1Haya ndiyo mambo utakayowafanyia Haruni na wana wake kwa kuwatakasa wapate kunitumikia kama vile makuhani. Utatwaa mwana-ngombe dume na kondoo dume wawili wasiokuwa na kilema,
2mikate isiyotiwa chachu, maandazi yasiyotiwa chachu yaliyopondwa kwa mafuta, na mikate myembamba isiyotiwa chachu, lakini iliyopakwa mafuta. Vyote hivi vikuwe vimetengenezwa kwa unga laini wa ngano.
3Kisha uweke hiyo mikate ndani ya kikapu kimoja na kunitolea wakati mumoja na yule mwana-ngombe dume na wale kondoo dume wawili.
4Kisha uwapeleke Haruni na wana wake kwenye mulango wa hema la mukutano na kuwanawisha.
5Kisha utatwaa zile nguo za kikuhani umuvalishe Haruni: koti, kanzu, kizibao, kifuko cha kifua, na kumufunga ule mukaba uliofumwa kwa ufundi.
6Tena utamuvalisha ile kofia juu ya kichwa na kuweka juu ya ile kofia ile taji takatifu.
7Kisha kufanya hivyo, utatwaa yale mafuta ya kupakaa, umumiminie Haruni juu ya kichwa chake kwa kumutakasa.
8Kisha utawaleta wana wa Haruni na kuwavalisha vizibao.
9Utawafunga mikaba katika viuno na kuwavalisha kofia zao. Hivi ndivyo utakavyowatakasa Haruni na wana wake kuwa makuhani. Hao watakuwa makuhani siku zote kwa ajili ya sharti la siku zote.
10Kisha utamuleta yule mwana-ngombe dume mbele ya hema la mukutano. Haruni na wana wake wataweka mikono yao juu ya kichwa cha mwana-ngombe yule
11na kumuchinja mbele ya Yawe, kwenye mulango wa hema la mukutano.
12Utatwaa sehemu ya damu na kuipakaa kwenye pembe za mazabahu kwa kidole chako, na damu yote inayobaki utaimwanga chini ya mazabahu.
13Halafu utatwaa mafuta yote yanayofunika matumbotumbo, sehemu bora ya maini pamoja na figo mbili na mafuta yake, uviteketeze vyote juu ya mazabahu.
14Lakini nyama ya ngombe dume yule pamoja na ngozi na mavi yake utavitwaa na kuviteketeza inje ya kambi yenu. Hii itakuwa sadaka ya kuondoa zambi.
15Kisha utatwaa mumoja wa wale kondoo dume na kumwambia Haruni na wana wake waweke mikono yao juu ya kichwa chake.
16Nawe utamuchinja na damu yake utairushia juu ya mazabahu pande zake zote.
17Halafu utamukata yule kondoo vipandevipande. Utasafisha matumbotumbo yake na miguu yake, uviweke vyote pamoja na kichwa na vipande vingine.
18Kisha utamuteketeza kondoo muzima juu ya mazabahu kwa kunitolea sadaka ya kuteketezwa. Harufu ya sadaka inayotolewa kwa moto itanipendeza mimi Yawe.
19Utatwaa yule kondoo mwingine, naye Haruni na wana wake wataweka mikono yao juu ya kichwa chake.
20Nawe utamuchinja na kutwaa sehemu ya damu na kumupakaa Haruni na wana wake kwenye incha za masikio yao ya kuume na vidole gumba vya mikono yao ya kuume, na vidole gumba vya miguu yao ya kuume. Damu inayobaki utairushia juu ya mazabahu pande zake zote.
21Kisha utatwaa sehemu ya damu inayokuwa juu ya mazabahu pamoja na yale mafuta ya kupakaa umunyunyizie Haruni na nguo yake, uwanyunyizie vilevile wana wake na nguo zao. Haruni na wana wake watakuwa wametakaswa kwa ajili yangu pamoja na nguo zao zote.
22Kisha utatwaa mafuta ya yule kondoo dume: mukia wake, mafuta yanayofunika matumbotumbo na sehemu bora ya maini, figo zake mbili na mafuta yake, pamoja na paja la kuume. (Kondoo yule ni kondoo wa utakaso.)
23Kutoka katika kile kikapu cha mikate isiyotiwa chachu kinachokuwa mbele yangu mimi Yawe, utatwaa mukate mumoja na andazi moja lililotiwa mafuta na mukate mwembamba mumoja.
24Vyote hivi utavipatia Haruni na wana wake nao wataviinua juu kuwa kitambulisho cha kunitolea sadaka mimi Yawe.
25Kisha utavitwaa tena kutoka mikono yao na kuviteketeza juu ya mazabahu pamoja na ile sadaka ya kuteketezwa, vikuwe harufu nzuri itakayonipendeza mimi Yawe. Hiyo ni sadaka inayotolewa kwa moto.
26Kisha utatwaa kilali cha yule kondoo wa kumutakasa Haruni na kufanya kitambulisho cha kunitolea mimi Yawe. Nacho kitakuwa sehemu yako.
27Kuhani anapotakaswa, kilali na paja la kondoo dume wa utakaso vitaletwa na kutakaswa mbele yangu kwa kufanya kitambulisho cha kunitolea, navyo vitakuwa vya Haruni na wana wake.
28Hivyo siku zote Waisraeli watatwaa sehemu hizo kutoka katika sadaka zao za amani wanazonitolea mimi Yawe na kumupa Haruni na wana wake. Hiyo ni sadaka yao kwa Yawe.
29Kisha kufa kwa Haruni, nguo zake takatifu zitapewa kwa wana wake, nao watazivaa siku yao ya kupakwa mafuta na kuwekewa mikono.
30Mwana wa Haruni atakayekuwa kuhani pahali pa baba yake atavaa nguo zile siku saba katika hema la mukutano, kwa kutumika katika Pahali Patakatifu.
31Utatwaa nyama ya yule kondoo wa utakaso na kuitokotesha katika Pahali Patakatifu.
32Kisha utawapa Haruni na wana wake, nao wataikula kwenye mulango wa hema la mukutano pamoja na ile mikate iliyobakia katika kikapu.
33Watakula vitu hivyo vilivyotumika kwa utakaso na kwa ajili ya kuwafanyia upatanisho, lakini mutu mwingine asiruhusiwe kuvikula maana ni vitakatifu.
34Kama nyama yoyote au mikate hiyo itabakia mpaka asubui yake, basi utaiteketeza kwa moto. Isikuliwe maana ni kitu kitakatifu.
35Hivi ndivyo utakavyowatendea Haruni na wana wake kufuatana na yote yale niliyokuamuru. Utawatakasa kwa muda wa siku saba,
36na kila siku utatoa ngombe dume akuwe sadaka ya maondoleo ya zambi kwa kufanya upatanisho. Kwa kufanya hivyo utasafisha mazabahu, kisha utaimiminia mafuta kwa kuitakasa.
37Kwa siku saba utafanyia mazabahu upatanisho na kuitakasa. Nyuma ya hayo, mazabahu itakuwa takatifu kabisa na chochote kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu.
Sadaka za kila siku(Hes 28.1-8)38Kila siku, wakati wote unaokuja, utatolea sadaka juu ya mazabahu: wana-kondoo wawili wenye umri wa mwaka mumoja.
39Mwana-kondoo mumoja utamutoa sadaka asubui na mwingine magaribi.
40Pamoja na mwana-kondoo wa kwanza, utatoa kilo moja ya unga laini uliochanganywa na litre moja ya mafuta safi, na litre moja ya divai kama sadaka ya kinywaji.
41Vilevile na yule mwana-kondoo mwingine wa magaribi utamutolea sadaka pamoja na sadaka ya ngano na ya kinywaji kama vile ulivyofanya asubui. Harufu ya sadaka hiyo inayotolewa kwa moto itanipendeza mimi Yawe.
42Sadaka hii ya kuteketezwa itatolewa siku zote, kizazi kwa kizazi, mbele yangu mimi Yawe, mbele ya mulango wa hema la mukutano ambapo mimi nitakutana nanyi na kuongea nanyi.
43Hapo ndipo nitakapokutana na Waisraeli na utukufu wangu utapafanya pawe patakatifu.
44Hema la mukutano na mazabahu nitavifanya vitakatifu. Vilevile Haruni na wana wake nitawatakasa kusudi wanitumikie kama makuhani.
45Nitaishi kati ya Waisraeli, nami nitakuwa Mungu wao.
46Hapo ndipo watakapotambua kwamba mimi ni Yawe, Mungu wao, niliyewaleta kutoka katika inchi ya Misri, kusudi niishi kati yao. Mimi ni Yawe, Mungu wao.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.