Hosea 11 - Swahili Congo Revised Bible 2002

Upendo wa Mungu unapita hasira yake

1Israeli alipokuwa mutoto, nilimupenda.

Kutoka Misri nilimwita mwana wangu.

2Lakini kadiri nilivyozidi kuwaita,

ndivyo walivyozidi kwenda mbali nami;

waliendelea kuyatambikia Mabali,

na kuvifukizia ubani sanamu za miungu.

3Mimi ndiye niliyemufundisha watu wa Efuraimu kutembea!

Mimi mwenyewe niliwatwaa katika mikono yangu;

lakini hawakutambua kwamba mimi ndiye niliyewatunza.

4Niliwaongoza kwa huruma,

nilishikamana nao kwa upendo;

kama baba anavyomunyanyua mutoto mpaka kwenye shavu lake,

ndivyo nami nilivyokuwa kwao.

Mimi niliinama chini na kuwakulisha.

5Basi, watarudi katika inchi ya Misri;

watatawaliwa na mufalme wa Asuria,

kwa sababu wamekataa kunirudilia.

6Upanga utavuma katika miji yao,

utavunjavunja miimo ya milango yake

na kuwaangamiza katika kuta zao.

7Watu wangu wamekusudia kuniacha mimi,

wakiitwa kusimama wapande juu,

hakuna hata mumoja anayeweza.

8Ewe Efuraimu, ninaweza kukuacha namna gani?

Ninaweza kukutupilia, ewe Israeli namna gani?

Nitaweza namna gani kukufanya kama muji wa Adama?

Nitaweza namna gani kukutendea kama Zeboimu!

Ninazuizwa na moyo wangu;

huruma yangu imezidi kuwa motomoto.

9Nitaizuia hasira yangu kali;

sitamwangamiza tena Efuraimu,

maana mimi ni Mungu, wala si mwanadamu.

Mimi ndimi Mutakatifu kati yenu,

nami sitakuja kuwaangamiza.

10Watanifuata mimi Yawe ninayenguruma kama simba;

nitakaponguruma watanifikia toka magaribi wakitetemeka.

11Watakuja kutoka Misri wakitetemeka kama ndege,

wataruka kutoka Asuria kama njiwa

nami nitawarudisha kwao.

–Ni ujumbe wa Yawe.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help