Ezekieli 16 - Swahili Congo Revised Bible 2002

Muji Yerusalema si mwaminifu

1Neno la Yawe lilinifikia kusema hivi:

2Wewe mwanadamu, ujulishe Yerusalema machukizo yake.

3Uuambie kwamba Bwana wake Yawe anauambia hivi: Kwa asili wewe ulizaliwa katika inchi ya Kanana. Baba yako alikuwa Mwamori, na mama yako alikuwa Muhiti.

4Siku ile ulipozaliwa, kitofu chako hakikukatwa wala haukusafishwa na maji; haukupakaliwa chumvi wala kuvalishwa nguo za kitoto.

5Hakuna aliyekuonea huruma na kukufanyia mambo hayo. Hakuna aliyekupenda. Lakini, siku ile ulipozaliwa, ulitupwa huko katika pori kwa sababu siku ulipozaliwa ulichukiza sana.

6Mimi nilipopita karibu nawe, nikakuona ukigaagaa katika damu yako, nikakuambia:

7Uishi, na ukomae kama mumea katika shamba. Nawe ukakomaa na kurefuka hata ukakuwa binti. Maziba yako yakakomaa na nywele zako nazo zikarefuka. Lakini ulikuwa uchi kabisa.

8Nilipopita tena karibu nawe, nikakuona. Wakati huu, ulikuwa umefikia umri wa kupendwa kama binti. Nikalitandaza vazi langu juu yako na kuufunika uchi wako. Nikafanya nawe agano la ndoa, nawe ukakuwa wangu.

–Ni ujumbe wa Bwana wetu Yawe.

9Kisha nikatwaa maji, nikakukogesha kwa kusafisha damu uliyokuwa nayo, nikakupakaa mafuta.

10Nilikuvalisha vilevile nguo iliyopambwa vizuri na viatu vya ngozi nzuri. Nikakuvalisha mukaba wa kitani safi na kitambaa cha hariri.

11Nikakupamba kwa mapambo, nikakuvalisha vikomo kwa mikono yako na mukufu kwenye shingo.

12Nikakutia pete kwenye pua, visikio kwenye masikio yako na juu ya kichwa chako nikakupamba kwa taji nzuri.

13Basi, ukapambwa kwa zahabu na feza. Nguo yako ikakuwa ya kitani safi na hariri, nayo ilikuwa imepambwa. Ulitumia unga safi, asali na mafuta kwa chakula chako. Ukakuwa na sura nzuri sana, ukaifikia hali ya malkia.

14Sifa zako zikaenea kati ya mataifa kutokana na uzuri wako, maana uzuri wako ulikamilika kwa sababu ya utukufu niliokujalia. –Ni ujumbe wa Bwana wetu Yawe.–

15Lakini, ulitegemea uzuri wako, ukatumia sifa yako kwa kufanya uzinzi, ukifanya ukahaba na mutu yeyote anayepita.

16Ulitwaa sehemu ya nguo zako, ukaitumia kwa kupamba pahali pako pa kutambikia na hapo ndipo ukafanyia uzinzi wako. Jambo la namna hiyo halijapata kutokea wala halitatokea hata kidogo!

17Ulitwaa vile vitu vyako vizuri vya zahabu na feza nilivyokupa kwa kujipamba, ukajifanyia sanamu za wanaume upate kufanya uzinzi nazo.

18Ukatwaa nguo nilizokupa zilizopambwa na kuzifunika zile sanamu, na mafuta yangu na ubani wangu, ukavitolea sanamu hizo.

19Niliwakulisha ninyi kwa unga safi, mafuta na asali. Lakini chakula changu nilichokupa, ulikitoa kwa sanamu hizo kuwa harufu ya kupendeza.

–Ni ujumbe wa Bwana wetu Yawe.

20Tena, wana wako na wabinti zako ulionizalia uliwatwaa, ukawatambikia kwa sanamu zako wapate kukuliwa. Unazani uzinzi wako ulikuwa ni jambo dogo?

21Jambo hili la kuwachinja watoto wangu kwa kuwa sadaka ya kuteketeza kwa ajili ya sanamu zako ni jambo dogo?

22Katika machukizo yako yote pamoja na uzinzi wako haukuzikumbuka siku za utoto wako, wakati ulipokuwa uchi kabisa, bila kitu, ukigaagaa katika damu yako!

23Ole kwako, ole kwako Yerusalema!

–Ni ujumbe wa Bwana wetu Yawe.–

Kisha kufanya hayo yote

24ulijijengea nafasi zinazoinuka kila pahali.

25Kwa mwanzo wa kila barabara ulijijengea nafasi inayoinuka, ukautumia uzuri wako kwa kufanya uzinzi ukijitoa kwa kila mupita njia na kuongeza uzinzi wako.

26Tena ulifanya uzinzi na jirani zako Wamisri waliojaa tamaa, ukaongeza uzinzi wako na kuichochea hasira yangu.

27Basi, niliunyoosha mukono wangu kwa kukuazibu. Nilipunguza chakula chako, nikakuachilia kwa waadui zako, wabinti za Wafilistini ambao walipata haya sana juu ya tabia yako chafu sana.

28Kwa sababu haukutosheka, ulifanya tena uzinzi na Waasuria. Na hiyo vilevile haikukutoshelea.

29Ulijitoa wewe mwenyewe utumiwe na Wababeli, watu wanaofanya biashara! Hata hivyo haukutosheka.

30Kweli wewe ni mugonjwa wa mapenzi.

–Ni ujumbe wa Bwana wetu Yawe.–

Unafanya uzinzi bila kuona haya hata kidogo.

31Umejijengea nafasi yako yenye kuinuka kwa mwanzo wa kila barabara na kujijengea pahali pa kutambikia katika kila kiwanja. Tena wewe haukukuwa kama kahaba maana ulikataa kulipwa.

32Ulikuwa kama muke muzinzi anayekaribisha wageni pahali pa mume wake.

33Kwa kawaida wanaume wanawalipa makahaba, lakini wewe umewalipa wapenzi wako wote, ukiwahonga wakuje kwako toka pande zote upate kuzini nao.

34Katika ukahaba wako haukufanya kama wanawake wengine: hakuna aliyekubembeleza kusudi uzini naye lakini wewe ulilipa feza pahali pa kulipwa.

Hukumu ya Mungu juu ya Yerusalema

35Sasa basi, ewe kahaba, usikilize neno la Yawe.

36Bwana wenu Yawe anasema hivi: Wewe umeponda feza, umefunua uchi wako kwa kuzini na wapenzi wako, umeziabudu sanamu zako zote za miungu na kuzitolea damu ya watoto wako.

37Basi, mimi nitawakusanya wapenzi wako wote uliojifurahisha nao, wote uliowapenda na wote uliowachukia. Nitawakusanya toka pande zote wakushambulie. Nitawafunulia uchi wako wapate kuuona.

38Nitakuhukumu kama vile wanawake wanaovunja ahadi ya ndoa au wauaji wanavyohukumiwa; nitakuhukumu kwa azabu ya kifo kwa hasira na kwa ajili ya wivu.

39Nitakutia katika mikono ya wapenzi wako, nao watabomoa nafasi yako yenye kuinuka na pahali pako pa kutambikia. Watakutosha nguo yako na kukunyanganya vitu vyako vya kujipamba, wakuache uchi, bila kitu.

40Watakuletea kundi kubwa kwa kukushambulia; watakuua kwa kukupiga mawe na kisha watakukatakata kwa panga zao.

41Nyumba zako wataziteketeza kwa moto na kuwafanya wanawake wengi waone azabu yako. Utakoma kujitoa kwa mutu yeyote afanye uzinzi nawe.

42Hivi, kasirani yangu itatosheka juu yako, wivu niliokuwa nao juu yako utakwisha; nitatulia wala sitaona hasira tena.

43Wewe umesahau yale ambayo mimi nilikufanyia ulipokuwa kijana. Wewe umenichukiza sana kwa mambo yale yote. Basi, nitakulipiza kisasi juu ya kila kitu ulichotenda.

–Ni ujumbe wa Bwana wetu Yawe.–

Haukuongeza uchafu juu ya machukizo yako yote?

Mutoto wa nyoka ni nyoka

44Ewe Yerusalema! Mutu akitaka kutumia mezali juu yako atasema hivi: Kama vile mama anavyokuwa ndivyo binti wake anavyokuwa.

45Kweli wewe ni mutoto wa mama aliyemuchukia mume wake na watoto wake; wewe ni sawa na dada zako waliowachukia waume wao na watoto wao. Mama yako alikuwa Muhiti na baba yako alikuwa Mwamori.

46Dada yako mukubwa ni Samaria, aliyekaa upande wako wa kaskazini pamoja na wabinti zake. Dada yako mudogo ni Sodoma, aliyekaa upande wako wa kusini pamoja na wabinti zake.

47Lakini wewe haukutosheka kufuata mienendo yao au kutenda sawa na machukizo yao. Kwa muda mufupi tu ulipotoka kuliko vile wao walivyopotoka katika mienendo yako yote.

48Kama vile ninavyoishi, –ni ujumbe wa Bwana wetu Yawe– dada yako Sodoma na wabinti zake, hawakufanya maovu kama yale uliyotenda wewe na wabinti zako.

49Kosa la dada yako Sodoma, lilikuwa hili: yeye pamoja na wabinti wake walipokuwa na chakula nao walifanikiwa sana, walianza kujivuna, wakaacha kuwasaidia wamasikini na wakosefu.

50Walijivuna, wakafanya machukizo mbele yangu. Kwa hiyo niliwaangamiza mara tu nilipoyaona hayo.

51Naye Samaria kwa kweli hakutenda hata nusu ya zambi zako. Wewe umefanya machukizo mengi kuliko wao. Ukilinganisha maovu yako na ya dada zako, maovu yao si kitu!

52Wewe utaibeba haya yako kabisa! Zambi zako ni mbaya zaidi kuliko za wadada zako, kwa kipimo cha kuwafanya wadada zako na zambi zao, waonekane kama hawana kosa. Basi, upate haya na kufezeheka, maana umewafanya wadada zako waonekane kama hawana kosa.

Sodoma na Samaria itajengwa upya

53Nitawarudishia Sodoma na Samaria pamoja na wabinti zao hali yao njema ya mbele. Nawe vilevile nitakufanikisha kati yao,

54kusudi ubebe haya yako na kufezeheka, kwa sababu ya mambo yote uliyotenda, ndipo kwa hali yako hiyo wadada zako watajiona kwamba wao ni afazali.

55Wadada zako, Sodoma na Samaria, pamoja na wabinti zao watairudilia hali yao ya pale mbele. Hata wewe na wabinti zako mutairudilia hali yenu.

56Kwa majivuno yako ulimuzarau dada yako Sodoma.

57Haukufanya hivyo mbele uovu wako haujafichuliwa. Sasa umekuwa kama Sodoma. Umekuwa kitu cha kuchekelewa mbele ya wabinti za Edomu na jirani zake wote, na wabinti za Wafilistini jirani zako ambao walikuchukia.

58Azabu ya uchafu wa tabia na machukizo yako utaibeba wewe mwenyewe.

–Ni ujumbe wa Yawe.

59Bwana wetu Yawe anasema hivi: Nitakutendea wewe Yerusalema kama unavyostahili. Wewe umekizarau kiapo, ukivunja agano.

60Lakini mimi nitalikumbuka agano langu nililoagana nawe katika siku za ujana wako. Nitafanya nawe agano la milele.

61Nawe utakumbuka mienendo yako na kupata haya wakati nitakapokupa wadada zako, mukubwa na mudogo, kama wabinti zako, ingawa si kwa sababu ya agano kati yangu na wewe.

62Mimi nitafanya agano nawe, nawe utatambua kwamba mimi ni Yawe.

63Nitakusamehe kila kitu ulichotenda. Nawe utakapokumbuka hayo yote uliyotenda utashangaa na kunyamaza kwa sababu ya haya wala hautasubutu kusema tena.

–Ni ujumbe wa Bwana wetu Yawe.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help