Wimbo mkuu 8 - Swahili Roehl Bible 1937

Welekevu wao wote wawili mpendwa mume na mpenzi wake mke.

1Laiti ungekuwa kama umbu aliyeyanyonya maziwa ya mama yangu!

Kama ningekukuta nje ningekunonea

pasipo kuona watu watakaonibeza.

2Ningekuongoza, nikupeleke nyumbani mwa mama yangu,

ungenifundisha; kisha ningekunywesha mvinyo yenye viungo,

nayo ni mbichi iliyotengenezwa kwa komamanga zangu.

3Mkono wake wa kushoto ungekuwa chini ya kichwa changu,

nao wa kuume ungenikumbatia.

4Nawaapisha ninyi, wanawake wa Yerusalemu,

msimwamshe, wala msimhangaishe yeye, ninayempenda,

ila mwacheni tu, mpaka atakapopendezwa mwenyewe.

5“Ni nani huyu mke apandaye kutoka nyikani

akimwegemea mpendwa wake?”

“Chini ya mchungwa nilikuamsha;

ndipo, mama yako aliposhikwa na uchungu

alipokuzaa na kuona uchungu.

6Na uniweke moyoni mwako kama pete yenye muhuri!

Na uniweke napo mkononi pako kama pete yenye muhuri!

Kwani upendo ni wenye nguvu kama kifo,

hushupaa kama kuzimu kwa wivu,

miali yake ni miali ya moto,

ni moto uwakao kwa kuwashwa na Bwana.

7Maji mengi hayawezi kuuzima upendo, majito makuu hayautosi,

Kama mtu angezitoa mali zote zilizomo nyumbani mwake

kwa kwamba: apate kupendwa, watu wangemsimanga kabisa.”

Tumepata ndugu wa kike mdogo,

8naye maziwa yake hayako bado;

sasa huyu ndugu yetu wa kike tumfanyie nini siku atakapoposwa?

9“Tutajenga juu yake kingio la fedha, kama yeye ni ukuta,

lakini kama ni mlango tutaufunga kwa mbao za miangati.”

10Mimi ni ukuta, nayo maziwa yangu ni kama minara.

Kwa hiyo nikawa machoni pake mahali patokeapo utulivu.

11Salomo alikuwa na shamba la mizabibu huko Baali-Hamoni,

naye akawakodisha walinzi hilo shamba la mizabibu,

kila mtu amtolee fedha elfu kwa matunda yake.

12Shamba langu la mizabibu ni langu, ninaliangalia mimi;

zile fedha ninakuachia wewe, Salomo,

tena mia mbili za kuwapa wao wayalindao matunda yake.

13“Wewe ukaaye bustanini, wenzako huisikiliza sauti yako;

itoe namo masikioni mwangu mimi!”

14Kimbia, mpendwa wangu, kama paa au kijana wa kulungu

warukao milimani kwenye manukato!

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help