1Wakati mwezi wa saba ulipofika, na watu wa Israeli wakiwa wamekwisha kukaa katika miji yao, wote wakakusanyika pamoja katika Yerusalema.
2Yesua mwana wa Yosadaki, pamoja na makuhani wenzake, na Zerubabeli, mwana wa Sealtieli, pamoja na wandugu zake, wakaijenga upya mazabahu ya Mungu wa Israeli, kusudi waweze kumutolea sadaka za kuteketezwa kwa moto kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Musa, mutu wa Mungu. Ang. Kut 27.1
3Wakaijenga mazabahu hiyo pahali palepale ilipokuwa hapo zamani, kwa kuwa waliwaogopa watu waliokuwa wanaishi katika inchi hiyo. Kisha wakakuwa wanamutolea Yawe sadaka za kuteketezwa kwa moto juu yake kila siku asubui na magaribi. Ang. Hes 29.1-8
4Wakafanya sikukuu ya vibanda kama ilivyoandikwa katika Sheria; kila siku walitoa sadaka za kuteketezwa kwa moto zilizohitajika kwa ajili ya siku hiyo. Ang. Hes 28.12-38
5Walitoa vilevile sadaka za kawaida ambazo ziliteketezwa nzima, sadaka zilizotolewa wakati wa sikukuu ya mwandamo wa mwezi na katika sikukuu nyingine zote alizoagiza Yawe. Vilevile walitoa sadaka zote za mapenzi. Ang. Hes 28.11–29.39
6Ingawa musingi wa hekalu la Yawe ulikuwa bado kuwekwa, watu walianza kutoa sadaka za kuteketezwa kwa moto tangu siku ya kwanza ya mwezi wa saba.
7Watu walitoa feza za kuwalipa waseremala na wajengaji, walitoa vilevile chakula, vinywaji na mafuta, kusudi vipelekwe katika miji ya Tiro na Sidona kubadilishwa na miti ya mierezi kutoka Lebanoni. Miti hiyo ililetwa kwa njia ya bahari mpaka Yopa. Haya yote yalifanyika kwa musaada wa mufalme Kiro wa Persia.
8Basi, watu wakaanza kazi katika mwezi wa pili wa mwaka wa pili nyuma ya kufikia kwenye nyumba ya Mungu katika Yerusalema. Zerubabeli, mwana wa Saltieli, Yesua mwana wa Yosadaki, wandugu zao wengine, makuhani, Walawi na watu wengine wote waliorudi Yerusalema kutoka katika uhamisho, wakajiunga nao katika kazi hiyo. Walawi wote waliokuwa na umri wa miaka makumi mbili au zaidi, walichaguliwa kwa kusimamia kazi ya kuijenga upya nyumba ya Yawe.
9Yesua, wana wake na jamaa yake, pamoja na Kadimieli na wana wake, (wa ukoo wa Yuda) walishirikiana kwa kusimamia ujenzi wa nyumba ya Mungu. Wakasaidiwa na wazao wa Henadadi na wandugu zao Walawi.
10Wajengaji walipoanza kuweka musingi wa hekalu la Yawe, makuhani wakiwa wamevaa nguo zao, walisimama pahali pao na baragumu katika mikono, nao Walawi wa ukoo wa Asafu wakisimama na matoazi yao, basi, wakamutukuza Yawe kufuatana na maagizo ya mufalme Daudi wa Israeli. Ang. 1 Sik 25.1
11Wakaimba kwa kupokezana, wakimusifu na kumutukuza Yawe:
“Yeye ni muzuri,
wema wake kwa Waisraeli unadumu milele.”
Watu wote walipaza sauti kwa nguvu zao zote, wakamusifu Yawe kwa sababu ya kuanza kujenga musingi wa nyumba ya Yawe. Ang. 1 Sik 16.36; 2 Sik 5.13; 7.3; Zab 100.5; 106.1; 107.1; 118.1; 136.1; Yer 33.11
12Wengi kati ya makuhani, Walawi, na viongozi wa ukoo waliokuwa wazee na ambao walikuwa wameiona nyumba ya kwanza, wakalia kwa sauti kubwa walipouona musingi wa nyumba hii mupya unawekwa, ingawa watu wengine wengi walipaza sauti kwa furaha.
13Watu hawakuweza kutofautisha kati ya sauti za furaha na za kilio kwa sababu zilikuwa nyingi na zilisikilika mbali sana.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.