Mwanzo 44 - Bible in Kiswahili, Revised Union Version 2013

Yusufu amweka Benyamini kizuizini

1Akamwamuru yule msimamizi wa nyumba yake akisema, Jaza magunia ya watu hawa chakula kwa kadiri wawezavyo kuchukua, utie na fedha ya kila mtu kinywani mwa gunia lake.

2Na kikombe changu, kikombe kile cha fedha, ukitie kinywani mwa gunia la yule mdogo pamoja na fedha ya nafaka yake. Akafanya kama vile alivyomwambia Yusufu.

3Asubuhi kulipopambazuka, hao watu wakapewa ruhusa, wao na punda wao.

4Na walipotoka mjini, kabla hawajaendelea sana, Yusufu akamwambia yule msimamizi wa nyumba yake, Ondoka, uwafuate watu hawa, nawe utakapowapata, waambie, Kwa nini mmelipa mabaya kwa mema?

5Je! Kikombe hiki, sicho anyweacho bwana wangu? Naye hufanya uaguzi kwacho. Mmefanya vibaya kwa kufanya hivi.

6Akawafuata, akawapata, na kuwaambia maneno hayo.

7Wakamwambia, Kwa nini bwana wangu anasema maneno kama haya? Hasha! Watumwa wako wasifanye hivi.

8Mwa 43:21 Tazama, hizo fedha mlizoziona kinywani mwa magunia yetu tumekuletea tena kutoka nchi ya Kanaani. Tuwezeje sisi kuiba nyumbani mwa Bwana wako fedha au dhahabu?

9Mwa 31:32 Atakayeonekana kuwa nacho miongoni mwa watumwa wako, na afe, na sisi nasi tutakuwa watumwa wa bwana wangu.

10Akasema, Basi na iwe hivyo kama mlivyosema, Mtu atakayeonekana kuwa nacho atakuwa mtumwa wangu, na ninyi mtakuwa hamna hatia.

11Wakafanya haraka, wakashusha kila mtu gunia lake, na kufungua kila mtu gunia lake.

12Naye akatafuta, akaanza kwa mkubwa na kuisha kwa mdogo. Kikombe kikaonekana katika gunia la Benyamini.

13Mwa 37:29,34; Hes 14:6; 2 Sam 1:11 Wakararua nguo zao, wakaweka kila mtu mzigo wake juu ya punda wake, wakarudi mjini.

14 Mwa 37:7 Akaja Yuda na ndugu zake nyumbani kwa Yusufu, naye mwenyewe alikuwamo, nao wakamwangukia kifudifudi.

15Yusufu akawaambia, Ni tendo gani hili mlilolitenda? Hamkujua ya kwamba mtu kama mimi naweza kufanya uaguzi?

16Ayu 40:4; Mwa 44:9 Yuda akasema, Tumwambie nini bwana wangu? Tusemeje! Tujivutieje haki? Mungu ameona uovu wa watumwa wako. Tazama, sisi ni watumwa wa bwana wangu, sisi na yeye ambaye kikombe kilionekana mkononi mwake.

17Yos 22:29; 1 Sam 12:23; Lk 20:16; Rum 3:4,6; 1 Kor 6:15; Gal 2:17 Akasema, Hasha! Nisifanye hivi; mtu ambaye kikombe kilionekana mkononi mwake, ndiye atakayekuwa mtumwa wangu. Nanyi nendeni zenu kwa amani kwa baba yenu.

Yuda aomba Benyamini aachiliwe

18 Mwa 18:30,32; Kut 32:22; Mit 19:12; Mwa 41:40 Ndipo Yuda akamkaribia, akasema, Tafadhali, bwana wangu, mtumwa wako na aseme neno moja masikioni mwa bwana wangu, wala hasira yako isimwakie mtumwa wako, maana wewe u kama Farao.

19Wewe, bwana wangu, ulituuliza watumwa wako, ukisema, Je! Mnaye baba, au ndugu?

20Mwa 37:3 Tukakuambia wewe, bwana wangu, Tunaye baba, naye ni mzee, na mwana wa uzee wake ni mdogo, na nduguye amekufa; amebaki yeye peke yake wa katika tumbo la mamaye, na baba yake anampenda.

21Mwa 42:15,20 Ukatuambia watumwa wako, Mleteni kwangu, ili macho yangu yamwangalie.

22Tukakuambia, bwana wangu, Kijana hawezi kumwacha babaye, maana akimwacha babaye, babaye atakufa.

23Mwa 43:3,5 Ukatuambia watumwa wako, Asiposhuka ndugu yenu mdogo pamoja nanyi, hamtaniona uso wangu tena

24Ikawa tulipokwenda kwa mtumwa wako, baba yangu, tukamwarifu maneno yako, bwana wangu.

25Mwa 43:2 Kisha baba yetu akanena, Rudini huko, mkatununulie chakula kidogo.

26Tukasema, Hatuwezi kwenda; ndugu yetu mdogo akiwapo pamoja nasi, tutashuka, maana hatutaweza kuuona uso wa mtu huyo, ndugu yetu mdogo asipokuwa pamoja nasi.

27Mwa 46:19 Mtumwa wako, baba yangu, akatuambia, Mnajua ya kuwa mke wangu alinizalia wana wawili;

28Mwa 37:33 mmoja alitoka kwangu, nikasema, Bila shaka ameraruliwa, wala sikumwona tangu hapo.

29Mwa 42:36,38 Na mkiniondolea huyu naye, na madhara yakimpata, mtashusha mvi zangu kwa msiba kaburini.

301 Sam 18:1 Basi, nikienda kwa mtumwa wako, baba yangu, na huyu kijana hayupo pamoja nasi, iwapo roho yake imeshikamana na roho ya kijana;

31itakuwa atakapoona ya kwamba huyu kijana hayuko, atakufa; na watumwa wako watashusha mvi za mtumwa wako, baba yetu, kwa huzuni kaburini.

32Mwa 43:9 Kwa maana mtumwa wako alijifanya mdhamini wa huyu kijana kwa baba yangu, nikisema, Nisipomrudisha kwako, nitakuwa na hatia kwa baba yangu daima.

33Kut 32:32 Basi, sasa nakusihi, uniache mimi mtumwa wako nikae badala ya huyu kijana kuwa mtumwa wa bwana wangu; na huyu kijana umwache aende pamoja na nduguze.

34Kwa maana nitawezaje kumwendea baba yangu, na huyu kijana hayuko pamoja nami? Nisije nikayaona mabaya yatakayompata baba yangu.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help