Hosea 9 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Adhabu kwa Israeli

1Usifurahie, ee Israeli;

usishangilie kama mataifa mengine.

Kwa kuwa hukuwa

mwaminifu kwa Mungu wako;

umependa ujira wa kahaba kwenye kila sakafu

ya kupuria nafaka.

2Sakafu za kupuria nafaka na mashinikizo ya kukamulia divai

havitalisha watu,

divai mpya itawapungukia.

3Hawataishi katika nchi ya Mwenyezi Mungu,

Efraimu atarudi Misri

na atakula chakula

kilicho najisi huko Ashuru.

4Hawatammiminia Mwenyezi Mungu sadaka ya divai

wala dhabihu zao hazitampendeza.

Dhabihu kama hizo zitakuwa kwao

kama mkate wa waombolezaji;

nao wote wazilao watakuwa najisi.

Chakula hiki kitakuwa kwa ajili yao wenyewe;

kisije katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.

5Mtafanya nini katika siku ya sikukuu zenu zilizoamriwa,

katika siku za sikukuu za Mwenyezi Mungu?

6Hata ikiwa wataokoka maangamizi,

Misri atawakusanya,

nayo Memfisi itawazika.

Hazina zao za fedha zitasongwa na michongoma,

nayo miiba itafunika mahema yao.

7Siku za adhabu zinakuja,

siku za malipo zimewadia.

Israeli na afahamu hili.

Kwa sababu dhambi zenu ni nyingi sana

na uadui wenu ni mkubwa sana,

nabii anadhaniwa ni mpumbavu,

mtu aliyeongozwa na Mungu

anaonekana mwendawazimu.

8Nabii, pamoja na Mungu wangu,

ndiye mlinzi juu ya Efraimu,

hata hivyo mitego inamngojea

katika mapito yake yote,

na uadui katika nyumba ya Mungu wake.

9Wamezama sana katika rushwa,

kama katika siku za Gibea.

Mungu atakumbuka uovu wao

na kuwaadhibu kwa ajili ya dhambi zao.

10“Nilipompata Israeli, ilikuwa kama

kupata zabibu jangwani;

nilipowaona baba zenu, ilikuwa kama kuona

matunda ya kwanza katika mtini.

Lakini walipofika Baal-Peori, walijiweka wakfu

kwa ile sanamu ya aibu,

nao wakawa najisi

kama kitu kile walichokipenda.

11Utukufu wa Efraimu utaruka kama ndege:

hakuna kuzaa, hakuna kubeba mimba,

hakuna kuchukua mimba.

12Hata wakilea watoto,

nitamuua kila mmoja.

Ole wao

nitakapowapiga kisogo!

13Nimemwona Efraimu, kama Tiro,

aliyeoteshwa mahali pazuri.

Lakini Efraimu wataleta

watoto wao kwa mchinjaji.”

14Wape, Ee Mwenyezi Mungu,

je, utawapa nini?

Wape tumbo zinazoharibu mimba

na matiti yaliyokauka.

15“Kwa sababu ya uovu wao wote huko Gilgali,

niliwachukia huko.

Kwa sababu ya matendo yao ya dhambi,

nitawafukuza katika nyumba yangu.

Sitawapenda tena,

viongozi wao wote ni waasi.

16Efraimu ameharibiwa,

mzizi wao umenyauka,

hawazai tunda.

Hata kama watazaa watoto,

nitawachinja wazao wao

waliotunzwa vizuri.”

17Mungu wangu atawakataa

kwa sababu hawakumtii;

watakuwa watu wa kutangatanga

miongoni mwa mataifa.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help