1Zaburi ya Daudi, inayoelekea sadaka yake ya ukumbusho.
2Ee Yawe,
usiniazibu kwa hasira yako,
usiniadibishe kwa kasirani yako.
3Mishale yako imenichoma;
mukono wako umenigandamiza.
4Hakuna uzima katika mwili wangu,
kwa sababu umenikasirikia.
Hakuna afya hata katika mifupa yangu,
kwa sababu ya zambi yangu.
5Nimefunikwa kabisa na zambi zangu,
zinanilemea kama muzigo muzito sana.
6Vidonda vyangu vimeoza na kunuka,
na hayo ni matokeo ya ujinga wangu.
7Nimepinduka mpaka chini na kupondekana;
muchana kutwa ninazunguka nikiomboleza.
8Viungo vyangu vimeshambuliwa na homa;
hakuna uzima katika mwili wangu.
9Nimeregea na kupondekanapondekana;
ninaugua kwa kusongwa katika moyo.
10Yawe, wewe unajua mahitaji yangu yote;
sifichi kilio changu mbele yako.
11Moyo wangu unapigapiga, nguvu zimeniishia;
hata macho yangu nayo yamekwisha fifia.
12Warafiki na wenzangu wanaepuka kuona mateso yangu,
na wandugu zangu wanakaa mbali nami.
13Wanaotaka kuniua wanatega mitego yao;
wanaonitakia niumie wanakusudia kuniangamiza.
Muchana kutwa wanafanya mipango juu yangu.
14Lakini mimi nimekuwa kama kiziwi, sisikii;
nimekuwa kama bubu asiyeweza kusema kitu.
15Kweli, nimekuwa kama mutu asiyesikia,
kama mutu asiyekuwa na chochote cha kujitetea.
16Lakini ninakutumainia wewe, ee Yawe;
wewe, ee Yawe, Mungu wangu, ndiwe utakayenijibu.
17Ninakuomba tu waadui wasinisimange,
wasijitukuze juu ya kuanguka kwangu.
18Mimi ni karibu ya kuanguka;
ninakuwa na maumivu ya siku zote.
19Ninaungama uovu wangu;
zambi zangu zinanisikitisha.
20Waadui zangu ni wazima, wana nguvu,
ni wengi sana hao wanaonichukia bure.
21Hao wanaonilipa mabaya kwa mazuri,
wananipinga kwa sababu ninatenda mazuri.
22Usinitupe, ee Yawe;
ee Mungu wangu, usikae mbali nami.
23Ukuje haraka kunisaidia,
ewe Yawe, mwokozi wangu.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.