1Heri watu wanaoishi katika ukamilifu,
wanaofuata sheria ya Yawe.
2Heri wanaoshika maagizo yake,
wanaomutafuta kwa moyo wao wote,
3watu wasiotenda uovu hata kidogo,
lakini wanafuata siku zote njia zake.
4Ee Mungu, umetupatia kanuni zako
kusudi tuzishike kwa uangalifu.
5Heri mwenendo wangu ungeimarika
kwa kuyafuata masharti yako!
6Nikichunguza amri zako zote,
hapo kweli sitapata haya.
7Nitakusifu kwa moyo wenye kunyooka,
nikijifunza maamuzi yako ya haki.
8Nitafuata masharti yako;
usiniache hata kidogo.
Kutii sheria ya Mungu9Namna gani kijana ataweza kujichunga katika njia safi?
Ni kwa kufuatilia neno lako.
10Ninakutafuta kwa moyo wote;
usiniachilie kugeuka mbali na amri zako.
11Nimeshika neno lako ndani ya moyo wangu,
kusudi nisikukosee.
12Utukuzwe, ee Yawe!
Unifundishe masharti yako.
13Nitarudiliarudilia kwa sauti
maamuzi yako yote uliyotoa.
14Ninafurahi kufuata maagizo yako,
kuliko kuwa na utajiri mwingi.
15Ninafikiri juu ya kanuni zako,
na kuangalia njia zako.
16Ninafurahia masharti yako;
sitasahau neno lako.
Kufurahia sheria ya Mungu17Unitendee mimi mutumishi wako kwa wema,
nipate kuishi na kushika neno lako.
18Uyafungue macho yangu,
nipate kuona maajabu ya sheria yako.
19Mimi ni mugeni tu hapa katika dunia;
usinifiche amri zako.
20Roho yangu inaugua kwa hamu kubwa
ya kutaka kujua siku zote maamuzi yako.
21Wewe unawakaripia wenye kiburi waliolaaniwa,
ambao wanageuka mbali na amri zako.
22Uniepushe na matusi na mazarau yao,
maana ninafuata maagizo yako.
23Hata kama wakubwa wananifanyia shauri baya,
mimi mutumishi wako nitafikiri juu ya masharti yako.
24Maagizo yako ndiyo furaha yangu;
hayo ndio washauri wangu.
Kushika sheria ya Mungu25Ninagaagaa chini ndani ya mavumbi;
unirudishie uzima sawa ulivyoahidi.
26Nimeungama niliyotenda, nawe ukanijibu;
unifundishe masharti yako.
27Unifundishe namna ya kushika kanuni zako,
nami nitafikiri juu ya matendo yako ya ajabu.
28Ninalia kwa uchungu;
unirudishie nguvu kama ulivyoahidi.
29Uniepushe na njia za upotovu;
unifundishe kwa huruma sheria yako.
30Nimechagua njia ya uaminifu;
nitafuatilia maamuzi yako.
31Ninashikamana na maagizo yako, ee Yawe;
usikubali nipatishwe haya!
32Nitafuatilia amri zako,
maana unanifungua akili zaidi.
Kuomba hekima33Ee Yawe, unifundishe kutii masharti yako,
nami nitayashika mpaka mwisho.
34Unieleweshe nipate kushika sheria yako,
niifuate kwa moyo wangu wote.
35Uniongoze katika njia ya amri zako,
maana humo ninapata furaha yangu.
36Uvute moyo wangu kufuata maagizo yako,
na si kwa ajili ya kupata faida isiyofaa.
37Uniepushe nisifuate mambo ya ovyo;
unionyeshe njia yako, unipe uzima.
38Unitimizie mimi mutumishi wako ahadi yako;
ahadi unayowapa wale wanaokuheshimu.
39Uniepushe na matusi ninayoogopa;
maana maamuzi yako ni mema.
40Ninatamani sana kutii kanuni zako;
unirudishie uzima maana wewe ni wa haki.
41Wema wako unifikie, ee Yawe;
uniokoe kama ulivyoahidi.
42Hapo nitaweza kuwajibu hao wanaonitukana,
maana mimi ninatumainia neno lako.
43Unijalie kusema ukweli wako siku zote,
maana ninatumainia maamuzi yako.
44Nitatii sheria yako siku zote,
nitaishika milele na milele.
45Nitaishi katika uhuru kamili,
maana ninashugulika na kanuni zako.
46Nitawatangazia wafalme maagizo yako,
wala sitaona haya.
47Furaha yangu ni kuzitii amri zako,
ambazo mimi ninazipenda.
48Ninaziheshimu na kuzipenda amri zako;
nitafikiri juu ya masharti yako.
Kuaminia sheria ya Mungu49Ukumbuke ahadi yako kwangu mimi mutumishi wako,
ahadi ambayo imenipa matumaini.
50Hata katika taabu, inanituliza,
maana ahadi yako inanipa uzima.
51Wasiomujali Mungu wananizarau siku zote,
lakini mimi sigeuki mbali na sheria yako.
52Ninapokumbuka maamuzi yako ya tangu zamani,
ninafarijika, ee Yawe.
53Ninashikwa na hasira kali,
ninapoona waovu wakivunja sheria yako.
54Masharti yako yamekuwa wimbo wangu,
nikikuwa huku kama mugeni.
55Usiku ninakukumbuka, ee Yawe,
na kushika sheria yako.
56Hili ni pato langu,
kwamba ninashika kanuni zako.
Heshima kwa sheria ya Mungu57Wewe, ee Yawe, ndiwe hitaji langu lote;
ninaahidi kushika maneno yako.
58Ninataka kukupendeza kwa moyo wangu wote;
unionee huruma kama ulivyoahidi!
59Nimefikiri juu ya mwenendo wangu,
na nimerudi nifuate maagizo yako.
60Bila kukawia ninafanya haraka
kushika amri zako.
61Waovu wametega mitego waninase,
lakini mimi sisahau sheria yako.
62Usiku kati ninaamuka kwa kukusifu,
kwa sababu ya maamuzi yako ya haki.
63Mimi ni rafiki ya wote wanaokuheshimu,
rafiki ya wanaoshika kanuni zako.
64Dunia imejaa wema wako, ee Yawe,
unifundishe masharti yako.
Ukamilifu wa sheria ya Mungu65Umenitendea vizuri mimi mutumishi wako,
kama ulivyoahidi, ee Yawe.
66Unipe hekima na ufahamu,
maana ninaaminia amri zako.
67Mbele sijateswa nilikuwa nimepotea,
lakini sasa ninashika neno lako.
68Wewe ni muzuri na unatenda mazuri;
unifundishe masharti yako.
69Wenye kiburi wanasema uongo juu yangu,
lakini mimi ninashika kanuni zako kwa moyo wote.
70Mioyo yao inafungana sana,
lakini mimi ninafurahia sheria yako.
71Nimefaidika kutokana na taabu yangu,
maana imeniwezesha kujifunza masharti yako.
72Sheria uliyoweka ni bora kwangu,
kuliko mali zote za dunia.
Ukamilifu wa sheria ya Mungu73Kwa mikono yako wewe mwenyewe uliniumba;
unijalie akili nijifunze amri zako.
74Wanaokuheshimu wataniona na kufurahi,
maana tumaini langu liko katika neno lako.
75Ninajua kwamba maamuzi yako ni ya haki, ee Yawe,
na kwamba umeniazibu maana wewe ni mwaminifu.
76Wema wako unifariji,
kama ulivyoniahidi mimi mutumishi wako.
77Unionee rehema nipate kuishi,
maana sheria yako ni furaha yangu.
78Wenye kiburi wafezeheke, maana wananisumbua na maneno ya uongo,
lakini mimi nitafikiri juu ya kanuni zako.
79Wote wanaokuheshimu wakuje kwangu,
wapate kujua maagizo yako.
80Moyo wangu ukuwe mukamilifu juu ya masharti yako,
kusudi nisifezeheke.
Kuteswa81Ninachoka kwa kukungojea uniokoe;
ninatumainia neno lako.
82Macho yangu yanafifia nikingojea ulichoahidi.
Ninauliza: “Utakuja wakati gani kunifariji?”
83Nimekunjamana kama mufuko wa ngozi katika moshi,
hata hivyo sijasahau masharti yako.
84Mimi mutumishi wako nitavumilia mpaka wakati gani?
Utawaazibu wakati gani wale wanaonitesa?
85Wenye kiburi wamenichimbia mashimo,
watu ambao hawafuati sheria yako.
86Amri zako zote ni za kuaminiwa;
watu wananitesa bila haki; unisaidie!
87Walifikia karibu ya kuniangamiza,
lakini mimi sikuvunja kanuni zako.
88Kwa wema wako, unirudishie uzima,
nipate kufuata maagizo uliyotangaza.
Sheria ya Mungu ni ya kutegemewa89Neno lako, ee Yawe, linadumu milele;
linasimama imara mbinguni.
90Uaminifu wako unadumu kwa vizazi vyote,
umeweka dunia pahali pake, nayo inadumu.
91Kwa amri yako viumbe vyote viko leo,
maana vitu vyote ni chini ya mamlaka yako.
92Kama sheria yako isingekuwa furaha yangu,
ningalikwisha kuangamia kwa taabu zangu.
93Sitasahau hata kidogo kanuni zako,
maana kwa njia yao unanirudishia uzima.
94Mimi ni wako, uniokoe,
maana nimejitoa kushika kanuni zako.
95Waovu wananivizia wapate kuniua;
lakini mimi ninafikiri juu ya maagizo yako.
96Nimetambua kwamba kila kitu kina mwisho,
lakini amri yako haina mupaka.
Kupenda sheria ya Mungu97Ninapenda sana sheria yako!
Ninafikiri juu yake muchana kutwa!
98Amri yako iko nami siku zote,
inanipa hekima kuliko waadui zangu.
99Ninaelewa kuliko walimu wangu wote,
kwa sababu ninafikiri juu ya maagizo yako.
100Ninawapita wazee kwa akili yangu,
kwa sababu ninashika kanuni zako.
101Ninajizuiza kufuata njia mbaya,
kusudi nipate kushika neno lako.
102Sikugeuka mbali na maamuzi yako,
maana wewe mwenyewe ulinifundisha.
103Maagizo yako ni matamu sana kwangu;
ni matamu kuliko asali!
104Kwa kanuni zako ninapata hekima,
kwa hiyo ninachukia kila mwenendo mubaya.
Sheria ya Mungu ni mwangaza105Neno lako ni taa ya kuniongoza,
na mwangaza katika njia yangu.
106Nimeapa na kuhakikisha kiapo changu,
kwamba nitashika maamuzi yako ya haki.
107Ee Yawe, ninateseka sana;
unirudishie uzima kama ulivyoahidi.
108Ee Yawe, upokee maombi yangu ya shukrani,
na kunielezea maamuzi yako.
109Maisha yangu yako katika hatari siku zote,
lakini sisahau sheria yako.
110Waovu wamenitegea mitego,
lakini sigeuki mbali na kanuni zako.
111Maagizo yako ni urizi mukubwa kwangu milele;
hayo ni furaha ya moyo wangu.
112Nimekusudia kwa moyo wote
kufuata masharti yako milele.
Usalama katika sheria ya Mungu113Ninachukia watu wanafiki,
lakini ninapenda sheria yako.
114Wewe ni ngao yangu, na kimbilio langu;
ninaweka tumaini langu katika neno lako.
115Muondoke kwangu, enyi waovu,
kusudi nipate kushika amri za Mungu wangu.
116Uniimarishe sawa ulivyoahidi, nami nitaishi;
usikubali nifezeheke katika tumaini langu.
117Unishike nipate kuwa salama,
nikuwe siku zote musikilivu kwa masharti yako.
118Unawakataa wote wanaogeuka mbali na masharti yako;
mawazo yao maovu ni ya bure.
119Unaona waovu wote kama vile takataka,
kwa hiyo mimi ninapenda maagizo yako.
120Ninatetemeka kwa kukuogopa wewe;
nimejaa hofu kwa sababu ya maamuzi yako.
Utii wa sheria ya Mungu121Nimefanya mambo mema na ya haki;
usiniache katika makucha ya waadui zangu.
122Uhakikishe kunisaidia mimi mutumishi wako;
usikubali wenye kiburi wanitese.
123Macho yangu yanafifia nikingojea uniokoe,
nikingojea utimize uliyoahidi.
124Unitendee mimi mutumishi wako kadiri ya wema wako,
unifundishe masharti yako.
125Mimi ni mutumishi wako.
Unipe akili nipate kujua maagizo yako.
126Ee Yawe, sasa ni wakati wa kutenda kitu,
kwa maana watu wanavunja sheria yako.
127Kweli, ninapenda amri zako,
kuliko hata zahabu safi kabisa.
128Kwa hiyo, ninafuata kanuni zako zote;
ninachukia kila njia ya upotovu.
Hamu ya kutii sheria za Mungu129Maagizo yako ni ya ajabu;
kwa hiyo ninayashika kwa moyo wote.
130Maelezo ya mafundisho yako yanaleta mwangaza;
yanawapa akili wajinga.
131Ninafungua kinywa kwa hamu kubwa,
maana ninatamani sana amri zako.
132Unigeukie na kunionea huruma,
kama unavyowatendea wanaokupenda.
133Uniimarishie hatua zangu kama ulivyoahidi;
usikubali mimi nitawaliwe na uovu.
134Unikomboe kutoka mateso ya wanadamu,
kusudi nipate kushika kanuni zako.
135Uniangazie uso wako kwa wema,
unifundishe masharti yako.
136Macho yangu yanatiririka machozi kama muto,
kwa sababu watu hawaishiki sheria yako.
Ukamilifu wa sheria ya Mungu137Ee Yawe, wewe ni wa haki;
na hukumu zako ni za usawa.
138Umetoa maagizo yako,
kwa haki na uaminifu.
139Upendo wangu kwako unanifanya niwake hasira,
maana waadui zangu hawajali maneno yako.
140Ahadi yako ni hakika kabisa,
nami mutumishi wako ninaipenda.
141Mimi ni mudogo na ninazarauliwa;
hata hivyo sisahau kanuni zako.
142Haki yako ni haki ya milele;
sheria yako ni ya kweli.
143Taabu na huzuni vimenipata,
lakini amri zako ndizo furaha yangu.
144Maagizo yako ni ya haki siku zote;
unijalie akili nipate kuishi.
Kuomba usalama145Ninakulilia kwa moyo wangu wote;
unijibu, ee Yawe, nifuate masharti yako.
146Ninakulilia, uniokoe
nipate kushika maagizo yako.
147Ninaamuka mbele ya mapambazuko na kukuomba musaada;
ninaweka tumaini langu katika maneno yako.
148Ninakaa macho wazi usiku kucha,
kusudi nifikiri juu ya ahadi zako.
149Kwa wema wako, ee Yawe, unisikilize;
kwa haki yako, unirudishie uzima.
150Wale wanaonitesa vibaya wanakaribia,
hao wako mbali kabisa na sheria yako.
151Lakini wewe ni karibu nami, ee Yawe,
na amri zako zote ni za kuaminiwa.
152Tangu zamani, nimejifunza maagizo yako
ambazo umeziweka hata zidumu milele.
Kuomba musaada153Uangalie mateso yangu, uniokoe,
kwa maana sikusahau sheria yako.
154Unitetee na kunikomboa;
unirudishie uzima kama ulivyoahidi.
155Waovu hawataokolewa hata kidogo,
maana hawajali juu ya masharti yako.
156Rehema yako ni kubwa, ee Yawe,
unirudishie uzima kama ulivyoahidi.
157Waadui na watesaji wangu ni wengi,
lakini mimi sigeuki mbali na maagizo yako.
158Ninapowaona waasi hao ninachukizwa sana,
kwa sababu hawashiki amri zako.
159Angalia, ee Mungu, ninavyopenda kanuni zako!
Unirudishie uzima kadiri ya wema wako.
160Kifungo cha neno lako ni ukweli,
maamuzi yako yote ya haki yanadumu milele.
161Wakubwa wananitesa bila sababu,
lakini mimi ninaheshimu maneno yako kwa moyo wote.
162Ninafurahi kwa sababu ya neno lako,
kama mutu aliyekuta kitu cha bei kali.
163Ninachukia kabisa uongo,
lakini ninapenda sheria yako.
164Ninakusifu mara saba kila siku,
kwa sababu ya maamuzi yako ya haki.
165Wanaopenda sheria yako wana amani kubwa;
hakuna kinachoweza kuwaangusha.
166Ee Yawe, ninakungojea uniokoe;
mimi ninatimiza amri zako.
167Ninashika maagizo yako;
ninayapenda kwa moyo wote.
168Ninashika kanuni na maagizo zako;
wewe unaona mwenendo wangu wote.
Kuomba musaada169Kilio changu kikufikie, ee Yawe!
Unijalie akili kama ulivyoahidi.
170Ombi langu likufikie;
uniokoe kama ulivyoahidi.
171Midomo yangu itatangaza sifa zako,
maana unanifundisha masharti yako.
172Nitaimba juu ya neno lako,
maana amri zako zote ni za haki.
173Ukuwe siku zote tayari kunisaidia,
maana nimeamua kufuata kanuni zako.
174Ninatamani sana uniokoe, ee Yawe;
sheria yako ndiyo furaha yangu.
175Unijalie kuishi nipate kukusifu;
na maamuzi yako yanisaidie.
176Ninatangatanga kama kondoo aliyepotea;
ukuje kunitafuta mimi mutumishi wako,
maana sikusahau amri zako.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.