Zaburi 147 - Swahili Congo Revised Bible 2002

Inafaa kumusifu Mungu

1Haleluia!

Kweli ni vizuri kumwimbia Mungu wetu sifa!

Inapendeza na inastahili kumwimbia.

2Yawe anajenga tena Yerusalema;

anawarudisha Waisraeli waliopelekwa katika uhamisho.

3Anawaponyesha waliovunjika moyo;

na kuwatunza vidonda vyao.

4Anakadirisha hesabu ya nyota,

na kupanga kila moja jina.

5Bwana wetu ni mukubwa, ana nguvu nyingi;

maarifa yake hayana kipimo.

6Yawe anawashikilia wanyenyekevu,

lakini anawaangusha waovu katika mavumbi.

7Mumwimbie Yawe nyimbo za shukrani,

mumupigie Mungu wetu kinubi!

8Yeye anafunika anga kwa mawingu,

anaitayarishia inchi mvua,

na kuchipukiza nyasi kwenye vilima.

9Anawapa nyama chakula chao,

na kulisha vitoto vya kibombobombo vinapomulilia.

10Yeye hafurahii nguvu za farasi,

wala hapendezwi na ushujaa wa waaskari;

11lakini anapendezwa na watu wanaomuheshimu,

ndio wanaotegemea wema wake.

12Umusifu Yawe, ee Yerusalema!

Umusifu Mungu wako, ee Sayuni!

13Maana yeye alikaza vifungio vya milango ya kuta zako,

anawabariki watu wanaokuwa ndani yako.

14Analeta amani katika eneo lako;

anakushibisha kwa ngano safi kabisa.

15Yeye anatuma amri yake katika dunia,

na neno lake linafikia shabaha yake kwa haraka.

16Ananyesha teluji inayoangaa kama pamba,

anasambaza umande kama majivu.

17Anaangusha mvua ya mawe kama makokoto,

hakuna anayeweza kuvumilia baridi anayoituma.

18Anapoamuru, hayo mawe yanayeyuka;

anapovumisha upepo, maji yanatiririka.

19Anatoa ujumbe wake kwa wazao wa Yakobo,

nayo masharti na maagizo yake kwa Waisraeli.

20Lakini hakuyatendea hivyo mataifa;

wao hawajui maagizo yake.

Haleluia!

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help