Yobu 38 - Swahili Congo Revised Bible 2002

Mungu anamujibu Yobu

1Halafu Yawe akamujibu Yobu kutoka katika zoruba:

2Nani wewe unayevuruga mipango yangu

kwa maneno yasiyokuwa na akili?

3Ujikaze kama mwanaume,

nami nitakuuliza nawe utanijibu.

4Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya dunia?

Uniambie, kama una maarifa.

5Ni nani aliyeweka vipimo vyake, unajua bila shaka!

Au nani aliyenyoosha kamba juu yake kwa kuipima?

6Nguzo za dunia zimesimikwa juu ya nini,

au nani aliyeliweka jiwe lake la musingi,

7nyota za asubui zilipokuwa zikiimba pamoja,

na wana wa Mungu wakapiga vigelegele vya shangwe?

8Ni nani aliyefunga mafuriko ya bahari

wakati yalipozuka na kuvuma kutoka katika vilindi?

9Ni nani aliyefunika bahari kwa mawingu

na kuiviringishia giza kubwa,

10aliyeiwekea bahari mipaka

na kuizuia kwa vifungio na milango

11na kuiambia: “Mwisho wako ni hapa, si zaidi!

Mawimbi yako ya nguvu yatakomea hapa!”

12Yobu, tangu uzaliwe umekwisha kuamuru kupambazuke

na kufanya mapambazuko yajue pahali pake,

13kusudi yapate kukamata dunia kwa pembe zake

na kuwatikisa watenda mabaya?

14Dunia inageuka na kupata rangi kama nguo;

kama udongo wa mufinyanzi unavyogeuzwa na muhuri.

15Lakini waovu watanyimwa mwangaza wao,

mukono wanaonyoosha kwa kupiga watu utavunjwa.

16Umepata kufika kwenye chemichemi za bahari

au kutembea juu ya sakafu ya kilindi cha bahari?

17Umekwisha kuonyeshwa milango ya kifo

au kuona milango ya makao ya giza kubwa?

18Unajua ukubwa wa dunia?

Uniambie kama unajua haya yote.

19Makao ya mwangaza yako wapi?

Kwenye nyumba ya giza ni wapi,

20kusudi upate kupeleka kwenye makao yake,

na kuifahamu njia ya kwenda kule kwake.

21Wewe unapaswa kujua,

wewe ambaye umekwisha ishi miaka mingi!

22Umekwisha kuingia katika akiba za teluji,

au kuona akiba za mvua ya mawe

23ambavyo nimeviweka kwa ajili ya wakati wa fujo,

kwa ajili ya siku ya mapigano na vita?

24Unajua mwangaza unagawanywa kwa njia gani,

au namna gani upepo wa mashariki unavyosambazwa katika dunia?

25Nani aliyechora katika anga njia kwa ajili ya mvua?

Nani aliyeonyesha radi njia yake katika mawingu,

26nayo ikasababisha mvua kunyesha katika inchi kusikoishi mutu

na katika jangwa ambako hakuna mutu,

27kusudi ikunyweshe inchi kavu na yenye kukauka

na kuifanya ioteshe majani?

28Mvua ina baba?

Au nani amezaa matone ya umande?

29Barafu ilitoka katika tumbo la nani?

Nani aliyezaa teluji?

30Maji yanageuka kuwa magumu kama jiwe,

na uso wa bahari unaganda.

31Angalia makundi ya nyota:

Unaweza kuifunga minyororo Kilimia,

au kuviregeza vifungo vya Orioni?

32Unaweza kuongoza nyota kwa wakati wake,

au kumwongoza Dubu pamoja na vitoto vyake?

33Unayajua maagizo ya mbingu?

Unaweza kuzipangia utaratibu wao katika dunia?

34Unaweza kupiga vigelegele na kuyaamuru mawingu

yakufunike kwa mutiririko wa mvua?

35Wewe ukiamuru umeme uangaze,

utakufikia na kusema: “Nipo hapa”?

36Ni nani aliyemujulisha kwarara kujaa kwa muto Nili

au aliyemwambia jogoo kwamba mvua inakuja?

37Nani mwenye akili ya kuweza kuhesabu mawingu

au kuinamisha vibuyu vya maji kule katika mbingu

38kusudi mavumbi katika dunia yagandamane

na udongo ushikamane na kuwa matope?

39Unaweza kumwindia simba dike

au kuishibisha hamu ya simba wakali

40wanapojificha ndani ya matundu yao,

au kulala katika maficho wakivizia?

41Ni nani anayewapa vibombobombo chakula chao,

vitoto vyao vinaponililia mimi Mungu,

na kurukaruka huku na kule kwa njaa?

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help