Hesabu 10 - Swahili Congo Revised Bible 2002

Baragumu za feza

1Yawe akamwambia Musa:

2Tengeneza baragumu mbili kwa feza iliyofuliwa. Utatumia baragumu hizo wakati wa kuwaita watu na wakati wa kuvunja kambi.

3Baragumu zote mbili zikipigwa pamoja, watu wote watakusanyika karibu nawe mbele ya mulango wa hema la mukutano.

4Lakini kama ikipigwa baragumu moja tu, basi ni viongozi tu wa makabila ya Israeli watakaokusanyika karibu nawe.

5Alama hiyo ikitolewa kwa kupiga baragumu, wakaaji wa kambi za upande wa mashariki wataanza safari.

6Alama hiyo ikipigwa mara ya pili, wale wa kambi za upande wa kusini wataanza kuondoka. Alama hiyo ya baragumu itatolewa kila wakati wa kuanza safari.

7Lakini wakati wa kuwaita watu wakusanyike pamoja, baragumu zitapigwa kwa njia ya kawaida.

8Wazao wa Haruni, makuhani, ndio watakaopiga baragumu hizo. Utaratibu huo utakuwa sharti la kufuata siku zote katika vizazi vyenu vyote.

9Wakati wa vita katika inchi yenu juu ya waadui wanaowashambulia, mutatoa kitambulisho cha vita kwa kupiga baragumu hizi kusudi Yawe, Mungu wenu apate kuwakumbuka na kuwaokoa na waadui zenu.

10Vilevile katika siku zenu za furaha, kama vile sikukuu za mwandamo wa mwezi na sikukuu nyingine, mutapiga baragumu hizi wakati munapotoa sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za amani. Hapo mimi Mungu wenu nitawakumbuka. Mimi ni Yawe, Mungu wenu.

Waisraeli wanasafiri

11Katika siku ya makumi mbili ya mwezi wa pili, mwaka wa pili tangu watu wa Israeli walipoondoka Misri, wingu lililokuwa juu ya hema la kuchunga vibao vya agano likainuliwa,

12nao Waisraeli wakaanza safari yao kutoka jangwa la Sinai. Wingu hilo likapanda na kisha likatua katika jangwa la Parani.

13Kwa mara ya kwanza Waisraeli walifunga safari hiyo kwa amri ya Yawe kama ilivyotolewa na Musa.

14Wale waliokuwa chini ya bendera ya jeshi la kabila la Yuda, wakatangulia, kundi moja kisha lingine. Kiongozi wao alikuwa Nasoni mwana wa Aminadabu.

15Netaneli mwana wa Suari, alikuwa kiongozi wa jeshi la kabila la Isakari.

16Naye Eliabu mwana wa Heloni, alikuwa kiongozi wa jeshi la kabila la Zebuluni.

17Kisha, hema likashushwa, na watu wa ukoo wa Gersoni na wa Merari ambao walilibeba, walianza kuondoka.

18Halafu, watu waliokuwa chini ya bendera ya jeshi lililoongozwa na kabila la Rubeni, wakafuata kundi moja nyuma ya lingine. Kiongozi wao alikuwa Elisuri mwana wa Sedeuri.

19Selumieli mwana wa Suri-Shadai, aliongoza kabila la Simeoni.

20Naye Eliasafu mwana wa Deueli, aliongoza kabila la Gadi.

21Kisha walifuata watu wa ukoo wa Kohati, wakiwa wamebeba vyombo vitakatifu. Walipofika, hema lilikuwa limekwisha kusimikwa.

22Nyuma ya hao, wakafuata watu waliokuwa chini ya bendera ya jeshi lililoongozwa na kabila la Efuraimu, kundi moja nyuma ya lingine. Kiongozi wao alikuwa Elisama mwana wa Amihudi.

23Gamalieli mwana wa Pedasuri aliongoza kabila la Manase,

24naye Abidani mwana wa Gideoni, aliongoza kabila la Benjamina.

25Mwisho, wale waliokuwa chini ya bendera ya jeshi lililoongozwa na kabila la Dani, waliokuwa kama walinzi nyuma ya majeshi yote, wakasafiri, kundi moja nyuma ya lingine. Hawa waliongozwa na Ahiezeri mwana wa Amishadai.

26Pagieli mwana wa Okrani, aliongoza kabila la Aseri.

27Naye Ahira mwana wa Enani, aliongoza kabila la Nafutali.

28Huu basi, ndio utaratibu Waisraeli waliofuata kulingana na makundi yao, kila wakati walipovunja kambi na kuanza kusafiri tena.

29Musa akamwambia shemeki yake Hobabu mwana wa Reueli Mumidiani, baba mukwe wake: Sisi tunasafiri kwenda pahali ambapo Yawe amesema: Nitawapa ninyi pahali hapo. Basi, tuende pamoja, nasi tutakutendea vizuri maana Yawe ameahidi kutendea Waisraeli vizuri.

30Lakini Hobabu akajibu: Mimi sitakwenda nanyi; lakini nitarudi katika inchi yangu na kwa wandugu zangu.

31Musa akamwambia: Tafazali usituache, maana wewe unajua pahali tunapoweza kupiga kambi katika jangwa, na unaweza kuwa mwongozi wetu.

32Tena ukienda nasi chochote chema Yawe atakachotutendea, ndicho utakachotendewa nawe vilevile.

Safari inaanza

33Basi, watu wakasafiri toka Sinai, mulima wa Yawe, mwendo wa siku tatu. Sanduku la Agano la Yawe liliwatangulia mwendo wa siku tatu, kwa kuwatafutia pahali pa kupigia kambi.

34Kila mara waliposafiri kutoka kambi moja mpaka ingine, wingu la Yawe lilikuwa juu yao muchana.

35Kila wakati sanduku liliposafiri kwenda mbele, Musa alisema: Inuka, ee Yawe, uwatawanye waadui zako, na hao wanaokuchukia uwafanye wakimbie kutoka mbele yako. Ang. Zab 68.1

36Na kila wakati liliposimama, Musa alisema: Uwarudilie, ee Yawe, hawa maelfu na maelfu ya Israeli.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help