Zaburi 84 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Zaburi 84Kuionea shauku nyumba ya Mwenyezi MunguKwa mwimbishaji. Mtindo wa gitithi. Zaburi ya wana wa Kora.

1Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni,

makao yako yapendeza kama nini!

2Nafsi yangu inatamani sana,

naam, hata kuona shauku,

kwa ajili ya nyua za Mwenyezi Mungu;

moyo wangu na mwili wangu

vinamlilia Mungu Aliye Hai.

3Hata shomoro amejipatia makao,

mbayuwayu amejipatia kiota

mahali awezapo kuweka makinda yake:

mahali karibu na madhabahu yako,

Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni,

Mfalme wangu na Mungu wangu.

4Heri wale wanaokaa nyumbani mwako,

wanaokusifu wewe daima.

5Heri wale ambao nguvu zao ziko kwako,

na njia ziendazo Sayuni zimo mioyoni mwao.

6Wanapopita katika Bonde la Baka,

hulifanya mahali pa chemchemi,

pia mvua za vuli hulijaza kwa madimbwi.

7Huendelea toka nguvu hadi nguvu,

hadi kila mmoja afikapo

mbele za Mungu huko Sayuni.

8Ee Bwana Mwenyezi Mungu,

Mungu wa majeshi ya mbinguni,

sikia maombi yangu;

nisikilize, Ee Mungu wa Yakobo.

9Ee Mungu, uitazame ngao yetu,

mtazame kwa wema mpakwa mafuta wako.

10Siku moja katika nyua zako ni bora

kuliko siku elfu mahali pengine;

afadhali ningekuwa bawabu katika nyumba ya Mungu wangu

kuliko kukaa katika mahema ya waovu.

11Kwa kuwa Bwana Mwenyezi Mungu ni jua na ngao;

Mwenyezi Mungu hutoa wema na heshima;

hakuna kitu chema anachowanyima

wale ambao hawana hatia.

12Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni,

heri mtu anayekutumaini wewe.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help