Nahumu 2 - Swahili Congo Revised Bible 2002

1Enyi watu wa Yuda muangalie:

Mutu anakuja kutoka milima anayeleta habari njema,

anayetangaza amani.

Mufanye sikukuu zenu,

mutimize viapo vyenu,

maana waovu hawatawashambulia,

kwa sababu wameangamizwa kabisa. Kuanguka kwa Ninawe

2Mwangamizaji amekuja kukushambulia, ee Ninawe.

Chunga kuta zako!

Weka ulinzi katika barabara!

Ujiweke tayari!

Kusanya nguvu zako zote!

3Yawe anamurudishia Yakobo utukufu wake,

anawapa tena Waisraeli utukufu wao,

ingawa washambulizi hawakuwaachia kitu,

hata matawi yao ya mizabibu waliyakata.

4Ngao za mashujaa wake ni nyekundu,

waaskari wake wamevaa nguo nyekundu sana.

Magari yao ya vita yanametameta kama ndimi za moto,

yamepangwa tayari kwa kushambulia;

farasi hawatulii kwa hamu ya kushambulia.

5Magari ya vita yanakimbia mbio katika barabara,

yanakwenda huko na huko katika uwanja.

Yanametameta kama ndimi za moto!

Yanakwenda mbio kama umeme.

6Sasa anawaita wakubwa wake,

nao wanajikwaa wanapomwendea;

wanakwenda kwenye ukuta kwa haraka

kutayarisha ukingo.

7Vikingio vya mito vimefunguliwa,

nyumba ya kifalme imejaa hofu.

8Muji uko wazi kabisa,

watu wamekamatwa mateka.

Wanawake wake wanaomboleza,

wanalia kama njiwa,

na kujipigapiga kwenye vifua.

9Muji Ninawe ni kama birika lililobomoka,

watu wake wanaukimbia ovyo.

Musimame! Musimame! Sauti inaita,

lakini hakuna anayerudi nyuma.

10Munyanganye feza,

munyanganye zahabu!

Mali yake haina mwisho!

Kuna wingi wa kila kitu cha bei kali!

11Muji wa Ninawe ni maangamizi matupu na uharibifu!

Watu wamekufa moyo, magoti yanagongana,

nguvu zimewaishia, nyuso zimebadilika!

12Basi lile pango la simba limekuwa namna gani,

lile lililokuwa maficho ya simba wakali?

Ile nafasi ya simba imekuwa namna gani,

nafasi ya wana-simba ambayo hakuna aliyeweza kuwashitua?

13Simba dume amewararulia watoto wake nyama ya kutosha,

akiwakamatia simba dike nyama zao;

ameyajaza mapango yake na nyama,

na makao yake vipande vya nyama.

14Mimi Yawe wa majeshi nitakushambulia: nitayateketeza kwa moto magari yako ya vita, nitawamaliza kwa upanga hao simba wako wakali, vitu ulivyonyanganya nitavikomesha kutoka katika inchi, na sauti ya wajumbe wako haitasikilika tena.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help