Matendo 24 - Bible in Kiswahili, Revised Union Version 2013

Paulo mbele ya Feliki katika Kaisaria

1Baada ya siku tano, Anania, Kuhani Mkuu, akateremka na baadhi ya wazee pamoja naye, na msemi mmoja, Tertulo, nao wakamweleza mtawala habari za Paulo.

2Naye alipoitwa, Tertulo akaanza kumshitaki, akisema, Kwa kuwa mnapata amani nyingi chini yako, Feliki mtukufu, na kwa uongozi wako mambo mabaya yanasuluhishwa kwa ajili ya taifa hili,

3Mdo 23:26; 26:25 basi tunayapokea kila wakati na kila mahali, kwa shukrani yote.

4Lakini nisikuudhi zaidi, nakusihi utusikilize maneno machache kwa fadhili zako.

5Mdo 17:6 Kwa maana tumemwona mtu huyu kuwa mkorofi, mwanzilishi wa fitina katika Wayahudi wote duniani, tena ni kichwa cha madhehebu ya Wanazareti.

6Mdo 21:28 Na tena alijaribu kulitia hekalu unajisi; tukamkamata; Wewe mwenyewe kwa kumwulizauliza utaweza kupata habari ya mambo yale yote tunayomshitaki sisi.

9Wayahudi nao wakamshitaki, wakisema ya kuwa ndivyo yalivyo.

Paulo ajitetea mbele ya Feliki

10Na mtawala alipompungia mkono ili anene, Paulo akajibu, Kwa kuwa ninajua ya kwamba wewe umekuwa mwamuzi wa taifa hili kwa muda wa miaka mingi, najitetea mwenyewe kwa moyo wa furaha.

11Mdo 21:17 Maana waweza kujua ya kuwa hazijapita siku zaidi ya kumi na mbili tangu nilipopanda kwenda Yerusalemu ili kuabudu.

12Watu hawa hawakuniona ndani ya hekalu, nikihojiana na mtu, au kufanya fujo katika mkutano, wala katika masinagogi wala ndani ya mji.

13Wala hawawezi kuyahakikisha mambo haya wanayonishitaki sasa.

14Mdo 24:5 Ila neno hili naungama kwako ya kwamba kwa Njia ile ambayo waiita uzushi, ndivyo ninavyomwabudu Mungu wa baba zetu, nikiyaamini yote yanayopatana na torati na yaliyoandikwa katika vyuo vya manabii.

15Dan 12:2; Yn 5:28,29 Nina tumaini kwa Mungu, ambalo hata hao nao wanalitazamia, ya kwamba kutakuwa na ufufuo wa wafu, wenye haki na wasio haki pia.

16Mdo 23:1 Nami ninajizoeza katika neno hili niwe na dhamiri isiyo na hatia mbele za Mungu na mbele ya watu siku zote.

17Mdo 21:17-28 Baada ya miaka mingi nilifika niwaletee watu wa taifa langu sadaka na matoleo. Rum 15:25,26; Gal 2:10

18Mdo 21:27 Wakaniona ndani ya hekalu nikishughulika na mambo haya, nilikuwa nimetakaswa, wala sikuwa na mkutano wala ghasia; lakini walikuwako baadhi ya Wayahudi waliotoka Asia,

19ambao imewapasa hao kuwapo hapa mbele yako na kunishitaki, kama wana neno lolote juu yangu.

20Au watu hawa wenyewe na waseme, ni kosa gani waliloliona kwangu niliposimama mbele ya baraza,

21Mdo 23:6 isipokuwa kwa ajili ya sauti hii moja, nilipolia nikisimama katikati yao, na kusema, Kwa ajili ya ufufuo wa wafu ninahukumiwa mbele yenu hivi leo.

22 Mdo 23:26 Basi Feliki aliwaahirisha, kwa sababu alijua habari za Njia ile kwa usahihi zaidi, akasema, Lisia jemadari atakapoteremka nitaamua kesi yenu.

23Mdo 27:3 Akamwamuru yule ofisa kwamba Paulo alindwe; ila awe na nafasi, wala asimkataze mmojawapo wa rafiki zake kumtumikia.

Paulo awekwa rumande

24Baada ya siku kadhaa, Feliki akafika pamoja na Drusila mkewe aliyekuwa Myahudi, akatuma kumwita Paulo akamsikiliza habari za imani iliyo kwa Kristo Yesu.

25Na Paulo alipokuwa akitoa hoja zake kuhusu haki, na kuwa na kiasi, na hukumu itakayokuja, Feliki akaingiwa na hofu na kusema, Sasa nenda zako, nami nikipata nafasi nitakuita.

26Pamoja na hayo alitaraji kwamba atapewa fedha na Paulo; kwa hiyo alimwita mara nyingi akaongea naye.

27Mdo 25:9 Na miaka miwili ilipotimia, Feliki akampokea Porkio Festo atawale badala yake. Na Feliki, akitaka kuwafanyia Wayahudi fadhili, akamwacha Paulo akiwa amefungwa.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help