1Kwa mukubwa wa waimbaji. Zaburi ya Daudi, mutumishi wa Mungu, aliyomwimbia wakati alipomwokoa katika mikono ya Saulo na waadui wengine.
2Ninakupenda,
ee Yawe, nguvu yangu!
3Yawe ni
kikingio changu,
kimbilio langu,
mukombozi wangu,
Mungu wangu,
yule ambaye ninamukimbilia,
ngao yangu,
nguvu ya wokovu wangu,
munara wangu.
4Ninamwita Yawe anayestahili sifa anisaidie,
nami ninaokolewa kutoka waadui zangu.
5Kamba za kifo zilinizunguka,
mafuriko ya maangamizi yalinishambulia;
6kamba za kuzimu zilinizunguka,
mitego ya kifo ilikuwa mbele yangu.
7Katika taabu yangu, nilimwita Yawe;
nilimulilia Mungu wangu anisaidie.
Toka katika hekalu lake, alisikia sauti yangu;
kilio changu kilimufikia katika masikio yake.
8Halafu dunia ikatetemeka na kutikisika,
misingi ya milima ikayumbayumba na kutetemeka,
kwa maana Mungu alikuwa amekasirika.
9Moshi ulifuka kutoka katika pua lake,
moto wenye kuteketeza ukatoka katika kinywa chake,
makaa ya moto yakatokea.
10Aliinamisha anga, akashuka chini,
na wingu jeusi lilikuwa chini ya miguu yake.
11Alipanda juu ya kerubi na kuruka,
akaruka juu ya mabawa ya upepo.
12Alijifunika giza pande zote,
alijizungushia mawingu mazito ya mvua.
13Umeme ulimetameta mbele yake;
na katika mawingu kukatokea mvua ya mawe na makaa ya moto.
14Yawe alinguruma kutoka mbingu;
Mungu Mukubwa akatoa sauti yake.
15Aliwapiga waadui mishale yake, akawatawanya;
alirusha umeme mukali, akawakimbiza.
16Ee Yawe, ulipovikaripia,
pumzi ya pua yako
ilifunua vilindi vya bahari
na misingi ya dunia ikaonekana.
17Mungu alinyoosha mukono wake kutoka juu, akanitwaa,
alininyanyua kutoka ndani ya maji mengi.
18Aliniokoa kutoka adui yangu mwenye nguvu,
kutoka hao walionichukia na kuwa na nguvu kunishinda.
19Walinishambulia nilipokuwa katika taabu,
lakini Yawe alinikinga.
20Alinileta, akaniweka kwenye nafasi ya usalama;
aliniponyesha kwa sababu alipendezwa nami.
21Yawe alinitendea kwa kadiri ya haki yangu;
alinilipa kwa vile mikono yangu haina kosa.
22Maana nimefuata njia za Yawe,
wala sikujitenga na Mungu wangu kwa ajili ya uovu.
23Nimeshika maagizo yake yote,
sikuacha kufuata masharti yake.
24Mbele yake nilikuwa mukamilifu;
nimejikinga nisikuwe na kosa.
25Yawe amenilipa kwa kadiri ya haki yangu;
kwa kadiri ya usafi wa mikono yangu mbele yake.
26Wewe ni mwema kwa wema,
mukamilifu kwa wakamilifu,
27bila kosa kwa wale ambao hawafanyi makosa,
lakini mukali kwa waovu.
28Wewe unawaokoa wanyenyekevu,
lakini unawashusha wenye macho ya kujivuna.
29Wewe, ee Yawe, unawakisha taa yangu.
Mungu wangu anafanya giza langu likuwe mwangaza.
30Kwa musaada wako, ninashinda kundi la waaskari;
kwa musaada wa Mungu wangu, ninaruka kuta.
31Njia ya Mungu ni kamilifu.
Ahadi ya Yawe ni ya kuaminika.
Yeye ni ngao kwa wote wanaomukimbilia.
32Nani anayekuwa Mungu isipokuwa Yawe?
Nani anayekuwa kikingio isipokuwa Mungu wetu?
33Ni Mungu ambaye ananipatia nguvu,
na kuifanya salama njia yangu.
34Ameiimarisha miguu yangu kama ya swala,
na kunilinda salama juu ya milima.
35Ananifundisha kupigana vita,
mikono yangu iweze kuvuta upinde wa chuma.
36Umenipa ngao yako ya wokovu
na kuniimarisha kwa mukono wako wa kuume.
Nimefanikiwa kwa sababu ulikubali kunisaidia.
37Umepanua njia yangu
wala miguu yangu haikuteleza.
38Niliwafuata waadui zangu na kuwakamata;
sikurudi nyuma mpaka wamemalizika.
39Niliwaangamiza,
wasiweze kuinuka tena;
walianguka chini ya miguu yangu.
40Wewe ulinijalia nguvu ya kupigana vita;
uliwaporomosha waadui chini yangu.
41Uliwakimbiza waadui zangu,
na wale walionichukia niliwaangamiza.
42Walitafuta musaada, lakini hakukukuwa wa kuwasaidia;
walimulilia Yawe, lakini hakuwajibu.
43Niliwatwanga, wakakuwa kama vumbi inayopeperushwa na upepo;
niliwakanyaga kama matope katika barabara.
44Wewe uliniokoa kutoka mashambulizi ya watu,
ukanifanya kuwa mutawala wa mataifa.
Watu nisiowajua walinitumikia.
45Waliposikia tu habari zangu, walinitii;
wageni walinijia wakinyenyekea.
46Wageni walivunjika moyo;
wakakuja kutoka makimbilio yao wakitetemeka.
47Yawe anaishi!
Yeye ni kikingio changu – asifiwe!
Mungu ni mwokozi wangu – atukuzwe!
48Yeye ameniwezesha kulipiza kisasi;
na kuwaweka mataifa chini ya mamlaka yangu.
49Ameniokoa kutoka waadui zangu,
Ee Yawe, ulinitukuza juu ya wapinzani wangu
na kuniponyesha kutoka watesaji wakali.
50Kwa hiyo, nitakutukuza kati ya mataifa,
nitaliimbia sifa jina lako.
51Mungu anamujalia mufalme wake ushindi mukubwa;
anamutendea mema muchaguliwa wake,
ndiye Daudi na wazao wake milele.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.