Ezekieli 5 - Swahili Congo Revised Bible 2002

Ezekieli ananyoa nywele zake

1Yawe aliniambia hivi: Wewe mwanadamu, utwae upanga mukali, uutumie kama wembe wa kinyozi. Unyoe kichwa na ndevu zako. Kisha utwae mizani, upime nywele zako na kuzigawanya kwa sehemu mbalimbali.

2Kisha kutimia kwa wakati wa kushambuliwa kwa muji wa Yerusalema, utachoma sehemu moja ya tatu ya nywele zako katikati ya muji. Sehemu ingine moja ya tatu utaikatakata kwa upanga ukiuzunguka muji. Sehemu ya tatu ya mwisho utaipeperusha kwa upepo, nami nitauchomoa upanga wangu na kuwafuatilia nyuma.

3Lakini utatwaa sehemu ndogo tu ya nywele zako na kuifungia kwenye upindo wa nguo yako.

4Utwae vilevile nywele kidogo uzitupe ndani ya moto na kuziteketeza. Moto utatokea humo na kuteketeza watu wote wa Israeli.

5Bwana wetu Yawe anasema hivi: Ndivyo itakavyokuwa juu ya Yerusalema. Mimi niliuweka kuwa katikati ya mataifa, umezungukwa na inchi za kigeni pande zote.

6Lakini wakaaji wake wameyaasi maagizo na masharti yangu, wakakuwa wabaya kuliko mataifa na inchi zinazowazunguka. Kweli, wameyakataa maagizo yangu na kuacha kuyafuata masharti yangu.

7Kwa hiyo, Bwana wetu Yawe anasema hivi: Ninyi ni waasi kuliko mataifa yanayowazunguka, hamukuishi kulingana na masharti yangu, wala hamukuyashika maagizo yangu, lakini mumetenda kulingana na maagizo ya mataifa yanayowazunguka.

8Basi, Bwana wetu Yawe anasema hivi: Nitapingana nanyi nami nitatimiza hukumu zangu juu yenu mbele ya mataifa.

9Kutokana na machukizo yenu yote nitawaazibu kwa azabu ambayo sijapata kuwapa ninyi na ambayo sitairudilia tena.

10Hukohuko katika muji wazazi watawakula watoto wao wenyewe na watoto watawakula wazazi wao. Nitatimiza hukumu zangu juu yenu na watakaobaki wazima nitawasambaza pande zote.

11Kwa hiyo, kama vile ninavyoishi, –ni ujumbe wa Bwana wetu Yawe– kwa vile mumechafua Pahali Patakatifu pangu, kwa matendo yenu mabaya na machukizo yenu, mimi nitawaangamiza bila huruma na bila kumwacha mutu yeyote.

12Sehemu moja ya tatu ya watu wako, ee Yerusalema, itakufa kwa ugonjwa mukali na kwa njaa. Sehemu ingine moja ya tatu itakufa katika vita. Na sehemu moja ya tatu inayobaki nitaisambaza pande zote za dunia na nitachomoa upanga wangu na kuwafuatilia nyuma.

13Ndivyo nitakavyomaliza hasira yangu, nami nitakuwa nimetuliza kasirani yangu na kufarijika ndani ya moyo. Hapo ndipo watakapojua kwamba mimi, Yawe, nimewaazibu kwa sababu ya wivu wangu kwa ukosefu wenu wa uaminifu.

14Tena, wewe Yerusalema nitakufanya kuwa ukiwa na kitu cha kuchekelewa kati ya mataifa yanayokuzunguka na mbele ya watu wote wanaopita karibu nawe.

15Utakuwa kitu cha kuzarauliwa na cha haya, mufano wa kitu cha kuchukiza kwa makabila yanayokuzunguka, wakati nitakapotimiza hukumu zangu juu yako kwa hasira na kasirani yangu kali. Ni mimi Yawe ninayasema hivyo.

16Wakati huo nitaiachilia mishale yangu mikali ya njaa iwachome na kuangamiza wakaaji wako. Nitawafanya wakufe na njaa kwa kuiharibu akiba yao ya chakula.

17Nitakutumia njaa na nyama wakali ambao wataua watoto wako; magonjwa makali, mauaji, na vita itakuja kukuangamiza. Ni mimi, Yawe, ninayesema hivyo.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help