1Maombi ya mutu anayekuwa katika taabu ambaye anamutolea Yawe malalamiko yake.
2Ee Yawe,
usikie maombi yangu,
na kilio changu kikufikie.
3Usijifiche mbali nami wakati wa taabu!
Unitegee sikio lako,
unijibu upesi wakati ninapokuomba!
4Siku zangu zinapita kama moshi;
mifupa yangu inaungua kama katika furu.
5Nimepondekana kama majani na kunyauka;
sina hata hamu ya chakula.
6Kutokana na kuugua kwangu,
nimebaki mifupa na ngozi.
7Nimekuwa kama ndege katika jangwa,
kama bundi kwenye matongo.
8Ninalala macho wazi,
kama ndege anayekuwa peke yake juu ya paa.
9Muchana kutwa waadui zangu wananisimanga,
wanaonichekelea wanatumia jina langu kwa kulaani.
10Majivu yamekuwa chakula changu,
machozi yanachangana na kinywaji changu,
11kwa sababu ya kasirani na hasira yako,
maana umeniokota na kunitupilia mbali.
12Maisha yangu ni kama kivuli cha magaribi;
ninanyauka kama majani.
13Lakini wewe, ee Yawe, unatawala milele;
jina lako linakumbukwa katika vizazi vyote.
14Wewe utasimama na kurehemu Sayuni,
maana wakati umefika wa kuuhurumia,
wakati wake uliopangwa umefika.
15Watumishi wako wanapenda muji ule,
ijapokuwa ni mabomoko sasa;
wanauonea huruma,
ingawa umeharibika kabisa.
16Mataifa yataheshimu jina la Yawe;
wafalme wote katika dunia wataogopa utukufu wake.
17Yawe atajenga upya Sayuni,
na kuonyesha utukufu wake.
18Atakubali maombi ya mukosefu;
wala hatakataa maombi yao.
19Andika jambo hili kwa ajili ya vizazi vinavyokuja
kusudi watakaozaliwa kisha wamusifu Yawe,
20kwamba alichungulia chini kutoka katika pahali pake patakatifu.
Yawe aliangalia dunia kutoka mbinguni,
21akasikia malalamiko ya wafungwa,
akawaachilia huru waliohukumiwa kuuawa.
22Watu watatangaza jina la Yawe kule Sayuni;
sifa zake zitatangazwa kule Yerusalema,
23wakati mataifa yatakapokusanyika pamoja
na falme zitakapokutana kumwabudu Yawe.
24Mungu amenipunguzia nguvu ningali kijana;
amefupisha maisha yangu.
25Ee Mungu wangu, usinihamishe sasa
wakati ningali bado kijana.
Ee Yawe, wewe unadumu milele.
26Wewe uliumba dunia tokea zamani,
mbingu ni kazi ya mikono yako.
27Vitatoweka na kuchakaa kama nguo,
lakini wewe utabaki.
Utavibadilisha kama nguo,
navyo vitapita.
28Lakini wewe unabaki sawasawa,
na maisha yako hayana mwisho.
29Watoto wa watumishi wako watakaa salama;
wazao wao wataimarishwa mbele yako.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.