Yoshua Mwana wa Sira 48 - Bible in Kiswahili, Revised Union Version 2013

Eliya

1 1 Fal 17:1-24; 18:38; 19:15-16; 2 Fal 1:10-16; Mal 4:5-6 Ndipo, aliposimama Nabii Eliya, kama moto, hata na neno lake likawaka kama tanuri.

2Yeye alileta njaa juu yao, na kwa juhudi yake akawapunguzia hesabu yao;

3kwa neno la BWANA akazifunga mbingu, na mara tatu kutoka huko akateremsha moto.

4Jinsi ulivyotisha kwa miujiza yako!

Aliye mfano wako ataona fahari.

5Aliyekufa ulimfufua katika mauti,

Kutoka kuzimu, kwa neno la BWANA.

6Ukawashusha wafalme mpaka shimoni,

Na watu wateule vitandani mwao.

7Ukapaka mafuta wafalme kwa kisasi,

Na nabii ili akufuate nyuma yako.

8Ulisikia makaripio huko Sinai,

Na hukumu za kisasi huko Horebu.

9Ukachukuliwa juu katika kisulisuli,

Katika gari la farasi wa moto.

10Ukaandikiwa kuwa utaleta makemeo,

Ili kutuliza hasira siku ile ya BWANA;

Kugeuza moyo wa baba umwelekee mwana

Na kuhuisha kabila za Israeli.

11Bila shaka wamebarikiwa wale waliokuona kwa macho, wakafa; lakini wewe umezidi kubarikiwa, kwa maana unaishi.

Elisha

12 2 Fal 2:9,13 Ndiye huyo Eliya aliyefunikwa kwa kisulisuli; hata na Elisha naye akajazwa roho yake; akazidisha ishara maradufu, na yale yaliyotoka kinywani mwake yalikuwa ya ajabu. Siku zake zote huyu pia hakushawishwa kwa kumwogopa mwenye kutawala, wala hakutiishwa na mtu yeyote.

132 Fal 13:20-21 Hakukutokea neno lililokuwa gumu la kumshinda, hata na alipolala mautini mwili wake ulitoa unabii;

14kama alivyofanya miujiza katika maisha yake, kadhalika na katika mauti yake kazi zake zikawa za ajabu.

Uasi na adhabu

15 2 Fal 18:11-12 Lakini kwa ajili ya hayo yote watu hawakutubu, wala hawakuziacha dhambi zao; hata walipochukuliwa mateka kutoka nchi yao, wakatawanyika juu ya uso wa dunia yote.

16Kisha walisalia katika Yuda watu wachache sana, ila mtawala akabaki katika mbari ya Daudi. Na baadhi yao wakatenda maadili, na baadhi yao wakazidi kutenda dhambi.

Hezekia

17 2 Fal 20:20 Hezekia aliujengea mji wake maboma, akaleta maji ndani yake; akafanya kuchimba mwamba kwa chuma, akajenga visima vya kuwekea maji.

182 Fal 18:13-17 Siku zake akaja Senakeribu, akampeleka yule amiri wake; naye akauinua mkono wake juu ya Sayuni, akamkufuru Mungu katika kiburi chake.

19Basi, watu wakatikisika mioyo, wakaona maumivu kama wanawake waonavyo uchungu;

202 Fal 19:15-20,35 wakamwita Mungu Aliye Juu, wakimnyoshea mikono yao; naye akawasikia hima kutoka mbinguni, akawaokoa kwa mkono wa Isaya.

21Aliipiga kambi ya Waashuri,

Na malaika wake akawaangamiza.

Isaya

22Maana Hezekia alifanya mapenzi ya BWANA,

Akawa hodari katika njia za Daudi.

Ambazo Nabii Isaya aliziamuru,

Aliyekuwa mkuu na amini katika njozi;

23 2 Fal 20:10-11 Katika siku zake jua likarudi nyuma,

Hata akayaongeza maisha ya mfalme.

24Huyo aliona kwa roho ya nguvu mambo ya mwisho; akawafariji wale walioomboleza katika Sayuni.

25Akaonesha mambo yatakayokuwako hata mwisho wa nyakati, na mambo yaliyofichwa kabla hayajatokea.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help