Wimbo mkuu 4 - Swahili Roehl Bible 1937

Uzuri wa mpenzi mke.

1Nikikutazama, mpenzi wangu, u mwanamke mzuri,

nikikutazama, u mwanamke mzuri kweli,

macho yako huwa ya hua yakichungulia katika mtandio wako;

nywele zako zinafanana na kundi la mbuzi

walalao upande wa kushukia wa mlimani kwa Gileadi.

2Meno yako ni kama kundi la kondoo waliokatwa manyoya,

wanaopanda na kutoka majini wakiisha kuogeshwa,

wote pia ni wenye wana wa pacha,

kwao hakuna hata mmoja aliye peke yake.

3Midomo yake ni kama uzi wenye rangi nyekundu,

kinywa chako kinapendeza nacho.

Shavu lako huonekana mtandioni mwako

kuwa kama komamanga ipevukayo sana.

4Shingo yako ni kama mnara wa Dawidi uliojengewa selaha,

vigao elfu viko vimeangikwa kwake,

vyote pia ni vya kuwakingia mafundi wa vita.

5Maziwa yako mawili yanafanana na vitoto viwili vya kulungu

au na wana wa pacha wa paa walishwao penye nyinyoro.

6Mpaka jua la mchana lipunguke ukali, vivuli vijiendee mbiombio,

ndipo, nitakapokwenda zangu mlimani kwenye manemane,

hata kilimani kwenye uvumba.

7Wewe, mpenzi wangu, u mzuri peke yako, huna doadoa kabisa.”

8Toka Libanoni, mchumba wangu, twende pamoja!

Toka Libanoni, twende pamoja, njoo!

Tazama, huko juu Amana nako juu Seniri na Hermoni

ndiko, simba wanakokaa, hata machui wako kule milimani.

9Umenipokonya moyo wangu, uliye umbu na mchumba wangu;

umenipokonya moyo wangu, kwa kunitazama na jicho lako moja tu,

ukanifunga kwa kikufu kimoja, unachokivaa shingoni pako.

10Ni kuzuri mno kukumbatiana na wewe,

uliye umbu langu na mchumba wangu;

kukumbatiana na wewe kunapendeza kuliko kunywa mvinyo,

mnuko wa mafuta yako ni mzuri kuliko wa manukato yote.

11Midomo yako, mchumba wangu, inadondoka asali safi,

asali na maziwa ndiyo yaliyoko chini ya ulimi wako,

nao mnuko wa mavazi yako ni mzuri kama wa Libanoni.

12Umbu langu aliye mchumba wangu ni bustani iliyofungwa,

ni kisima kilichofungwa,

ni chemchemi iliyozibwa na kutiwa muhuri.

13Machipukizi yako ni kimwitu cha mikomamanga

izaayo matunda yapendezayo sana, nayo mihina na miafu iko.

14Iko hata mianjano na mikumbi na mikoroshi na midalasini,

miti yote itokayo uvumba na manemane nayo mishubiri iko,

tena iko miti yote itokayo manukato yapitayo mengine.

15Nayo chemchemi iko bustanini na kisima chenye maji ya uzima

na vijito vitokavyo Libanoni.”

16Inuka, upepo wa kaskazini! Njoo, upepo wa kusini!

Vuma bustanini mwangu, minuko yake mizuri ifurikie!

17Mpendwa wangu aingie bustanini pake,

ayale matunda yake yapendezayo!

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help