Zaburi 22 - Swahili Congo Revised Bible 2002

Kilio

1Kwa mukubwa wa waimbaji. Mutindo wa wimbo “Swala wa mapambazuko”.

2Mungu wangu, Mungu wangu,

mbona umeniacha?

Mbona uko mbali sana kwa kunisaidia,

mbali na maneno ya kilio changu?

3Ee Mungu wangu, ninakulilia muchana lakini haujibu;

ninakulalamikia usiku, lakini sipumziki.

4Hata hivyo, wewe ni mutakatifu;

wewe unatawala na kusifiwa na Waisraeli.

5Babu zetu walikutegemea;

walikutegemea, nawe ukawaokoa.

6Walikulilia wewe, wakaokolewa;

walikutegemea, nao hawakufezeheka.

7Lakini mimi ni mududu tu, wala si mutu;

nimetukaniwa na kuzarauliwa na watu.

8Wote wanaoniona wananichekelea;

wananizomea na kutikisa vichwa vyao.

9Wanasema: “Alimutegemea Yawe,

basi, Mungu amuponyeshe!

Kama Mungu anapendezwa naye,

basi, amwokoe!”

10Lakini wewe ndiwe uliyenitoa katika tumbo la mama yangu,

uliniweka salama kwa kifua cha mama yangu.

11Nimekutegemea tangu kuzaliwa kwangu.

Tangu nilipozaliwa, wewe umekuwa Mungu wangu.

12Usikae mbali nami, kwa maana taabu imekaribia;

wala hakuna wa kunisaidia.

13Waadui wengi wananizunguka kama ngombe dume;

wamenisonga kama ngombe dume wanono wa Basani!

14Wanafungua vinywa vyao kama simba,

tayari kushambulia na kurarua.

15Nimekwisha kama maji yaliyomwangika;

mifupa yangu yote imeteguka;

moyo wangu ni kama inta,

unayeyuka ndani yangu.

16Koo langu limekauka kama kigae;

ulimi wangu unanata ndani ya kinywa changu.

Wewe umenilaza pembeni ya kaburi.

17Kundi la waovu limenizunguka;

wananizunguka kama kundi la imbwa;

wamenitoboa mikono na miguu.

18Nimebaki mifupa mitupu;

waadui zangu wananiangalia na kunisimanga.

19Wanagawanya nguo zangu,

na kuipigia kanzu yangu kura.

20Lakini wewe, ee Yawe, usikae mbali nami.

Ukuwe musaada wangu, ukuje haraka kunisaidia.

21Uokoe nafsi yangu toka upanga,

uokoe maisha yangu toka mikono ya imbwa hao!

22Uniokoe toka kinywa cha simba;

uokoe nafsi yangu zaifu toka pembe za mbogo hao.

Wimbo wa shukrani

23Nitawaelezea wandugu zangu matendo yako;

nitakusifu kati ya kusanyiko lao,

nikisema:

24“Enyi munaomwabudu Yawe, mumusifu!

Mumutukuze, enyi wazao wote wa Yakobo!

Mumwogope Mungu, enyi wazao wote wa Israeli!

25Maana yeye hatupilii au kuzarau taabu ya muzaifu;

wala hajifichi mbali naye,

lakini anamusikiliza anapomwomba musaada.”

26Kwa sababu yako ninakusifu

katika kusanyiko kubwa la watu;

nitatimiza ahadi zangu mbele ya wanaomwabudu.

27Wamasikini watakula na kushiba;

wanaomutafuta Yawe watamusifu.

Mungu awajalie waishi milele!

28Ulimwengu wote utakumbuka na kumurudilia Yawe;

jamaa zote za mataifa zitamwabudu.

29Maana Yawe ni mufalme;

yeye anatawala mataifa.

30Wenye kiburi wote katika dunia watamwabudu;

wote ambao ni wa kufa watainama mbele yake,

wote ambao hawawezi kudumisha uzima wao.

31Vizazi vyao vitamutumikia;

watu wataelezea kizazi kinachokuja habari za Yawe,

32watatangazia wale watakaozaliwa matendo yake ya wokovu.

Watu wasiozaliwa bado wataambiwa:

“Yawe ndiye aliyefanya hayo!”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help