Zaburi 27 - Swahili Congo Revised Bible 2002

Kwa Mungu kuna usalama

1Zaburi ya Daudi.

Yawe ni mwangaza wangu na wokovu wangu,

ni nani nitakayemwogopa?

Yawe ni mulinzi wa maisha yangu,

sitamwogopa mutu yeyote.

2Waovu wakinishambulia,

na kutaka kuniangamiza,

hao wapinzani wangu watajikwaa na kuanguka.

3Hata jeshi likinizunguka,

moyo wangu hautaogopa kitu;

hata nikishambuliwa kwa vita,

sitakata tumaini.

4Jambo moja nimemwomba Yawe,

ninatafuta hili tu:

nikae ndani ya nyumba ya Yawe

siku zote za maisha yangu,

niuone uzuri wa Yawe,

na kutafuta maongozi yake ndani ya hekalu lake.

5Siku ya taabu atanificha ndani ya nyumba yake;

atanificha katika hema lake,

atanilinda salama juu ya mulima.

6Nami nitawaangalia kwa majivuno

waadui zangu wanaonizunguka.

Nitamutolea Yawe sadaka kwa shangwe,

ndani ya hekalu lake,

nitaimba na kumushangilia.

Musaada unapatikana kwa Mungu

7Usikie, ee Yawe, ninapokulilia,

unionee huruma na kunijibu.

8Moyo wangu unaniambia: “Kuja umutafute Mungu!”

Basi, ninakutafuta, ee Yawe.

9Usinigeuzie mugongo,

usinikatae kwa hasira mimi mutumishi wako.

Wewe umekuwa siku zote musaada wangu.

Usinitupe wala usiniachilie, ee Mungu Mwokozi wangu.

10Hata kama wazazi wangu wakinitupa,

Yawe atanipokea kwake.

11Unifundishe njia yako, ee Yawe.

Uniongoze katika njia inayokuwa sawa

kwa sababu ya waadui zangu.

12Usiniache waadui wanitendee wanavyopenda;

maana washuhuda wa uongo wananiinukia,

nao wanatoa vitisho vyao vikali.

13Ninaamini kwamba nitauona uzuri wa Yawe

katika makao ya wazima.

14Umutegemee Yawe!

Ujitie moyo, ukuwe hodari!

Umutegemee Yawe!

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help