1Wakati huo, kijana Samweli alipokuwa anamutumikia Yawe chini ya uangalizi wa Eli, ujumbe kutoka kwa Yawe ulikuwa mara haba tu; hata na maono kutoka kwake yalipatikana mara chache.
2Siku moja usiku, Eli ambaye macho yake yalikuwa yamefifia, alikuwa amelala katika chumba chake.
3Samweli naye alikuwa amelala ndani ya hekalu la Yawe karibu na Sanduku la Agano la Mungu. Taa ya Yawe ilikuwa ingali inawaka maana kulikuwa hakujapambazuka.
4Halafu Yawe akamwita Samweli, naye Samweli, akaitika: “Niko hapa!”
5Kisha Samweli akamwendea Eli kwa haraka, akamwambia: “Nimekuja, maana umeniita.”
Lakini Eli akamwambia: “Mimi sikukuita. Kwenda ulale.” Samweli akarudi na kulala.
6Yawe akamwita tena: “Samweli!” Samweli akaamuka, akamwendea Eli na kumwambia: “Nimekuja, maana umeniita.”
Lakini Eli akamwambia: “Sikukuita mwana wangu, ulale tena.”
7Samweli alikuwa hamujui Yawe bado, wala ujumbe wa Yawe ulikuwa bado haujafunuliwa kwake.
8Yawe akamwita Samweli kwa mara ya tatu. Samweli akaamuka, akamwendea Eli na kumwambia: “Nimekuja, maana umeniita.”
Halafu Eli alitambua kwamba Yawe ndiye aliyemwita Samweli.
9Kwa hiyo Eli akamwambia Samweli: “Kwenda ulale, na akikuita, umwambie hivi: ‘Sema, ee Yawe, maana mimi mutumishi wako ninasikiliza.’ ” Hivyo Samweli akarudi na kulala pahali pake.
10Kisha Yawe akakuja na kusimama hapo, akamwita Samweli kama pale mbele: “Samweli! Samweli!”
Samweli akasema: “Sema, maana mimi mutumishi wako ninasikiliza.”
11Kisha, Yawe akamwambia Samweli: “Ninataka kutenda jambo fulani katika Israeli ambalo kila mutu atakayesikia, atashituka kwa kulisikia.
12Siku hiyo, nitatimiza yale yote niliyosema tangu mwanzo mpaka mwisho juu ya Eli na juu ya jamaa yake.
13Nimekwisha kumwambia kwamba nitaiazibu jamaa yake milele, kwa uovu anaoujua kwa sababu wana wake wamenikufuru mimi na hakuwazuia.
14Kwa hiyo ninaapa juu ya jamaa ya Eli kwamba uovu wao hautaondolewa hata kidogo kwa matoleo wala kwa sadaka.”
15Samweli akalala pale mpaka asubui, kisha akaamuka na kufungua milango ya nyumba ya Yawe. Lakini Samweli aliogopa kumwambia Eli maono hayo.
16Hata hivyo, Eli alimwita Samweli, akamwambia: “Mwana wangu Samweli.”
Samweli akaitika: “Niko hapa!”
17Eli akamwuliza: “Yawe alikuambia nini? Usinifiche alichokuambia. Ikiwa utanificha kitu alichokuambia, Mungu akuazibu vikali.”
18Basi, Samweli akamwelezea Eli yote aliyoambiwa, bila kumuficha chochote. Halafu Eli akasema: “Yeye ni Yawe; afanye anachoona ni chema kwake.”
19Samweli aliendelea kukomaa na Yawe akakuwa pamoja naye, na yale yote aliyosema hakuna hata moja ambalo halikutimia.
20Watu wote katika inchi ya Israeli toka Dani, upande wa kaskazini, mpaka Beri-Seba, upande wa kusini, wakajua kwamba Samweli alikuwa nabii mwaminifu wa Yawe.
21Yawe alizidi kujionyesha kule Shilo, ambako alimutokea Samweli na kuongea naye. Naye Samweli aliposema kitu, Waisraeli wote walimusikiliza.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.