1Kwa mukubwa wa waimbaji. Zaburi. Wimbo wa Daudi.
2Ee Mungu,
unastahili sifa huko Sayuni.
Watu wanapaswa kukutimizia viapo vyao,
3maana wewe unajibu maombi yetu.
Wanadamu wote watakuja kwako wewe peke.
4Tunapolemewa na makosa yetu,
wewe mwenyewe unatusamehe.
5Heri wale unaowachagua na kuwaleta karibu,
waishi katika kiwanja chako.
Sisi tutatoshelewa na mazuri ya nyumba yako,
mazuri ya hekalu lako takatifu.
6Kwa matendo yako makubwa unatuitikia na kutuokoa,
ewe Mungu mwokozi wetu.
Wewe ndiwe tumaini la viumbe vyote
katika dunia yote na mbali katika bahari.
7Kwa nguvu yako uliisimika milima pahali pake.
Wewe una nguvu nyingi!
8Unatuliza uvumi wa bahari na wa mawimbi yake,
unakomesha fujo za watu.
9Wakaaji wa miisho ya dunia wanashangazwa na vitambulisho vyako.
Unasababisha furaha kila pahali,
tokea mashariki hata magaribi.
10Wewe unatunza udongo kwa kuunyeshea mvua,
unaujalia mboleo na kuustawisha;
muto wako umejaa maji tele,
unaifanikisha inchi na kuipatia mavuno.
Hivi ndivyo unavyotayarisha udongo.
11Unanyeshea mashamba mvua kwa wingi,
na kuyalowanisha kwa maji;
unalainisha udongo kwa manyunyu,
na kubariki mimea ichipuke.
12Unakamilisha mwaka
kwa kutupatia mazao mazuri;
kila nafasi ulipopita kumejaa utajiri.
13Mbuga za majani zimejaa mifugo,
milima nayo imejaa furaha.
14Mashamba ya kulishia nyama yamejaa kondoo,
mabonde yamefunikwa na ngano.
Kila kitu kinashangilia kwa furaha.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.