Isaya 43 - Bible in Kiswahili, Revised Union Version 2013

Ahadi ya matengenezo na ulinzi

1 Isa 44:6; 42:6; 1 Kor 1:9; 2 Tim 1:9 Lakini sasa, BWANA aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu.

2Zab 66:12; Kum 31:6-8; Dan 3:25 Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.

3Mit 21:18 Maana mimi ni BWANA, Mungu wako; Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako, nimetoa Misri kuwa ukombozi wako; nimetoa Kushi na Seba kwa ajili yako.

4Kut 19:5,6 Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na makabila ya watu kwa ajili ya maisha yako.

5Isa 41:10,14; 44:2 Usiogope; maana mimi ni pamoja nawe; nitaleta wazao wako toka mashariki, nitakukusanya toka magharibi;

6nitaiambia kaskazi, Toa; nayo kusi, Usizuie; waleteni wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia.

7Isa 63:19; 29:23; Zab 100:3; Yn 3:3; 2 Kor 5:17; Efe 2:10 Kila mmoja aliyeitwa kwa jina langu, niliyemwumba kwa ajili ya utukufu wangu; mimi nimemwumba, naam, mimi nimemfanya.

8Isa 6:9; 42:19 Walete watu wasioona, japo wana macho, wasiosikia japo wana masikio.

9Na wakusanyike mataifa yote, kabila zote wakutanike; ni nani miongoni mwao awezaye kuhubiri neno hili, na kutuonesha mambo ya zamani? Na walete mashahidi wao, wapate kuhesabiwa kuwa na haki; au na wasikie, wakaseme, Ni kweli.

10Yn 1:7; Mdo 1:8; Ebr 12:1; Ufu 1:5; Isa 44:8; 41:8 Ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, na mtumishi niliyemchagua; mpate kujua, na kuniamini, na kufahamu ya kuwa mimi ndiye; kabla yangu hakuumbwa Mungu awaye yote, wala baada yangu mimi hatakuwapo mwingine.

11Mimi, naam, mimi, ni BWANA, zaidi yangu mimi hapana mwokozi.

12Kum 32:16 Nimetangaza habari, nimeokoa, nimeonesha, na hapakuwa mungu wa kigeni kati yenu; kwa sababu hiyo ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, nami ni Mungu.

13Zab 90:2; Mit 8:23; Mik 5:2; Mt 19:26 Naam, tangu siku ya leo, mimi ndiye; wala hakuna awezaye kuokoa katika mkono wangu; mimi nitatenda kazi, naye ni nani awezaye kuizuia?

14BWANA, Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Kwa ajili yenu nimetuma ujumbe Babeli nami nitawashusha wote mfano wa wakimbizi, naam, Wakaldayo, katika merikebu zao walizozifurahia.

15Hos 13:10 Mimi ni BWANA, Mtakatifu wenu, Muumba wa Israeli, mfalme wenu.

16Zab 77:19 BWANA asema hivi, yeye afanyaye njia katika bahari; na mahali pa kupita katika maji yenye nguvu;

17Kut 14:4 atoaye gari na farasi, jeshi la askari na uwezo; wamelala, hawataondoka; wametoweka, wamezimwa kama utambi.

18Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani.

192 Kor 5:17; Ufu 21:5 Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani.

20Isa 48:21; Lk 1:74; Efe 1:5 Wanyama pori wataniheshimu, mbweha pia na mbuni; kwa sababu nimewapa maji jangwani, na mito nyikani, ili kuwanywesha watu wangu, wateule wangu;

21watu wale niliojiumbia nafsi yangu, ili wazitangaze sifa zangu.

22Mal 1:13 Lakini hukuniita, Ee Yakobo, bali umechoka nami, Ee Israeli.

23Hukuniletea wana-kondoo kuwa kafara zako, wala hukuniheshimu kwa dhabihu zako. Sikukutumikisha kwa matoleo, wala sikukuchosha kwa ubani.

24Isa 1:14; Mal 2:17; Yud 1:4 Hukuninunulia manukato kwa fedha, wala hukunishibisha kwa mafuta ya sadaka zako; bali umenitumikisha kwa dhambi zako, umenichosha kwa maovu yako.

25Isa 44:22; Yer 31:34; Mik 7:18,19; Eze 36:22 Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako.

26Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako.

27Rum 5:12 Baba yako wa kwanza alifanya dhambi, na wakalimani wako wameniasi.

28Isa 47:6; Omb 2:2; Zab 79:4; Yer 24:9; Dan 9:11; Zek 8:13 Kwa hiyo nitawatia unajisi wakuu wa patakatifu, nami nitamfanya Yakobo kuwalaani, na Israeli kuwa tukano.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help