Zaburi 88 - Swahili Congo Revised Bible 2002

Kilio cha musaada

1Kwa mukubwa wa waimbaji. Zaburi ya Wakora: Kwa mutindo wa wimbo wa huzuni. Mashairi ya Hemani Mwezra.

2Ee Yawe, mwokozi wangu,

ninalia muchana kutwa, na usiku ninakulalamikia.

3Maombi yangu yakufikie,

usikilize kilio changu.

4Hasara inanipita kipimo,

nami niko karibu kufa.

5Ninaonekana kama mutu anayeshuka katika shimo la wafu.

Nguvu zangu zote zimeniishia.

6Ninahesabiwa kati ya wafu,

kama waliouawa, wanaokuwa katika kaburi,

kama wale ambao hauwakumbuki tena,

ambao wametengwa na ulinzi wako.

7Umenitupa mbali katika shimo la wafu,

katika giza kubwa.

8Hasira yako imenilemea;

umenisonga kwa zoruba yako yote.

9Umewafanya warafiki zangu waniepuke,

umenifanya kuwa chukizo kwao.

Nimefungwa wala siwezi kutoroka.

10Macho yangu yamefifia kwa huzuni.

Kila siku ninakulilia, ee Yawe.

Ninakunyooshea mikono yangu.

11Wewe unawatendea wafu maajabu yako?

Waliokufa wanafufuka na kukusifu?

12Wema wako unatajwa ndani ya kaburi,

au uaminifu wako katika shimo la kuangamia?

13Maajabu yako yanajulikana humo katika giza,

au matendo yako ya haki katika inchi ya waliosahauliwa?

14Mimi ninakulilia, ee Yawe.

Kila asubui ninakuletea ombi langu.

15Mbona, ee Yawe, unanitupilia mbali?

Kwa nini unanificha uso wako?

16Nimeteseka na kukaribia kifo tangu ujana wangu;

ninateseka kwa mapigo yako, niko tabani kabisa.

17Kasirani yako imeniwakia;

mashambulio yako ya kutisha yananiangamiza.

18Yananizunguka kama mafuriko muchana kutwa;

yananizunguka yote pamoja.

19Umewafanya warafiki na wenzangu wote waniepuke;

giza ndilo limekuwa mwenzangu.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help