Ezekieli 27 - Swahili Congo Revised Bible 2002

Maombolezo juu ya muji wa Tiro

1Neno la Yawe lilinifikia kusema hivi:

2Sasa ewe mwanadamu, imba wimbo huu wa maombolezo juu ya muji wa Tiro.

3Muji wenye kuwa karibu ya bahari, unaofanya biashara na mataifa ya visanga vingi. Umwambie:

Bwana wetu Yawe anasema hivi:

Ewe Tiro, wewe umejivuna

kuwa muzuri kwelikweli!

4Mipaka yako imeenea kwelikweli!

Umejengwa kama mashua nzuri.

5Waliokujenga walitumia miti ya misunobari ya kutoka Seniri

kwa kupasua mbao zako zote;

walitwaa mierezi kutoka Lebanoni

kwa kukutengenezea mulingoti.

6Walitwaa miti ya mialo toka Basani

wakakuchongea makasia;

walikutengenezea mbao za kuikalia

kwa miti ya misunobari ya kisanga cha Kipuro,

na kuipamba kwa pembe ya tembo.

7Kitani kilichopindwa vizuri kutoka Misri

kilikuwa kwa kupamba tanga lako

na kwa ajili ya bendera yako.

Chandarua chako kilitengenezwa na nguo

ya rangi ya samawi na nyekundu-nyeusi

kutoka visanga vya Elisa.

8Watu wa miji Sidona na Arwadi

walikuwa wapiga makasia wako.

Wenye hekima wako walikuwa ndani

wakifanya kazi ya kuongoza.

9Wazee wa Gebali na wafundi wao

walikuwa wakiziba nyufa zako.

Wachuuzi wa bahari waliokuwa wakipitia kwako

walifanya biashara nawe.

10Watu kutoka Persia, Ludi na Puti

walijiunga katika kundi lako la waaskari;

walilundika ngao zao na kofia zao

kwenye kambi zao za kiaskari.

Waaskari hao walikupatia utukufu.

11Watu wa Arwadi pamoja na waaskari wako walilinda kuta zako pande zote, nao watu wa Gamadi walilinda minara yako. Walitundika ngao zao kwenye kuta zako pande zote, na hivyo wakaukamilisha uzuri wako.

12Watu wa Tarsisi walifanya biashara nawe kwa sababu ya utajiri wako mwingi na wa kila namna. Walitoa feza, chuma, bati, na risasi kwa kupata biashara yako.

13Watu wa Yavani, Tubali na Meseki, walifanya biashara nawe, wakakupatia watumwa na vifaa vya shaba wapate vitu vyako.

14Uliuzisha biashara yako huko Beti-Togarma kwa kujipatia farasi wa kubeba mizigo na farasi wa vita, ngamia na nyumbu.

15Watu wa Dedani walifanya biashara nawe. Inchi nyingi za kandokando ya bahari zilikuwa masoko yako makubwa. Watu wake walikuletea pembe za tembo na miti mizuri inayoitwa ebene kwa kununua vitu kwako.

16Watu wa Edomu walifanya biashara nawe kwa sababu ya wingi wa vitu vyako. Kwa kupata vitu vyako walikupa akiki, vitambaa vya rangi nyekundu-nyeusi, vitambaa vilivyopindwa vizuri, kitani safi, matumbawe na yakuti.

17Hata watu wa inchi ya Yuda na ya Israeli walifanya biashara nawe; walikupa ngano, mizeituni, tini za kwanzakwanza, asali, mafuta na marasi kwa kununua vitu kwako.

18Watu wa Damasiki walifanya biashara nawe kwa sababu ya wingi wa vitu vyako; walikupa divai kutoka muji wa Helboni na manyoya meupe ya kondoo.

19Wedani na Yavani walisafirisha vitu vyako toka muji wa Uzali; hata chuma kilichofuliwa, mudalasini na muchaichai kwa kununua vitu kwako.

20Watu wa Dedani walifanya biashara nawe kwa kukupatia matandiko ya farasi.

21Waarabu na wakubwa wote wa inchi ya Kedari walikuwa wachuuzi wako wakubwa katika biashara ya wana-kondoo, kondoo dume na mbuzi.

22Wachuuzi wa Seba na wa Rama walifanya biashara nawe; walikuletea viungo vya chakula, mawe ya bei kali na zahabu kwa kujipatia vitu vyako safi.

23Wakaaji wa miji ya Harani, Kane na Edeni na wachuuzi wa Asuria na Kilmadi walifanya biashara nawe.

24Hao walifanya nawe biashara ya nguo za bei kali, nguo za rangi nyekundu nyeusi zilizopindwa vizuri, nguo za rangi mbalimbali na kamba ngumu zilizosokotwa.

25Mashua makubwa za Tarsisi ndizo zilikusafirishia vitu vyako.

Basi wewe ulikuwa umejaa vitu

kama vile mashua katikati ya bahari.

26Wavuta makasia wako walikupeleka mbali katika bahari.

Upepo mukali wa mashariki umekuvunjavunja

ukiwa mbali katikati ya bahari.

27Mali yako, biashara yako, na vitu vyako,

waongozi wako wote katika chombo,

wafundi wako wa mashua na wachuuzi wako,

waaskari wako wote wanaokuwa kwako,

pamoja na wasafiri wanaokuwa kwako,

vyote vitaangamia ndani ya bahari,

siku ile ya kuangamizwa kwako.

28Kilio cha waongozi wako kitakaposikilika,

inchi za kandokando ya bahari zitatetemeka.

29Halafu wavuta makasia wote

wataziacha mashua zao.

Waongozi wote wa mashua watakaa inchi kavu.

30Wataomboleza kwa uchungu wa moyo juu yako,

na kulia kwa uchungu mukubwa;

watajitupia mavumbi juu ya vichwa vyao

na kugaagaa kwenye majivu.

31Watajinyoa vichwa kwa ajili yako

na kuvaa gunia.

Watalia kwa uchungu wa moyo juu yako.

32Wataimba wimbo wa maombolezo juu yako;

Nani aliyepata kuangamizwa kama Tiro

katikati ya bahari?

33Vitu vyako vilipofika katika inchi za ngambo,

ulitimiza mahitaji ya watu wengi!

Kwa wingi wa utajiri wa vitu vyako

uliwatajirisha wafalme wa dunia.

34Lakini sasa umevunjikia ndani ya bahari;

umeangamia katika vilindi vya maji.

Biashara yako na watu wote waliokuwa ndani yako

vimezama pamoja nawe.

35Wakaaji wote wa visanga

wameshangaa sana juu yako;

wafalme wao wameogopa sana,

nyuso zimekunjamana kwa huzuni.

36Wachuuzi wa mataifa watakuzomea!

Umekuwa kitu cha kuogopesha,

na umetoweka kwa milele!

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help