1 Mambo ya Siku 10 - Swahili Congo Revised Bible 2002

Kifo cha mufalme Saulo(1 Sam 31.1-13)

1Siku moja, Wafilistini wakapigana vita na Waisraeli; nao Waisraeli wakakimbia mbele ya Wafilistini na kuuawa katika mulima wa Gilboa.

2Lakini Wafilistini wakamuzunguka Saulo na wana wake, kisha wakawaua Yonatani, Abinadabu na Malikisua wana wa Saulo.

3Vita ilikuwa kali sana juu ya Saulo. Wapiga mishale walipomwona wakamwumiza sana.

4Kwa hiyo Saulo akamwambia mutu aliyemubebea silaha: “Chomoa upanga wako unichome nikufe, kusudi watu hawa wasiotahiriwa wasikuje kunichekelea.” Lakini yule aliyemubebea silaha hakutaka kufanya vile; aliogopa sana. Halafu, Saulo alitwaa upanga wake mwenyewe akauangukia.

5Wakati yule aliyemubebea silaha alipoona kwamba Saulo amekufa, naye vilevile akauangukia upanga wake, akakufa.

6Hivi ndivyo Saulo alivyokufa, yeye na wana wake watatu, na jamaa yake yote.

7Nao watu wa Israeli walioishi katika bonde walipoona waaskari wamekimbia waadui, na kwamba Saulo na wana wake wamekufa, wakahama toka miji yao, wakakimbia. Wafilistini wakaenda na kukaa katika miji hiyo.

8Kesho yake, Wafilistini walipokwenda kutwaa vitu vya wale waliouawa, wakakuta maiti ya Saulo na wana wake kwenye mulima Gilboa.

9Wakamvua nguo, wakatwaa kichwa chake pamoja na silaha zake, halafu wakatuma wajumbe katika inchi yote ya Filistia kutangaza habari kwa sanamu zao na watu.

10Wakaweka silaha za Saulo katika hekalu la miungu yao, kisha wakatundika kichwa chake katika hekalu la Dagoni.

11Lakini watu wa Yebesi Gileadi waliposikia yote Wafilistini waliyomutendea Saulo,

12mashujaa wote wakaondoka na kutwaa mwili wa Saulo na miili ya wana wake, wakaileta mpaka Yabesi. Wakazika mifupa yao chini ya muti wa mwalo kule Yabesi, nao wakafunga kula kwa muda wa siku saba.

13Saulo alikufa kwa sababu ya kutokuwa mwaminifu; hakukuwa mwaminifu maana hakutii neno la Yawe na alikwenda kwa mwaguzi kumwomba shauri, Ang. Law 19.31; 20.6; 1 Sam 13.8-14; 15.1-24; 28.7-8

14pahali pa kumwendea Yawe kwa kumwomba shauri. Kwa sababu hiyo Yawe akamwua, na akamupa Daudi mwana wa Yese ufalme wake.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help