Hesabu 23 - Swahili Congo Revised Bible 2002

1Balamu akamwambia Balaki: Unijengee mazabahu saba hapa kisha uniletee ngombe dume saba na kondoo dume saba.

2Balaki akafanya kama vile Balamu alivyosema. Basi, wakatolea juu ya kila mazabahu ngombe dume mumoja na kondoo dume mumoja.

3Halafu Balamu akamwambia Balaki: Baki hapa karibu na sadaka yako ya kuteketezwa kwa moto, nami niende. Labda Yawe atakutana nami. Chochote atakachonionyesha nitakuja kukuambia. Basi, Balamu akaenda peke yake juu ya kilele cha mulima.

4Mungu akakutana naye. Balamu akamwambia: Nimetayarisha mazabahu saba na kutoa ngombe dume mumoja na kondoo dume mumoja juu ya kila mazabahu.

5Yawe akamupa Balamu maneno atakayosema na kumwambia arudi kwa Balaki.

6Balamu akarudi, akamukuta Balaki akisimama palepale karibu na sadaka yake ya kuteketezwa kwa moto, pamoja na wakubwa wote wa Moabu.

7Balamu akamutolea Balaki mashairi yake, akasema:

Balaki amenileta hapa kutoka Aramu,

hakika, mufalme wa Moabu amenileta kutoka milima ya mashariki:

Kuja uwalaani watu wa Yakobo kwa ajili yangu,

hakika, kuja uwakaripie Waisraeli!

8Nitamulaani namna gani mutu ambaye Mungu hakumulaani?

Nitawakaripia watu ambao Yawe hakuwakaripia?

9Kutoka vilele vya mawe makubwa ninawaona,

kutoka juu ya milima nawachungulia,

hilo taifa linalokaa peke yake,

lisilojiona kuwa sawa na mataifa mengine.

10Nani anayeweza kuhesabu wingi wa watu wa Yakobo,

au kuhesabu makundi ya Waisraeli?

Nikufe kifo cha haki,

mwisho wangu ukuwe kama wao.

11Kwa hiyo, Balaki akamwambia Balamu: Umenifanyia nini? Nimekuleta hapa uwalaani waadui zangu, lakini pahali pake umewabariki!

12Balamu akamwambia Balaki: Hainipasi tu kusema maneno Yawe aliyoweka ndani ya kinywa changu?

Unabii wa pili wa Balamu

13Kisha, Balaki akamwambia Balamu: Tuende pahali pengine ambapo utaweza kuwaona; hata hivyo utaona tu sehemu yao, hautaweza kuwaona wote. Kisha uwalaani kutoka huko kwa ajili yangu.

14Basi, Balaki akamutwaa Balamu kwenye shamba la Sofimu, juu ya kilele cha mulima Pisiga. Hapo akajenga mazabahu saba na kutoa juu ya kila mazabahu ngombe dume mumoja na kondoo dume mumoja.

15Balamu akamwambia Balaki: Baki hapa karibu na sadaka yako ya kuteketezwa kwa moto, nami niende kule ngambo kukutana na Yawe.

16Yawe akakutana na Balamu, akamupa maneno atakayosema, na kumwambia arudi kwa Balaki.

17Basi, Balamu akarudi, akamukuta Balaki amesimama karibu na sadaka ya kuteketezwa pamoja na wakubwa wote wa Moabu. Balaki akamwuliza: Yawe amekuambia nini?

18Halafu, Balamu akamutolea Balaki mashairi yake:

Simama, Balaki, usikie!

Unisikilize, ewe mwana wa Sipori!

19Mungu si mutu, hata aseme uongo,

wala si mwanadamu, hata abadilishe nia yake!

Ataahidi kitu na asikifanye,

au kusema kitu asikitimize?

20Nimepewa amri ya kubariki,

naye amebariki wala siwezi kuigeuza.

21Yawe hajaona ubaya kwa watu wa Yakobo,

wala uovu kwa hao watu wa Israeli.

Yawe Mungu wao yuko pamoja nao,

Yeye anasifiwa kwa vigelegele kati yao,

yeye anapokea sifa zao za kifalme.

22Mungu aliyewatoa kutoka Misri,

anawapigania kwa nguvu kama za mbogo.

23Hakika ulozi hauwezi kuwapinga watu wa Yakobo,

wala uchawi juu ya watu wa Israeli.

Sasa juu ya Israeli, watu watasema:

Muangalie maajabu Mungu aliyotenda!

24Angalia! Waisraeli wameinuka kama simba dike,

wanasimama kama simba dume.

Ni kama simba asiyelala mpaka amalize windo lake,

na kunywa damu ya windo.

25Halafu Balaki akamwambia Balamu: Basi, usiwalaani wala usiwabariki kabisa!

26Lakini Balamu akamujibu Balaki: Sikukuambia kwamba kile Yawe anachosema ndicho ninachopaswa kufanya?

27Balaki akamwambia Balamu: Kuja, nitakupeleka pahali pengine. Labda Mungu atakubali uwalaani watu hao kutoka huko kwa ajili yangu.

28Basi, Balaki akamupeleka Balamu mpaka kwenye kilele cha mulima Peori, ambapo mutu akisimama anaona katika jangwa.

29Balamu akamwambia Balaki: Unijengee mazabahu saba hapa, unitayarishie ngombe dume saba na kondoo dume saba.

30Balaki akafanya kama vile alivyoambiwa na Balamu, kisha akatoa juu ya kila mazabahu ngombe dume mumoja na kondoo dume mumoja.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help