1Hakika kuna nafasi ya kuchimba feza,
na pahali ambako zahabu inasafishwa.
2Watu wanachimba chuma ndani ya udongo,
wanayeyusha shaba kutoka mawe ya madini.
3Wachimba madini wanaleta taa katika giza,
wanatafutatafuta mpaka chini zaidi ya udongo,
na kuchimbua mawe yenye madini katika giza.
4Mwanadamu anachimba mashimo mbali na makao ya watu,
mbali na watu pahali kusipofikiwa,
wachimba madini wananinginia wakifungwa kamba.
5Kutoka ndani ya udongo chakula kinapatikana,
lakini chini yake kila kitu kinavurugwa kwa moto.
6Katika mawe yake kunatoka mawe ya yakuti,
na udongo wake una mavumbi ya zahabu.
7Njia ya kwenda kule
hakuna ndege mukula nyama anayeijua;
na wala jicho la tai halijaiona.
8Nyama wakali hawajaikanyaga
wala simba mwenyewe hajapita ndani yake.
9Mwanadamu anachimbua mawe magumu kabisa,
anachimbua milima mpaka kwenye misingi yake.
10Anapasua mifereji kati ya mawe makubwa,
na jicho lake linaona mawe ya bei kali.
11Anaziba chemichemi zisitiririke,
na kufichua vitu vilivyofichwa.
12Lakini hekima itapatikana wapi?
Ni pahali gani panapopatikana maarifa?
13Hakuna mutu anayejua bei ya hekima,
wala hekima haipatikani katika inchi ya wanaokuwa wazima.
14Vilindi vinasema: “Hekima haiko kwetu.”
Bahari inasema: “Haiko kwangu.”
15Hekima haiwezi kupatikana kwa zahabu,
wala kwa kupima kiasi kingi cha feza.
16Haiwezi kupimwa kwa zahabu ya Ofiri,
wala kwa mawe ya sardoniki au ya yakuti samawi.
17Zahabu au kioo havilingani nayo,
wala haiwezi kubadilishwa na mawe ya zahabu safi.
18Hekima ina bei kali kuliko mawe ya matumbawe na marijani,
bei kali yake inashinda bei kali ya ushanga.
19Topazi ya Etiopia haiwezi kulinganishwa nayo,
wala haiwezi kupewa bei ya zahabu safi.
20Basi, hekima inatoka wapi?
Ni wapi panapopatikana maarifa?
21Imefichwa mbali na macho ya viumbe vyote vyenye uzima,
na ndege hawawezi kuiona.
22Shimo la kuangamia na Kifo wanasema:
“Tumesikia uvumi wake kwa masikio yetu.”
23Mungu anajua njia ya hekima,
anajua pahali inapopatikana.
24Maana yeye anaona mpaka kwenye miisho ya dunia,
anaona kila kitu chini ya mbingu.
25Alipoupa upepo uzito wake
na kuyapimia maji mipaka yake,
26alipoamua mvua inyeshe wapi,
umeme na radi vipite wapi,
27pale ndipo alipoiona hekima na kuitangaza.
Aliisimika na kuichunguza.
28Kisha Mungu akamwambia mwanadamu:
Sikia! Kumwogopa Bwana ndiyo hekima,
na kujitenga na uovu ndiyo maarifa.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.