1Kiebrania: Kwa mukubwa wa waimbaji: kwa mutindo wa wimbo “Usiharibu”. Mashairi ya Daudi wakati Saulo alipotuma wapelelezi wamwue.
2Ee Mungu wangu,
uniokoe kutoka waadui zangu,
unikinge na hao wanaonishambulia.
3Uniokoe na hao wanaotenda maovu,
Uniponyeshe kutoka hao wauaji!
4Angalia! Wananivizia waniue.
Watu wakali wanachochea ugomvi juu yangu
ingawa sikufanya ubaya wowote.
5Ingawa sina kosa,
wanakimbia, ee Yawe, kujiweka tayari.
Uinuke, ee Yawe,
uwaangalie na kunisaidia!
6Uinuke, ee Yawe,
Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli.
Uamuke, uwaazibu hao watu wasiokujua;
usiwaache hao waasi na wabaya.
7Kila magaribi waadui hao wanarudi
wakifoka kama imbwa,
na kuzungukazunguka katika muji.
8Angalia, ni matusi tu yanayotoka katika midomo yao,
maneno yao ni kama panga kali;
tena wanafikiri hakuna anayewasikia.
9Lakini wewe, ee Yawe, unawachekelea;
unawazarau hao watu wasiokujua.
10Nitakungojea, ewe unayekuwa nguvu yangu;
maana wewe, ee Mungu, ni kimbilio langu.
11Mungu wangu mwema sana atakuwa mbele yangu,
ataniwezesha kuwaona waadui zangu wameshindwa.
12Usiwaue mara moja, watu wangu wasisahau;
uwasambazesambaze kwa nguvu yako, uwaporomoshe chini.
Ee Bwana, wewe ndiwe ngao yetu!
13Wao wanatenda zambi katika masemi yao yote,
kwa hiyo wanaswe katika kiburi chao!
Kwa sababu ya laana na uongo wao,
14uwateketeze kwa hasira yako,
uwateketeze watoweke kabisa,
kusudi watu wote wajue mpaka kwa miisho ya dunia
ya kuwa wewe Mungu unatawala wazao wa Yakobo.
15Kila magaribi waadui hao wanarudi
wakifoka kama imbwa,
na kuzungukazunguka katika muji.
16Wanapitapita huko na huko wakitafuta chakula,
nao wasiposhiba wananguruma.
17Lakini mimi nitaimba sifa za nguvu yako,
nitashangilia asubui juu ya wema wako,
maana wewe umekuwa kikingio changu,
wewe ni kimbilio langu wakati wa taabu.
18Ewe unayekuwa nguvu yangu, nitakuimbia sifa;
ee Mungu, wewe ni kikingio changu,
Mungu anayenitendea mema!
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.