Ufunuo 15 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Malaika saba na mapigo saba

1Ndipo nikaona ishara nyingine kubwa ya ajabu mbinguni: malaika saba wenye yale mapigo saba ya mwisho, kwa sababu kwa mapigo hayo ghadhabu ya Mungu ilikuwa imekamilika.

2Nikaona kile kilichoonekana kama bahari ya kioo iliyochanganyikana na moto. Kando ya hiyo bahari, walikuwa wamesimama wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake pamoja na tarakimu ya jina lake. Mikononi mwao walikuwa wameshika vinubi walivyopewa na Mungu.

3Nao wakaimba wimbo wa Musa, mtumishi wa Mungu, na wimbo wa Mwana-Kondoo, wakisema:

“Bwana Mungu Mwenyezi,

matendo yako ni makuu na ya ajabu.

Njia zako wewe ni za haki na za kweli,

Mfalme wa nyakati zote!

4Ni nani ambaye hatakuogopa wewe Mwenyezi Mungu

na kulitukuza jina lako?

Kwa kuwa wewe peke yako ndiwe mtakatifu.

Mataifa yote yatakuja

na kuabudu mbele zako,

kwa kuwa matendo yako ya haki

yamedhihirishwa.”

5Baada ya haya nikatazama, nalo Hekalu la Hema la Ushuhuda lilikuwa limefunguliwa mbinguni.

6Ndani ya lile Hekalu wakatoka malaika saba wakiwa na mapigo saba. Walikuwa wamevaa nguo safi za kitani iliyong’aa, na kufungwa mikanda ya dhahabu vifuani mwao.

7Ndipo mmoja wa wale viumbe wanne wenye uhai akawapa wale malaika saba mabakuli saba ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, yeye aishiye milele na milele.

8Nalo lile Hekalu lilijawa na moshi uliotokana na utukufu wa Mungu na uweza wake, wala hakuna yeyote aliyeweza kuingia mle Hekaluni hadi yale mapigo saba ya wale malaika saba yalipomalizika.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help