1Umusifu Yawe, ee nafsi yangu!
Ee Yawe, Mungu wangu, wewe ni mukubwa kabisa!
Umevaa utukufu na mamlaka.
2Umejifunika mwangaza kama kanzu,
umekunjua mbingu kama hema;
3umejenga makao yako katika mbingu juu ya maji.
Umeyafanya mawingu kuwa gari lako
nawe unatembea katika anga.
4Unaufanya upepo kuwa mujumbe wako,
moto na ndimi zake kuwa watumishi wako.
5Umeiweka dunia imara juu ya misingi yake,
isitikisike hata milele.
6Uliifunika dunia kwa bahari kama nguo,
na maji yakaimeza milima mirefu.
7Ulipoyakaripia, yalikimbia;
yaliposikia ngurumo yako, yalitelemuka mbio.
8Yaliporomoka toka milima mpaka katika mabonde,
mpaka pahali ulipoyatengenezea.
9Uliyawekea hayo maji mipaka
yasiyoweza kutambuka,
kusudi yasifunike tena dunia.
10Umetokeza chemichemi katika mabonde,
na vijito vyao vinapita kati ya vilima.
11Hivyo vinakunywesha wanyama wote wa pori,
na humo punda wa pori wanatulizia kiu chao.
12Ndege wanajenga chicha zao katika miti ya hapo,
wanatua katika matawi yake na kuimba.
13Toka juu angani, unainyeshea milima mvua,
nayo dunia unaishibisha kwa baraka yako.
14Unaotesha majani kwa ajili ya mifugo,
na mimea kwa matumizi ya mwanadamu
kusudi naye apate chakula chake toka udongo:
15apate divai ya kumuchangamusha,
mafuta ya muzeituni ya kumwangarisha,
na mukate wa kumupa nguvu.
16Miti mikubwa ya Yawe inapata maji ya kutosha;
ndiyo mierezi ya Lebanoni aliyoipanda.
17Humo, ndege wanajenga chicha zao,
korongo wanafanya makao yao katika misunobari.
18Milima mirefu ni makao ya mbuzi wa pori;
makimbilio ya sungura wa pori ni chini ya mawe.
19Umeumba mwezi kwa kutupimia nyakati,
nalo jua linalojua wakati wa kutua.
20Unaleta giza, nao usiku unaingia;
nao wanyama wote wa pori wanatoka:
21simba wakali wananguruma wanapokosa mawindo yao,
wanakungojea wewe Mungu uwape chakula chao.
22Jua linapopanda, wanarudi kwao,
na kujipumzisha ndani ya mapango yao.
23Hapo mwanadamu naye anaenda kwenye kazi zake;
naye anatumika mpaka magaribi.
24Ee Yawe, matendo yako ni mengi sana!
Umeyafanya kwa hekima yote!
Dunia imejaa viumbe vyako!
25Mbali kule kuna bahari kubwa na pana,
ambamo kumejaa viumbe visivyokuwa na hesabu,
viumbe vizima, vikubwa na vidogo.
26Mashua zinasafiri humo,
na yule nyama mukubwa Leviatani
uliyemwumba achezee humo.
27Hao wote wanakungojea wewe,
uwapatie chakula chao kwa wakati wake.
28Wanaokota kitu chochote unachowapa;
ukiwafungulia mukono, wanashiba vyakula vizuri.
29Ukiwageuzia mugongo, wanaogopa;
ukiondoa pumzi yao, wanakufa
na kurudi ndani ya mavumbi walimotoka.
30Ukiwapulizia pumzi yako, wanaumbwa;
wewe unafanya vitu vipya katika dunia.
31Utukufu wa Yawe unadumu hata milele;
Yawe anapendezwa na matendo yake mwenyewe.
32Anaiangalia dunia, nayo inatetemeka;
anagusa milima, nayo inatoa moshi!
33Nitamwimbia Yawe maisha yangu yote;
nitamusifu Mungu wangu muda wote nitakaoishi.
34Upendezwe na hayo mashairi yangu, ee Yawe,
maana wewe ndiye furaha yangu.
35Wenye zambi wote waondolewe katika dunia,
waovu wote wasikuwe tena!
Umusifu Yawe, ee nafsi yangu!
Haleluia!
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.