Isaya 3 - Swahili Congo Revised Bible 2002

Fujo katika Yerusalema

1Sasa, Bwana wetu Yawe wa majeshi

ataondoa kutoka Yerusalema na inchi ya Yuda kila tegemeo:

tegemeo lote la chakula na la kinywaji.

2Ataondoa mashujaa na waaskari,

waamuzi na manabii,

waaguzi na wazee,

3majemadari na wakubwa,

washauri, wachawi wafundi na waganga wenye maarifa.

4Mungu anasema: Nitaweka watoto kuwa wakubwa wao;

watoto wachanga watawatawala.

5Watu watatesana,

kila mutu na mwenzake;

vijana watawazarau wazee,

na watu wa ovyo ovyo watawazarau wenye heshima.

6Wakati huo mutu atamwambia ndugu yake

wakiwa bado katika nyumba ya baba yao:

Wewe uko na nguo;

utakuwa mukubwa wetu.

Kamata utawala juu ya mabomoko haya!

7Lakini siku hiyo atasema:

Mimi siwezi kuwa muponyaji.

Ndani ya nyumba yangu hamuna chakula wala nguo.

Musinifanye mimi kuwa mukubwa wenu.

8Watu wa Yerusalema wamejikwaa,

watu wa Yuda wameanguka,

kwa sababu wanamupinga Yawe

kwa maneno na matendo,

wakizarau utukufu wake kati yao.

9Ubaguzi wao unashuhudia juu yao;

wanatangaza zambi yao kama vile watu wa Sodoma,

wala hawaifichi.

Ole kwao watu hao,

kwa sababu wamejiletea maangamizi wenyewe.

10Muwaambie watu wa haki jinsi wanavyokuwa na heri,

maana watakula matunda ya matendo yao.

11Lakini ole kwao watu waovu!

Mambo yatawaendekea vibaya,

maana yale waliyotenda yatawapata wao wenyewe.

12Watu wangu watateswa na watoto;

wanawake ndio watakaowatawala.

Enyi watu wangu, wakubwa wenu wanawapotosha,

wanavuruga njia munayopaswa kufuata.

Yawe anawahukumu watu wake

13Yawe yuko tayari kuanza mashitaki,

anasimama kwa kuwahukumu watu wake.

14Yawe anawashitaki

wazee na wakubwa wa watu wake:

Ninyi ndio mulioliharibu shamba la mizabibu;

mali wamasikini walizonyanganywa ziko ndani ya nyumba zenu.

15Muna haki gani kuwagandamiza watu wangu,

na kuwatendea wamasikini vibaya?

–Ni ujumbe wa Bwana wetu Yawe wa majeshi.

Maonyo kwa wanawake wa Yerusalema

16Yawe anasema:

Wanawake wa Sayuni wako na kiburi;

wanatembea wakiinua kichwa juu,

wakirembua macho yao kwa tamaa.

Hatua zao ni za maringo,

nao wanalilisha mikufu kwenye miguu yao.

17Basi, mimi Yawe nitawaazibu;

nitawanyoa nywele hao wanawake wa Sayuni,

na kuwavua nguo za kufunika uchi wao.

18Siku zinakuja ambapo Yawe atawanyanganya wanawake wa Yerusalema vitu vyote wanavyoringia: pete za miguu, vitana, mibano ya nywele,

19pete za masikio, vikomo na vitambaa vya ushungi,

20vitambaa vya kichwa, mikufu, mikaba iliyosokotwa, hirizi na mikufu ya kuleta bahati,

21pete za vidole na pua,

22nguo za sikukuu, kanzu, vitambaa vya kichwa na mifuko ya mikono,

23nguo nzuri, shemizi nzuri, vioo na vitambaa mbalimbali.

24Kwa pahali pa harufu ya marasi watatoa uvundo;

kwa pahali pa mikaba mizuri watatumia kamba;

kwa pahali pa nywele nzuri watakuwa na upaa;

kwa pahali pa nguo nzuri watavaa magunia;

uzuri wao wote utageuka kuwa haya.

25Wanaume wenu wataangamia kwa upanga,

watu wenu wenye nguvu watakufa katika vita.

26Halafu watu watalia na kuomboleza kwenye milango ya muji;

nao wataikaa ndani ya mavumbi katika ukiwa.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help