Walawi 6 - Swahili Congo Revised Bible 2002

Sadaka za kuteketezwa kwa moto

1Yawe akamwambia Musa:

2Umupatie Haruni na wana wake maagizo haya: hii ndiyo sheria ya ibada juu ya sadaka ya kuteketezwa kwa moto. Sadaka ya kuteketezwa itakuwa kwenye moto juu ya mazabahu usiku kucha mpaka asubui na moto wake uchochewe, usizimike.

3Kisha kuhani akiwa amevaa nguo yake ya kitani na kapitula yake ya kitani, atatwaa majivu ya ile sadaka kutoka juu ya mazabahu na kuyaweka kando ya mazabahu.

4Halafu kisha kubadilisha nguo zake atapeleka yale majivu inje ya kambi pahali panapokuwa safi.

5Moto wa mazabahu lazima uendelee kuwaka wala usizimike. Kila siku asubui kuhani ataweka kuni kwenye moto huo na juu yake atapanga sadaka ya kuteketezwa, mbele ya kuteketeza mafuta ya sadaka ya amani.

6Moto utaendelea kuwaka siku zote juu ya mazabahu bila kuzimika hata kidogo.

Sadaka za vyakula

7Hii ndio sheria juu ya ibada inayoelekea sadaka ya vyakula. Wazao wa Haruni ndio wanaokuwa na uwezo wa kumutolea Yawe sadaka hiyo juu ya mazabahu.

8Mumoja wa makuhani atatwaa mukono mumoja wa unga wa sadaka ya vyakula pamoja na mafuta na ubani wote na kuviteketeza juu ya mazabahu kama vile sehemu ya ukumbusho. Harufu yake itamupendeza Yawe.

9Unga uliobakia Haruni na wazao wake makuhani wataukula bila kutiwa chachu. Wataukula kwenye Pahali Patakatifu katika kiwanja cha hema la mukutano.

10Usipikwe hata kidogo pamoja na chachu. Nimewapa wao sehemu hiyo kutoka sadaka wanazonitolea kwa moto. Ni sadaka takatifu kabisa kama vile sadaka kwa ajili ya zambi na kwa ajili ya kosa zinavyokuwa.

11Wazao wanaume wa Haruni ndio peke yao wanaoruhusiwa kula sehemu hiyo maana hiyo imetengwa siku zote kwa ajili yao kutoka sadaka Yawe anazotolewa kwa moto. Yeyote atakayezigusa atakuwa mutakatifu.

12Yawe akamwambia Musa:

13Tangu wakati wa kutakaswa kwa Haruni na wazao wake wanapaswa kumutolea Yawe kilo moja ya unga laini kwa siku, nusu moja ya unga huo ataitoa asubui na nusu ingine magaribi.

14Unga huo utachanganywa na mafuta na kupikwa juu ya kikaango. Kisha utauleta ukiwa vipandevipande na kumutolea Yawe na harufu ya sadaka yake itamupendeza Mungu.

15Kuhani anayekuwa muzao wa Haruni ambaye amepakwa mafuta kushika nafasi yake atamutolea Yawe sadaka hiyo. Hilo ni agizo la milele. Sadaka yote itateketezwa kwa moto.

16Sadaka yoyote ya ngano iliyotolewa na kuhani itateketezwa yote; haitakuliwa hata kidogo.

17Yawe akamwambia Musa:

18Umwambie Haruni na wana wake kwamba hii ndiyo sheria ya ibada kuelekea sadaka kwa ajili ya zambi, pahali ambapo nyama wa sadaka ya kuteketezwa anapochinjiwa ndipo atakapochinjiwa nyama wa sadaka kwa ajili ya zambi, mbele ya Yawe. Hiyo ni sadaka takatifu kabisa.

19Kuhani anayetolea sadaka hiyo ndiye atakayeikula. Itakuliwa katika Pahali Patakatifu, kwenye kiwanja cha hema la mukutano.

20Chochote kitakachogusa nyama hiyo kitakuwa kitakatifu. Nguo yoyote ikidondokewa na damu ya sadaka hiyo, basi, nguo hiyo itafuliwa katika Pahali Patakatifu.

21Sadaka hiyo ikipikiwa katika vyombo vya udongo, vyombo hivyo vitavunjwa. Lakini ikiwa vyombo hivyo ni vya shaba, basi, vitasafishwa vizuri kwa maji.

22Wanaoruhusiwa kuikula ni wanaume wa ukoo wa makuhani peke yao kwa vile hiyo ni sadaka takatifu kabisa.

23Lakini kama damu ya sadaka yoyote kwa ajili ya zambi imeletwa ndani ya hema la mukutano kwa kufanya ibada ya upatanisho katika Pahali Patakatifu, sadaka hiyo itateketezwa kwa moto.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help