1Waisraeli wakaanza safari tena, wakaenda kupiga kambi yao katika bonde za Moabu, upande wa mashariki wa muto Yordani, kuelekea muji wa Yeriko.
2Mufalme Balaki mwana wa Sipori, alijua mambo yote Waisraeli waliyowatendea Waamori.
3Yeye pamoja na Wamoabu wakashikwa na hofu kubwa juu ya Waisraeli. Waliwaogopa hasa kwa sababu ya wingi wao.
4Basi Wamoabu wakawaambia viongozi wa Midiani: Makundi haya ya watu sasa hivi yataharibu kila kitu kandokando yetu kama vile ngombe dume anavyokula majani katika shamba. Kwa hiyo, Balaki mwana wa Sipori aliyekuwa mufalme wa Moabu wakati ule,
5akapeleka ujumbe kwa Balamu mwana wa Beori, huko Petori, karibu na muto Furati katika inchi ya Amawi. Akamwambia Balamu hivi: Kuna taifa ambalo limetoka Misri, nalo limeenea kila pahali katika inchi, tena linatishia kutwaa inchi yangu. Ang. Hes 31.8; 2 Pet 2.15-16; Yuda 11
6Kuja sasa uwalaani watu hawa kwa ajili yangu maana wana nguvu kuliko mimi. Labda nitaweza kuwashinda na kuwafukuza wasiingie katika inchi yangu, kwa maana unajua kwamba wewe ukimubariki mutu anabarikiwa, ukimulaani mutu analaaniwa.
7Basi, wazee wa Moabu na Midiani wakapeleka zawadi za uaguzi, wakaondoka kwenda kwa Balamu. Walifika, wakamupa Balamu ujumbe wa Balaki.
8Balamu akawaambia: Mulale huku usiku huu, nami nitawajulisha vile Yawe atakayoniambia. Basi, wazee hao wa Moabu wakakaa na Balamu.
9Kisha Mungu alimufikia Balamu, akamwuliza: Ni nani hawa wanaokaa nawe?
10Balamu akamujibu Mungu: Balaki mwana wa Sipori amenitumia ujumbe kwamba
11kuna watu wa taifa fulani waliotoka Misri, nao wameenea kila pahali katika inchi. Ameniomba niende kuwalaani watu hao kusudi pengine ataweza kupigana nao na kuwafukuza.
12Mungu akamwambia Balamu: Usiende pamoja na watu hawa, wala usiwalaani watu hao maana wamebarikiwa.
13Basi, asubui yake Balamu akaamuka, akawaambia wazee wa Balaki: Murudie katika inchi yenu, kwa maana Yawe hapendi kuniruhusu kwenda pamoja nanyi.
14Kwa hiyo wazee wa Moabu wakaondoka, wakarudi kwa Balaki, wakamwambia: Balamu amekataa kuja pamoja nasi.
15Kisha, Balaki akatuma wakubwa wengine, wengi zaidi na wa vyeo vya juu kuliko wale wa kwanza.
16Hao wakafika kwa Balamu, wakamwambia: Balaki mwana wa Sipori anasema hivi: Usikubali kuzuiwa na chochote hata uache kuja kwangu.
17Nitakupatia heshima kubwa, na chochote utakachoniomba nitakutimizia. Kuja uwalaani watu hawa.
18Lakini Balamu akawajibu watumishi wa Balaki: Hata kama Balaki atanipa nyumba yake imejaa feza na zahabu, mimi sitaweza kuvunja amri ya Yawe, Mungu wangu, juu ya jambo lolote, dogo au kubwa.
19Lakini tafazali mulale hapa usiku huu kama wale wenzenu, nami nipate kujua kile Yawe atakachoniambia tena.
20Basi, Mungu akamufikia Balamu usiku ule, akamwambia: Kama watu hawa wamekuja kukuita, kwenda pamoja nao, lakini fanya tu kile nitakachokuambia.
21Balamu akaamuka asubui, akatandika punda wake, akaenda pamoja na hao wakubwa.
Balamu, punda na malaika22Hasira ya Mungu ikawaka kwa sababu Balamu alikuwa anakwenda; hivyo malaika wa Yawe akakutana naye katika njia. Wakati huo Balamu alikuwa amepanda juu ya punda wake naye alisindikizwa na watumishi wake wawili.
23Basi, punda akamwona malaika huyo wa Yawe amesimama katika njia, akishika upanga uliochomolewa. Kwa hiyo akaacha njia, akaenda pembeni. Balamu akamupiga huyo punda, akamurudisha katika njia.
24Kisha malaika huyo wa Yawe akatangulia mbele, akasimama pahali hiyo njia ilikuwa nyembamba, kati ya mashamba ya mizabibu na kuta pande zote mbili.
25Punda alipomwona malaika huyo wa Yawe, akajibanisha kwenye ukuta na kubana muguu wa Balamu hapo. Kwa hiyo Balamu akamupiga tena huyo punda.
26Kisha malaika akatangulia tena, akasimama pahali pembamba pasipo na nafasi ya kupita kuume wala kushoto.
27Punda alipomwona huyo malaika wa Yawe, akalala chini. Balamu akawaka hasira, akamupiga kwa fimbo yake.
28Hapo Yawe akafungua kinywa cha huyo punda, akamwambia Balamu: Nimekutendea nini hata ukanipiga mara hizi tatu?
29Balamu akamwambia punda: Wewe umenichekelea! Kama ningekuwa na upanga ningalikuua sasa hivi!
30Punda akamwambia Balamu: Mimi si yuleyule punda wako aliyekubeba maisha yako yote mpaka siku hii ya leo? Nimekwisha kukutendea namna hii? Balamu akajibu: Hapana.
31Hapo, Yawe akafungua macho ya Balamu, naye akamwona malaika wa Yawe amesimama katika njia, akishika upanga uliochomolewa toka kifuko chake. Balamu akajitupa uso mpaka chini.
32Malaika wa Yawe akamwambia Balamu: Mbona umemupiga punda wako mara tatu? Nimekuja kukuzuia, kwa sababu njia yako ni mbaya.
33Punda wako ameniona akaniepuka mara tatu. Kama asingaligeuka mbali nami hakika ningalikuua wewe na kumwacha muzima punda huyu.
34Balamu akamwambia malaika wa Yawe: Nimetenda zambi maana sikujua kwamba umesimama katika njia kwa kunizuia. Sasa, kama haikupendezi niendelee na safari hii, basi nitarudi kwangu.
35Lakini malaika wa Yawe akamwambia Balamu: Kwenda na watu hawa, lakini utasema tu kile nitakachokuambia. Basi, Balamu akaendelea na safari pamoja na viongozi wa Balaki.
36Balaki alipopata habari kwamba Balamu anakuja, akatoka kwenda kumupokea katika muji wa Ari, muji uliokuwa kwenye ukingo wa muto Arnoni kwenye mupaka wa Moabu.
37Balaki akamwambia Balamu: Kwa nini haukukuja kwangu mara moja nilipokuita? Ulifikiri sitaweza kukupatia heshima ya kutosha?
38Balamu akamujibu Balaki: Sasa nimekuja! Lakini, nina mamlaka ya kusema neno lolote? Jambo Mungu atakaloniambia ndilo ninalopaswa kusema.
39Basi, Balamu akaenda pamoja na Balaki. Wakafika katika muji Kiriati-husoti.
40Huko Balaki akatoa sadaka ya ngombe na kondoo, akawagawanyia Balamu na wakubwa waliokuwa pamoja naye nyama.
Balamu anawabariki Waisraeli41Kesho yake, Balaki akamutwaa Balamu, akapanda naye mpaka Bamoti-Bali; kutoka huko, Balamu aliweza kuwaona wamoja kati ya Waisraeli.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.