Isaya 54 - Swahili Congo Revised Bible 2002

Upendo wa Mungu kwa Israeli

1Yawe anasema hivi:

Imba kwa shangwe, ewe unayekuwa tasa,

wewe ambaye haujapata kuzaa!

Piga kelele na kuimba kwa nguvu,

wewe usiyepata kuzaa mutoto.

Maana watoto wako wewe uliyeachwa

watakuwa wengi kuliko wa yule anayekuwa na mume.

2Panua nafasi katika hema yako,

ongeza mapazia ya makao yako,

usijali mali unayotumia.

Urefushe kamba zako,

na kuimarisha misumari yako;

3maana utapanuka kila upande;

wazao wako watarizi mataifa,

miji iliyokuwa ukiwa itajaa watu.

4Usiogope, hautapata haya tena.

Usifazaike, hautazarauliwa tena.

Utaisahau haya uliyopata katika ujana wako,

wala hautakumbuka tena mazarau ya ujane wako.

5Muumba wako atakuwa mume wako.

Jina lake Yawe wa majeshi.

Mukombozi wako ni Mutakatifu wa Israeli.

Yeye anaitwa Mungu wa Ulimwengu Wote.

6Yerusalema, Yawe amekuita tena.

Ulikuwa kama vile muke aliyeachwa na kuhuzunika.

Mungu wako anasema:

Muke aliyeolewa akiwa kijana, anaweza kuachiliwa?

7Nilikuacha kwa muda mufupi tu.

Kwa huruma nyingi, nitakurudisha.

8Kwa hasira nyingi nilikuficha uso wangu kwa muda kidogo,

lakini kwa wema wa milele nitakuonea huruma.

Ni Yawe Mukombozi wako anayesema hivyo.

9Nitafanya kama nilivyofanya wakati wa Noa.

Wakati ule niliapa kwamba

sitaifunika tena dunia kwa mafuriko ya maji.

Basi sasa ninaapa kwamba sitakukasirikia tena

wala sitakukaripia tena.

10Milima inaweza kutoweka,

vilima vinaweza kuondolewa,

lakini rehema zangu kwako sitaziacha,

agano langu la amani litaimarishwa.

Ni Yawe anayekuhurumia anayesema hivyo.

Yerusalema mupya

11Ewe Yerusalema, uliteseka,

ulitaabishwa na kukosa wa kukufariji,

lakini nitakujenga upya kwa mawe ya bei kali,

misingi yako itakuwa ya mawe ya yakuti.

12Minara yako nitaijenga kwa mawe ya akiki,

milango yako kwa almasi,

na ukuta wako kwa mawe ya bei kali.

13Watu wako watafundishwa nami Yawe,

wana wako watapata ustawi mwingi.

14Utaimarishwa katika haki,

mbali na kaoneo,

nawe hautaogopa kitu;

mbali na hofu,

maana haitakukaribia.

15Mutu yeyote akikuja kukushambulia,

hatakuwa ametumwa nami.

Yeyote atakayekushambulia,

ataangamia mbele yako.

16Mimi ndiye niliyemwumba mufuaji wa vyuma,

anayewasha moto wa makaa na kufua silaha.

Ni mimi vilevile niliyemwumba mwangamizaji anayeangamiza.

17Silaha zote zilizotengenezwa kwa kukuzuru wewe

hazitafaa kwa kitu chochote.

Mutu akikushitaki, utamushinda.

Hiyo ndiyo haki niliyowapangia watumishi wangu.

Hizo ndizo haki nilizowahakikishia.

–Ni ujumbe wa Yawe.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help