwa kadiri ya usafi wangu mbele yake.
26Wewe ni mwema kwa wema,
mukamilifu kwa wakamilifu,
27bila kosa kwa wale ambao hawafanyi makosa,
lakini mukali kwa waovu.
28Wewe unawaokoa wanyenyekevu,
lakini unaangalia wenye majivuno kusudi uwashushe.
29Ee Yawe, wewe ni taa yangu.
Yawe anafanya giza langu likuwe mwangaza.
30Kwa musaada wako, ninashinda kundi la waaskari;
kwa musaada wa Mungu wangu, ninaruka kuta.
31Matendo ya Mungu ni makamilifu.
Ahadi ya Yawe ni ya kuaminika.
Yeye ni ngao kwa wote wanaomukimbilia.
32Nani anayekuwa Mungu isipokuwa Yawe?
Nani anayekuwa kikingio isipokuwa Mungu wetu?
33Ni Mungu ambaye ananipatia nguvu,
na anaifanya salama njia yangu.
34Ameiimarisha miguu yangu kama ya swala,
na kunilinda salama juu ya milima.
35Ananifundisha kupigana vita,
mikono yangu iweze kuvuta upinde wa shaba.
36Umenipa ngao yako ya kuniokoa;
umenifanikisha kwa wema wako.
37Umepanua njia yangu
wala miguu yangu haikuteleza.
38Niliwafuata waadui zangu na kuwaangamiza;
sikurudi nyuma mpaka wamemalizika.
39Niliwamaliza kabisa.
Hawakuinuka tena;
walianguka chini ya miguu yangu.
40Wewe ulinijalia nguvu ya kupigana vita;
uliwaporomosha waadui chini yangu.
41Uliwakimbiza waadui zangu,
na wale walionichukia niliwaangamiza.
42Walitafuta musaada, lakini hakukukuwa wa kuwasaidia;
walimulilia Yawe, lakini hakuwajibu.
43Niliwatwanga, wakakuwa kama mavumbi,
nikawaponda na kuwakanyaga kama matope katika barabara.
44Wewe uliniokoa na mashambulizi ya watu wangu,
ukanichunga kuwa mutawala wa mataifa.
Watu nisiowajua walinitumikia.
45Wageni walinifikia wakinyenyekea;
waliposikia tu habari zangu, walinitii.
46Wageni walivunjika moyo;
wakakuja kutoka makimbilio yao wakitetemeka.
47Yawe anaishi!
Asifiwe yeye kikingio changu!
Atukuzwe Mungu, kikingio na mwokozi wangu.
48Yeye ameniwezesha kulipiza kisasi,
ameweka mataifa chini yangu.
49Ameniokoa kutoka waadui zangu.
Ee Yawe, ulinitukuza juu ya wapinzani wangu
na kuniponyesha kutoka watesaji wakali.
50Kwa hiyo, nitakutukuza kati ya mataifa;
nitaliimbia sifa jina lako.
51Mungu anamujalia mufalme wake ushindi mukubwa;
anamutendea mema muchaguliwa wake, ndiye Daudi na wazao wake milele.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.