1Mutu yeyote akileta sadaka ya ngano kwa Yawe, sadaka hiyo ikuwe ya unga laini. Atautia mafuta na ubani.
2Kisha, atawaletea hao makuhani, wazao wa Haruni. Atatwaa mukono mumoja wa unga huo laini wenye mafuta na ubani na kumupelekea kuhani mumoja ambaye atauteketeza juu ya mazabahu ukuwe sadaka ya ukumbusho kwa Yawe. Hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumupendeza Yawe.
3Sehemu inayobaki ya sadaka hiyo ni ya makuhani. Hiyo ni sehemu takatifu kabisa ya sadaka Yawe anayotolewa kwa moto.
4Kama mutu anamutolea Mungu sadaka ya ngano iliyochomwa kwenye furu, hiyo itakuwa ya mikate isiyotiwa chachu ya unga laini uliochanganywa na mafuta ya zeituni, au ya mikate myembamba isiyokuwa na chachu na isiyopakwa mafuta.
5Ikiwa sadaka unayotoa ni ya mukate uliokaangwa kwenye kikaango, hiyo itakuwa ya unga laini uliochanganywa na mafuta ya zeituni lakini bila chachu.
6Mikate hiyo itakatwakatwa na kumiminiwa mafuta. Hiyo ni sadaka ya ngano.
7Kama sadaka unayotoa ni ya mikate iliyopikwa katika sufuria, hiyo itakuwa ya unga laini na imetiwa mafuta.
8Utaleta sadaka ya ngano iliyotengenezwa kwa vitu hivyo mbele ya Yawe na kuhani ataipeleka kwenye mazabahu.
9Kuhani atatwaa sehemu ya sadaka hiyo ikiwa ni sadaka ya ukumbusho na kuiteketeza juu ya mazabahu. Hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumupendeza Yawe.
10Sehemu inayobaki ya sadaka ya ngano, ni ya makuhani. Hiyo ni sehemu takatifu kabisa ya sadaka inayotolewa Yawe kwa moto.
11Sadaka yoyote ya ngano utakayomuletea Yawe inapaswa kuwa imetengenezwa bila chachu, maana hakuna ruhusa hata kidogo ya kutumia chachu wala asali katika sadaka Yawe anazotolewa kwa moto.
12Unaweza kumuletea Yawe mazao yako ya kwanza kama sadaka. Lakini hayo hayatatolewa kwenye mazabahu kama harufu ya kumupendeza.
13Utakoleza sadaka zako zote za ngano kwa chumvi. Usiache hata kidogo kuweka chumvi katika sadaka yako ya ngano, maana chumvi ni kitambulisho cha agano Mungu alilofanya pamoja nanyi.
14Ukimutolea Yawe sadaka ya mazao yako ya kwanza utaitoa hiyo ikiwa imechomwa katika masuke yake, au utaitoa katika mikate ya kuchomwa iliyotengenezwa kwa ngano iliyosagwa.
15Utaitia mafuta na kuweka ubani. Hiyo ni sadaka ya ngano.
16Kuhani atateketeza sehemu ya sadaka hiyo ya ngano iliyopondwa na mafuta pamoja na ubani wake wote, ikuwe sadaka ya ukumbusho. Hiyo ni sadaka Yawe anayotolewa kwa moto.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.