Yoshua 21 - Swahili Congo Revised Bible 2002

Miji ya Walawi

1Walipokuwa kule Shilo katika inchi ya Kanana viongozi wa ukoo za Walawi wakawaendea kuhani Eleazari na Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi wa jamaa za makabila yote ya Waisraeli,

2wakawaambia: “Yawe alimwagiza Musa kwamba tupewe miji ya kuishi na mbuga za malisho ya nyama wetu.” Ang. Hes 35.1-8

3Basi, kulingana na amri ya Yawe, Waisraeli walichagua kutoka katika maeneo ya inchi zao, miji na vijiji vya malisho, wakawapa Walawi ikuwe sehemu yao.

4Kura ya kwanza ilizipata jamaa za ukoo wa Kohati. Kati ya wazao wa kuhani Haruni walipewa kwa kura, miji iliyokuwa katika maeneo ya makabila ya Yuda, Simeoni, na Benjamina. Jumla ya miji waliyopewa ni kumi na mitatu.

5Watu wa ukoo wa Kohati waliobaki wakapewa miji kumi inayokuwa katika maeneo ya makabila ya Efuraimu, Dani na katika eneo la nusu ya kabila la Manase.

6Watu wa ukoo wa Gersoni wakapewa kwa kura miji kumi na mitatu katika maeneo ya makabila ya Isakari, Aseri, Nafutali na katika eneo la nusu ya kabila la Manase kule Basani.

7Jamaa za ukoo wa Merari wakapewa miji kumi na miwili katika maeneo ya makabila ya Rubeni, Gadi na Zebuluni.

8Waisraeli wakawapa Walawi miji hiyo pamoja na vijiji vya malisho yao, kama Yawe alivyomwagiza Musa.

9Haya ndiyo majina ya miji kutoka kwenye maeneo ya kabila la Yuda na Simeoni ambayo ilitolewa kwa

10wazao wa kuhani Haruni, waliokuwa jamaa za ukoo wa Kohati ambaye alikuwa wa kabila la Lawi. Sehemu yao walipata kwanza maana kura yao ilitokea kwanza.

11Wakapewa Kiriati-Arba, ni kusema Hebroni (Arba alikuwa baba ya Anaki), katika milima ya Yuda, pamoja na mbuga zilizoizunguka.

12Lakini mashamba ya muji ule pamoja na vijiji vilivyouzunguka vilikuwa vimekwisha kupewa kwa Kalebu mwana wa Yefune vikuwe mali yake.

13Zaidi ya kuwapa wazao wa kuhani Haruni muji wa Hebroni ambao vilevile ulikuwa umetengwa kuwa muji wa kukimbilia usalama, waliwapa miji ya Libuna pamoja na mbuga zake za malisho;

14Yatiri pamoja na mbuga zake za malisho, Estemoa pamoja na mbuga zake za malisho,

15Holoni pamoja na mbuga zake za malisho, Debiri pamoja na mbuga zake za malisho.

16Aini pamoja na mbuga zake za malisho, Yuta pamoja na mbuga zake za malisho na Beti-Semesi pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla ya miji hiyo inayokuwa katika maeneo ya makabila hayo mawili ni tisa.

17Katika eneo la kabila la Benjamina walipewa miji mingine: Gibeoni pamoja na mbuga zake za malisho,

18Anatoti pamoja na mbuga zake za malisho, Almoni pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla ya miji waliyopewa ni mine.

19Miji yote ya wazao wa Haruni ambao walikuwa makuhani, ilikuwa kumi na mitatu pamoja na mbuga zao za malisho.

20Watu waliobaki wa ukoo wa Kohati, ambao vilevile ni watu wa ukoo wa Lawi walipewa miji katika eneo la kabila la Efuraimu.

21Walipewa Sekemu, muji ambao ulikuwa vilevile muji wa kukimbilia usalama, pamoja na mbuga zake za malisho katika inchi ya milima ya Efuraimu, na Gezeri pamoja na mbuga zake za malisho,

22Kibusaimu pamoja na mbuga zake za malisho na Beti-Horoni pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla ya miji waliyopewa ni mine.

23Katika eneo la kabila la Dani walipewa Elteke pamoja na mbuga zake za malisho, Gibetoni pamoja na mbuga zake za malisho,

24Ayaloni pamoja na mbuga zake za malisho, na Gati-Rimoni pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla ya miji waliyopewa ni mine.

25Katika eneo la nusu ya kabila la Manase walipewa Tanaki pamoja na mbuga zake za malisho na Gati-Rimoni pamoja na malisho yake. Jumla ya miji waliyopewa ni miwili.

26Basi, miji ambayo walipewa watu wa ukoo wa Kohati iliyobaki ilikuwa kumi pamoja na mbuga zao za malisho.

27Watu wa uzao wa Lawi wa ukoo wa Gersoni, walipewa miji miwili katika nusu ya eneo la kabila la Manase: Golani, kule Basani, muji wa kukimbilia usalama, pamoja na mbuga zake za malisho, na Be-Estera pamoja na malisho yake.

28Katika eneo la kabila la Isakari, walipewa Kisioni pamoja na mbuga zake za malisho, Daberati pamoja na mbuga zake za malisho,

29Yarmuti pamoja na mbuga zake za malisho na Eni-Ganimu pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla ya miji waliyopewa ni mine.

30Katika eneo la kabila la Aseri walipewa Misali pamoja na mbuga zake za malisho, Abudoni pamoja na mbuga zake za malisho,

31Helkati pamoja na mbuga zake za malisho na Rehobu pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla ya miji waliyopewa ni mine.

32Katika eneo la kabila la Nafutali walipewa Kedesi, muji wa kukimbilia usalama unaokuwa kule Galilaya pamoja na mbuga zake za malisho, Hamoti-Dori pamoja na mbuga zake za malisho na Kartani pamoja na mbuga zake za malisho. Kwa jumla, miji mitatu.

33Jumla ya miji ya jamaa mbalimbali za ukoo wa Gersoni ilikuwa kumi na mitatu pamoja na mbuga zao za malisho.

34Walawi wengine waliobaki, ni kusema wazao wa Merari, walipewa miji katika eneo la kabila la Zebuluni. Nayo ni Yokinamu pamoja na mbuga zake za malisho, Karta pamoja na mbuga zake za malisho,

35Dimuna pamoja na mbuga zake za malisho na Nahalali pamoja na mbuga zake za malisho. Kwa jumla, miji mine.

36Katika eneo la kabila la Rubeni walipewa Bezeri pamoja na mbuga zake za malisho, Yahazi pamoja na mbuga zake za malisho,

37Kedemoti pamoja na mbuga zake za malisho na Mefati pamoja na mbuga zake za malisho. Kwa jumla, miji mine.

38Katika eneo la kabila la Gadi walipewa Ramoti wa Gileadi, muji wa kukimbilia usalama, pamoja na mbuga zake za malisho, Mahanaimu pamoja na mbuga zake za malisho,

39Hesiboni pamoja na mbuga zake za malisho na Yazeri pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla miji mine.

40Miji yote waliyopewa wazao wa Merari, ni kusema watu wa ukoo wa Walawi zilizobaki, ilikuwa kumi na miwili.

41Jumla ya miji yote ambayo Walawi walipewa katika maeneo ya Waisraeli ilikuwa makumi ine na nane pamoja na mbuga zao za malisho.

42Kila mumoja kati ya miji hii ulizungukwa na mbuga za malisho.

43Basi, Yawe aliwapa Waisraeli inchi yote ambayo alikuwa amewaahidi wazee wao. Nao wakairizi na kuishi mule.

44Yawe akawapa amani kila pahali katika inchi kama vile alivyowaapia wazee wao. Hakuna adui yeyote aliyesubutu kuwashambulia maana Yawe alikuwa amewatia waadui hao katika mikono yao.

45Hakuna hata ahadi yoyote njema ambayo Yawe aliiahidi Waisraeli ambayo haikutimia. Ahadi zote zilitimia.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help