Yobu 30 - Swahili Congo Revised Bible 2002

1Lakini sasa watu wananichekelea,

tena watu wanaokuwa wadogo kuliko mimi;

watu ambao niliwaona baba zao hawafai

hata kuwahesabu kama imbwa wangu wakilinda kondoo.

2Ningepata faida gani katika mikono yao,

watu ambao nguvu zao zilikuwa zimewaishia?

3Katika ukosefu na njaa kali

walitafutatafuta kitu cha kutafuna katika jangwa,

sehemu tupu zisizokuwa na chakula.

4Walichuma mimea katika jangwa na majani katika pori wakakula,

walikula hata mizizi ya muti wa vifagio.

5Walifukuzwa mbali na watu,

watu waliwapigia kelele kama wezi.

6Iliwapasa kutafuta usalama katika mifereji kwenye maporomoko,

katika mashimo ndani ya udongo na mawe.

7Kule katika vichaka walilia kama nyama,

walikusanyika pamoja chini ya nyasi.

8Walikuwa wapumbafu wakubwa na waovu

ambao walilazimishwa kufukuzwa katika inchi kwa fimbo.

9Na sasa wamenitungia wimbo wa kunizomea,

nimekuwa kitu cha kuchekesha kwao.

10Wananichukia na kuniepuka;

wakiniona tu wanatema mate kwenye uso.

11Kwa maana Mungu ameniregeza na kunishusha,

wamekuwa huru kunitendea wanavyopenda.

12Kundi la watu linasimama kwa kunishitaki,

likitafuta kuniangusha kwa kunitegea.

Linanishambulia kusudi niangamie.

13Watu hao wanakata njia yangu,

wanazidisha hasara yangu,

na hakuna mutu wa kuwazuia.

14Wanakuja kama kwenye njia kubwa,

na kisha mashambulio wanasonga mbele.

15Hofu kubwa imenishika.

Heshima yangu imetoweka kama kwa upepo,

na raha yangu imepita kama wingu.

16Sasa sina nguvu yoyote ndani ya nafsi yangu;

siku za mateso zimenipata.

17Usiku mifupa yangu yote inauma;

maumivu yanayonitafuna hayapoi.

18Mungu amenishika kwa nguo zangu,

amenibana kama shingo ya kanzu yangu.

19Amenitupa katika matope;

nimekuwa kama majivu na mavumbi.

20Ninakulilia, lakini haunijibu,

ninasimama kuomba lakini haunisikilizi.

21Umegeuka kuwa mukali kwangu,

unanitesa kwa mukono wako wenye nguvu.

22Unanitupa katika upepo na kunipeperusha;

unanitupatupa huku na kule katika zoruba kali.

23Kweli! Ninajua utanipeleka tu katika kifo,

pahali wote wanaoishi watakapokutana.

24Basi, mutu akiangamia hainui mukono?

Mutu akiwa tabani haombi musaada?

25Sikuwalilia wale waliokuwa na taabu?

Sikuona uchungu kwa ajili ya wamasikini?

26Lakini nilipotazamia mazuri, mabaya yalinipata;

nilipongojea mwangaza, giza lilikuja.

27Moyo wangu unahangaika wala hautulii hata kidogo.

Siku za mateso zimenipata.

28Ninapitapita nikiomboleza.

Kwangu hakuna jua.

Ninasimama katika makutano kuomba musaada.

29Kwa kilio nimekuwa ndugu ya imbwa wa pori,

kati ya mimi na mbuni hakuna tofauti.

30Ngozi yangu inakuwa nyeusi na inachubuka,

mifupa yangu inaungua kwa homa.

31Kinubi changu kimekuwa cha kufanya kilio

filimbi yangu kwa ajili ya kuomboleza.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help