1Maombi ya nabii Habakuki:
2Ee Yawe, nimesikia juu ya utukufu wako,
juu ya matendo yako, nami ninaogopa.
Uyafanye tena mambo yale wakati wetu;
uyafanye yajulikane wakati huu wetu.
Unapokasirika tafazali ukumbuke huruma yako!
3Mungu amekuja kutoka jimbo la Temani,
Mungu mutakatifu anakuja kutoka mulima Parani.
Utukufu wake umeenea pote mbinguni,
nayo dunia imejaa sifa zake.
4Anangaa kama jua;
mishale ya mwangaza inatoka katika mukono wake
ambamo nguvu yake inajificha.
5Ugonjwa mukali unatangulia mbele yake,
nyuma yake hasara inafuata.
6Akisimama dunia inatikisika;
akiyatupia mataifa jicho, hayo yanatetemeka.
Milima ya milele inavunjwavunjwa,
vilima vya zamani za kale vinaanguka;
ni juu yao kulipokuwa njia zake za kale na kale.
7Niliwaona watu wa Kusani wakiteseka,
na watu wa Midiani wakitetemeka.
8Ee Yawe, umeikasirikia mito?
Umeyakasirikia maji ya bahari?
Ulipanda juu ya gari lako la vita
na kuendesha farasi kwa kupata ushindi.
9Uliuweka tayari upinde wako,
ukaweka mishale yako kwenye kamba.
Uliupasua udongo kwa mito.
10Milima ilikuona, ikanyauka;
mafuriko ya maji yakapita mule.
Vilindi vya bahari vilinguruma,
na kurusha juu mawimbi yake.
11Jua na mwezi vilikaa kimya katika makao yao,
vilipoona mwangaza wa mishale yako ikienda mbio,
vilipouona mukuki wako ukimetameta.
12Kwa kasirani ulipita juu ya inchi,
uliyakanyaga mataifa kwa hasira yako.
13Ulitoka kwenda kuwaokoa watu wako,
kumwokoa yule uliyemusimika kwa kumupakaa mafuta.
Ulimuponda mutawala wa jamii ya waovu,
ukawaangamiza kabisa wafuasi wake.
14Umetoboa vichwa vya wakubwa wao
kwa mikuki yao wenyewe,
waliotufikia kama zoruba kututawanya,
wakijivuna kwa kuwameza wamasikini kwa siri.
15Kwa farasi wako ulitembea juu ya bahari,
bahari inayosukwasukwa na mawimbi.
16Nikasikia hayo, matumbotumbo yangu yakatetemeka.
Midomo yangu inatetemeka kwa hofu,
mifupa yangu inateguka,
miguu yangu inatetemeka.
Ninangojea kwa utulivu siku ile ya hasara,
ambayo inawafikia wale wanaotushambulia.
17Hata kama miti ya tini isipochanua maua
wala mizabibu kuzaa zabibu,
hata kama mizeituni isipozaa zeituni
na mashamba yasipotoa chakula,
hata kama kondoo wakitoweka katika zizi
na nyama wa kufugwa kukosekana katika mazizi,
18mimi nitaendelea kumufurahia Yawe.
Nitamushangilia Mungu anayeniokoa.
19Bwana, Yawe ndiye nguvu yangu,
anaimarisha miguu yangu kama ya paa,
ananiwezesha kupita juu katika milima.
Kwa mwimbishaji: pamoja na ala za muziki wa nyuzi.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.