Hesabu 17 - Swahili Congo Revised Bible 2002

Vyetezo

1Nyuma ya hayo, Yawe akamwambia Musa:

2Umwambie Eleazari mwana wa kuhani Haruni atoe hivyo vyetezo kwenye moto, atupe mbali moto unaokuwa ndani, maana vyetezo hivyo ni vitakatifu.

3Vimekuwa vitakatifu kwa sababu watu hawa walivileta kwenye mazabahu ya Yawe. Basi, utwae vyetezo vya watu hao waliouawa kwa sababu ya zambi zao, vifuliwe kuwa vyembamba kusudi vikuwe kifuniko cha mazabahu. Hili litakuwa onyo kwa Waisraeli wote.

4Basi, kuhani Eleazari akatwaa vyetezo hivyo vya shaba ambavyo vililetwa mbele ya Yawe na wale watu walioteketezwa vikafuliwa kuwa kifuniko cha mazabahu.

5Hili lilikuwa onyo kwa Waisraeli kwamba mutu yeyote ambaye si kuhani, maana yake asiyekuwa wa ukoo wa Haruni asiende kwenye mazabahu kwa kumufukizia Yawe ubani. Kama sivyo ataangamizwa kama Kora na wafuasi wake. Haya yote yalitendeka kama vile Yawe alivyomwambia Eleazari kwa njia ya Musa.

Haruni anaokoa watu

6Kesho yake, Waisraeli wote pamoja wakamunungunikia Musa na Haruni wakisema: Mumewaua watu wa Yawe.

7Walipokusanyika mbele ya Musa na Haruni kwa kutoa malalamiko yao, wakageuka kuelekea hema la mukutano, wakaona kwamba wingu limeifunika hema na utukufu wa Yawe ulikuwa umetokea pale.

8Musa na Haruni wakakwenda, wakasimama mbele ya hema la mukutano, Ang. Ebr 9.4

9na Yawe akamwambia Musa:

10Ujitenge na watu hawa, niwaangamize mara moja!

Lakini wao wakajitupa uso mpaka chini.

11Musa akamwambia Haruni: Twaa chetezo chako, utie moto ndani yake na kukiweka kando ya mazabahu, kisha utie ubani halafu uende nacho haraka kwa watu na kuwafanyia upatanisho. Fanya haraka! Kasirani ya Yawe imekwisha kuwafikia na pigo limeanza kuwashambulia.

12Basi, Haruni akafanya kama vile alivyoambiwa na Musa. Akatwaa chetezo chake na kukimbia mpaka katikati ya watu waliokuwa wamekusanyika pamoja. Alipoona kwamba pigo limekwisha kuanza, akatia ubani katika chetezo na kuwafanyia watu upatanisho.

13Alipofanya hivyo, pigo hilo likakoma, naye akabaki katikati ya waliokufa na waliokuwa wazima.

14Hesabu ya watu waliokufa kwa pigo ilikuwa elfu kumi na ine mia saba, bila kuhesabu wale waliokufa kutokana na uasi wa Kora.

15Pigo lilipokoma, Haruni akarudi kwa Musa kwenye mulango wa hema la mukutano.

Fimbo ya Haruni

16Kisha Yawe akamwambia Musa:

17Uwaambie Waisraeli wakuletee fimbo kumi na mbili, kila kiongozi wa kabila fimbo moja. Uandike jina la kila mumoja wao kwenye fimbo yake,

18na jina la Haruni uliandike juu ya fimbo inayosimamia kabila la Lawi. Kutakuwa fimbo moja kwa kila kiongozi wa kabila.

19Upeleke fimbo hizo katika hema la mukutano na kuziweka mbele ya Sanduku la Agano, pahali ambapo mimi ninakutana nawe.

20Fimbo ya mutu nitakayemuchagua itachipuka. Kwa njia hii nitakomesha manunguniko ya Waisraeli juu yenu.

21Musa akaongea na watu wa Israeli. Viongozi wao wote wakamupa kila mumoja fimbo yake kulingana na kabila lake kwa jumla zikakuwa fimbo kumi na mbili. Fimbo ya Haruni ikawekwa pamoja na fimbo hizo.

22Musa akaziweka fimbo hizo zote mbele ya Yawe katika hema la mukutano.

23Kesho yake asubui, Musa akakwenda katika hema la mukutano. Mule, akakuta fimbo ya Haruni wa kabila la Lawi, imechipuka na kutoa vifundo vilivyochanua maua na kuzaa matunda mabichi ya lozi.

24Kisha Musa akatoa fimbo zote hapo mbele ya Yawe, akawaonyesha Waisraeli wote, na kila kiongozi akatwaa fimbo yake.

25Yawe akamwambia Musa: Urudishe fimbo ya Haruni mbele ya Sanduku la Agano. Hiyo itatunzwa pahali pale, na ni onyo kwa waasi hao kwamba wasipoacha kuninungunikia, watakufa.

26Musa akafanya kama vile alivyoamriwa na Yawe.

27Waisraeli wakamwambia Musa: Angalia sasa! Tunaangamia! Tumekwisha! Wote tumekwisha.

28Kila mutu atakayekaribia hema la Yawe atakufa. Tutaangamia sisi wote?

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help