Zaburi 7 - Swahili Congo Revised Bible 2002

Maombi ya mutu anayeteswa

1Kwa mukubwa wa waimbaji. Wimbo wa malalamiko ya Daudi, aliomwimbia Yawe kwa ajili ya Kushi wa kabila la Benjamina.

2Ee Yawe, Mungu wangu,

ninakukimbilia wewe.

Uniokoe kutoka wote wanaonitesa,

uniponyeshe.

3Kama si vile, watakuja kunirarua kama simba,

kunipasua vipandevipande wala hakuna wa kuniokoa.

4Ee Yawe, Mungu wangu!

Kama nimetenda moja ya mambo haya:

kama nimechafua mikono yangu kwa ubaya,

5kama nimemurudishia rafiki yangu mabaya pahali pa mema,

au nimemunyanganya adui yangu bila sababu,

6basi, adui anifuatilie na kunikamata,

akomeshe maisha yangu

na kuuzika uzima wangu ndani ya mavumbi.

7Ee Yawe, kwa hasira yako,

simama sasa ukomeshe kasirani ya waadui zangu!

Amuka, ee Mungu wangu,

wewe umeamuru haki ifanyike.

8Ukusanye mataifa kandokando yako,

nawe uyatawale tokea kule juu.

9Wewe, ee Yawe, unayehukumu mataifa,

unihukumu kadiri ya haki yangu,

kulingana na ukamilifu wangu.

10Ukomeshe uovu wa watu wabaya,

uwaimarishe watu wa haki,

ee Mungu unayetenda haki,

unayejua siri za mioyo na mafikiri ya watu.

11Mungu ndiye ngao yangu;

yeye anawaokoa watu wenye moyo wa usawa.

12Mungu ni mwamuzi wa haki;

kila siku analaumu maovu.

13Watu wasipogeuka toka ubaya wao,

Mungu atanoa upanga wake;

atavuta upinde wake na kupima shabaha.

14Atatayarisha silaha zake za hatari,

na kuitia mishale yake moto.

15Mutu mubaya anatunga uovu,

anajaa uharibifu

na kuzaa udanganyifu.

16Anachimba shimo, na kulirefusha,

kisha anatumbukia humo yeye mwenyewe.

17Uharibifu wake utamurudilia yeye mwenyewe;

ukali wake utamwangukia yeye mwenyewe.

18Nitamushukuru Yawe kwa sababu ya haki yake;

nitaimba sifa za jina la Yawe, Mungu Mukubwa.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help