Zaburi 9 - Swahili Congo Revised Bible 2002

Shukrani kwa Mungu

1Kwa mukubwa wa waimbaji. Kwa mutindo wa wimbo “Kilio cha mwana.”

2Nitakushukuru wewe Mungu kwa moyo wangu wote;

nitayaeleza matendo yako yote ya ajabu.

3Nitafurahi na kushangilia kwa ajili yako;

nitaliimbia sifa jina lako, ewe Mungu Mukubwa.

4Waadui zangu walirudi nyuma,

walijikwaa na kuangamia mbele yako.

5Umeitetea haki yangu katika maneno yangu;

umeikaa katika kiti chako cha kifalme,

wewe mwamuzi wa haki.

6Umeyakaripia mataifa,

umewaangamiza waovu;

umeyafuta majina yao kwa milele.

7Waadui wameangamia milele;

umeiongoa miji yao,

ukumbusho wao umetoweka.

8Lakini Yawe anatawala milele;

ameweka kiti chake cha kifalme, apate kuhukumu.

9Anauhukumu ulimwengu kwa haki;

anayaamua mataifa kama vile inavyofaa.

10Yawe ni kikingio cha watu wanaoonewa;

yeye ni kikingio katika nyakati za taabu.

11Wanaojua jina lako, wanakutegemea,

kwa maana wewe, ee Yawe, hauwatupi wanaokutafuta.

12Mumwimbie sifa Yawe anayekaa Sayuni!

Muyatangazie mataifa mambo aliyotenda!

13Mungu analipiza kisasi cha damu iliyomwangwa;

wala hasahau hata kidogo kilio cha wenye kuonewa.

14Ee Yawe,

wewe unayeniopoa kutoka nguvu za kifo,

uangalie mateso wale wanaonichukia wanayoniletea

na kunirehemu

15kusudi nitangaze sifa zako mbele ya watu wa Sayuni,

nipate kushangilia kwa sababu umeniokoa.

16Mataifa yameanguka katika shimo walilochimba,

miguu yao imenaswa kwenye wavu waliotega.

17Yawe amejitambulisha;

anatoa hukumu.

Waovu wamenaswa kwa matendo yao wenyewe.

18Waovu wataishia katika kuzimu;

ndiyo mataifa yote yanayomusahau Mungu.

19Lakini wakosefu hawatasahauliwa siku zote;

tumaini la wamasikini halitapotea milele.

20Ee Yawe,

simama sasa mwanadamu asishinde!

Uyakusanye sasa hivi mataifa mbele yako, uyahukumu.

21Uyatie hofu, ee Yawe,

watu wa mataifa watambue kwamba wao ni watu tu!

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help