1Yawe akawapa Musa na Haruni, maagizo haya:
2Waisraeli watapiga kambi zao, kila mumoja akikaa pahali penye bendera yake, penye vitambulisho vya ukoo wake. Watapiga kambi zao kuzunguka na kuelekea hema la mukutano.
3Wale watakaopiga kambi upande wa mashariki watakuwa kikundi cha watu wanaokuwa chini ya bendera ya Yuda na kiongozi wao atakuwa Nasoni mwana wa Aminadabu.
4Jeshi lake kulingana na hesabu ni wanaume elfu makumi saba na ine na mia sita.
5Wale watakaofuata kupiga kambi nyuma ya watu wa Yuda watakuwa kabila la Isakari. Kiongozi wao atakuwa Netaneli mwana wa Suari.
6Jeshi lake kulingana na hesabu ni wanaume elfu makumi tano na ine na mia ine.
7Kisha kabila la Zebuluni, kiongozi wao akiwa Eliabu mwana wa Heloni,
8jeshi lake kulingana na hesabu ni wanaume elfu makumi tano na saba na mia ine.
9Jumla yote ya watu watakaokuwa katika kambi ya Yuda kulingana na jeshi lake ni watu elfu mia moja makumi nane na sita na mia ine. Hao ndio watakaotangulia kusafiri.
10Kwa upande wa kusini, wale wanaokuwa chini ya bendera ya kundi la Rubeni kulingana na jeshi lake, kiongozi wao akiwa Elisuri mwana wa Sedeuri,
11jeshi lake kulingana na hesabu ni wanaume elfu makumi ine na sita na mia tano.
12Kisha wale watakaopiga kambi kando ya watu wa Rubeni watakuwa ni watu wa kabila la Simeoni, kiongozi wao akiwa Selumieli mwana wa Suri-Sadai,
13jeshi lake kulingana na hesabu ni wanaume elfu makumi tano na tisa na mia tatu.
14Halafu kabila la Gadi, kiongozi wao akiwa Eliasafu mwana wa Reueli,
15jeshi lake kulingana na hesabu ni wanaume elfu makumi ine na tano mia sita na makumi tano.
16Jumla ya wanaume watakaokuwa katika kambi ya Rubeni kulingana na jeshi lake ni watu elfu mia moja makumi tano na moja mia ine na makumi tano. Hawa ndio watakaokuwa katika kundi la pili.
17Halafu, kambi ya kabila la Walawi likiwa katikati ya kambi zote nao wakibeba hilo hema la mukutano wataondoka; kila kundi likisafiri kwa kufuata nafasi yake kwa bendera.
18Kwa upande wa magaribi, wale wanaokuwa chini ya bendera ya kundi la Efuraimu watapiga kambi kulingana na jeshi lake kiongozi wao akiwa Elisama mwana wa Amihudi,
19jeshi lake kulingana na hesabu ni wanaume elfu makumi tatu na mbili na mia mbili.
20Mara tu nyuma ya Waefuraimu litafuata kabila la Manase: kiongozi wake akiwa Gamalieli mwana wa Pedasuri,
21jeshi lake kulingana na hesabu litakuwa watu elfu makumi tatu na mbili na mia mbili.
22Kisha kabila la Benjamina: kiongozi wake ni Abidani, mwana wa Gideoni,
23jeshi lake kulingana na hesabu ni wanaume elfu makumi tatu na tano na mia ine.
24Jumla ya watu waliokuwa katika kambi ya Efuraimu kulingana na jeshi lake ni watu elfu mia moja na nane na mia moja. Hawa ndio watakaokuwa katika kundi la tatu.
25Kwa upande wa kaskazini, watapiga kambi katika jeshi lake wale wanaokuwa chini ya bendera ya Dani, kiongozi wao atakuwa Ahiezeri, mwana wa Amishadai,
26jeshi lake kulingana na hesabu litakuwa na watu elfu makumi sita na mbili na mia saba.
27Kisha wale watakaopiga kambi nyuma yao watakuwa watu wa kabila la Aseri, kiongozi wao akiwa Pagieli mwana wa Okrani,
28jeshi lake kulingana na hesabu litakuwa na watu elfu makumi ine na moja na mia tano.
29Kisha watu wa kabila la Nafutali, kiongozi wake akiwa Ahira mwana wa Enani,
30jeshi lake kulingana na hesabu, ni wanaume elfu makumi tano na tatu na mia ine.
31Jumla ya watu waliokuwa katika kambi ya Dani kulingana na jeshi lake ni watu elfu mia makumi tano na saba na mia sita. Hawa ndio watakaokuwa katika kundi la mwisho nyuma ya bendera zao.
32Hao ndio Waisraeli waliohesabiwa kulingana na ukoo zao, katika kambi na majeshi yao, wote walikuwa elfu mia sita na tatu na mia tano makumi tano.
33Lakini Walawi hawakuhesabiwa kati ya watu wa Israeli kama vile Yawe alivyomwamuru Musa.
34Hivi ndivyo, Waisraeli walivyofanya kila kitu kama vile Yawe alivyomwamuru Musa. Wakapiga kambi zao, kufuata bendera zao na wakasafiri kila mumoja akiandamana na jamaa yake kwa kufuata ukoo wake.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.