1Mwenyezi Mungu akaniambia, “Chukua kitabu kikubwa, uandike kwa kalamu ya kawaida jina: Maher-Shalal-Hash-Bazi.
2Nami nitawaita kuhani Uria, na Zekaria mwana wa Yeberekia kama mashahidi wangu waaminifu.”
3Kisha nikaenda kwa nabii mke, naye akapata mimba, akazaa mwana. Kisha Mwenyezi Mungu akaniambia, “Mwite huyo mtoto Maher-Shalal-Hash-Bazi.
4Kabla mtoto hajaweza kusema ‘Baba yangu’ au ‘Mama yangu,’ utajiri wa Dameski na nyara za Samaria zitachukuliwa na mfalme wa Ashuru.”
5Mwenyezi Mungu akasema nami tena:
6“Kwa sababu watu hawa wamekataa maji ya Shilo yanayotiririka taratibu
wakamfurahia Resini na mwana wa Remalia;
7kwa hiyo Bwana yu karibu kuleta dhidi yao
mafuriko makubwa ya Mto:
yaani mfalme wa Ashuru na fahari yake yote.
Yatafurika juu ya mifereji yake yote,
yatamwagikia juu ya kingo zake zote,
8na kufika hadi Yuda, yakizunguka kwa kasi juu yake,
yakipita katikati na yakifika hadi shingoni.
Mabawa yake yaliyokunjuliwa
yatafunika upana wa nchi yako,
Ee Imanueli!”
9Inueni ukelele wa vita, enyi mataifa,
na mkavunjwevunjwe!
Sikilizeni, enyi nyote nchi za mbali.
Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe!
Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe!
10Wekeni mikakati yenu, lakini itashindwa;
fanyeni mipango yenu, lakini haitafanikiwa,
kwa maana Mungu yu pamoja nasi.
11Mwenyezi Mungu alisema nami mkono wake wenye nguvu ukiwa juu yangu, akinionya nisifuate njia za taifa hili. Akasema:
12“Usiite fitina kila kitu ambacho watu hawa hukiita fitina,
usiogope kile wanachokiogopa,
wala usikihofu.
13Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndiye peke yake
ikupasaye kumheshimu kuwa mtakatifu,
ndiye peke yake utakayemwogopa,
ndiye peke yake utakayemhofu,
14naye atakuwa mahali patakatifu;
lakini kwa nyumba zote mbili za Israeli atakuwa
jiwe lile linalosababisha watu kujikwaa
na mwamba wa kuwaangusha.
Kwa watu wa Yerusalemu,
atakuwa mtego na tanzi.
15Wengi wao watajikwaa;
wataanguka na kuvunjika,
watategwa na kunaswa.”
16Funga ushuhuda na kutia muhuri sheria
miongoni mwa wanafunzi wangu.
17Nitamngojea Mwenyezi Mungu,
ambaye ameificha nyumba ya Yakobo uso wake.
Nitaliweka tumaini langu kwake.
18Niko hapa, pamoja na watoto ambao Mwenyezi Mungu amenipa. Sisi ni ishara na mfano wake katika Israeli, kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, anayeishi juu ya Mlima Sayuni.
19Watu wanapowaambia ninyi kutafuta ushauri kwa waaguzi na wenye kuongea na mizimu, ambao hunong’ona na kunung’unika, je, watu wasingeuliza kwa Mungu wao? Kwa nini watake shauri kwa wafu kwa ajili ya walio hai?
20Kwa sheria na kwa ushuhuda! Kama hawatasema sawasawa na neno hili, hawana mwanga wa mapambazuko.
21Watazunguka katika nchi yote, wakiwa na dhiki na njaa. Watakapotaabika kwa njaa, watapatwa na hasira kali, nao, wakiwa wanatazama juu, watamlaani mfalme wao na Mungu wao.
22Kisha wataangalia duniani na kuona tu dhiki na giza, hofu na huzuni tupu, nao watasukumiwa kwenye giza nene kabisa.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.